Kufuatia agizo
la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli la
kuhakiki watumishi wa Umma nchini, Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umebaini watumishi
hewa 33 na watoro 29 kati ya watumishi 13,174 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za
Serikali kuu.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari jana mara baada kikao cha kutathmini hali ya Watumishi
katika Mkoa , Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony J. Mtaka alisema uwepo wa
watumishi hewa na watoro umeisababishia Serikali hasara ya shilingi
320,993,683.69 .
Mtaka alisema
mara baada ya kubaini uwepo wa watumishi
watoro, amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kusimamisha mishahara ya watumishi hao wakiwemo
walimu ambao walikwenda masomoni bila ruhusa ya waajiri wao na wale ambao
mashauri yao yapo kwa muda mrefu katika Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD) mpaka
mashauri hayo yatakapopatiwa ufafanuzi.
Kutokana na idadi ya watumishi wa kada ya
ualimu kuwa kubwa katika watumishi hewa na watoro kuliko kada zingine, Uongozi
wa Mkoa wa Simiyu umeshauri Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD) kushughulikia kwa
haraka mashauri ya walimu yanayopelekwa kutoka ngazi za Wilaya na Mikoa na
kutoa ufafanuzi kwa wakati, ili kuondokana hasara ya kulipa mishahara hewa.
Aidha , Uongozi
wa Mkoa umeshauri Ofisi ya HAZINA na Utumishi kuona namna ya kugatua madaraka kutoka
Ofisi kuu kwenda Ofisi za kanda na mikoa, ili pale mtumishi anapotakiwa
kusimamishiwa mshahara wake anapostaafu,kufariki au kufukuzwa kazi iwe rahisi
kuwaondoa katika mfumo wa mishahara badala ya kusubiri Ofisi kuu Dar es Salaam
kuwatoa kwenye mfumo wa mishahara.
Hali ya
watumishi watoro katika Mkoa wa Simiyu inaongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya
Meatu yenye watumishi watoro 18, hewa mmoja (01), ikifuatiwa na Halmashauri ya
Wilaya ya Bariadi yenye watumishi watoro 11, hewa watano (05), huku Halmashauri
ya Mji wa Bariadi ikiwa na watumishi hewa watano (05), Itilima sita (06),
Busega wanne na Maswa 12 ambapo Halmashauri hizi nne (04) hazina watumishi
watoro.
0 comments:
Post a Comment