Thursday, April 7, 2016

SIMIYU KUPATA MASAFA YA UTANGAZAJI


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ameahidi kushughulikia na kuhakikisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  inatoa masafa kwa ajili ya utangazaji kwa  Mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bibi.. Mwamvua Jilumbi (kulia) akisoma taarifa ya Mkoa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape M. Nnauye (kushoto) wakati wa ziara yake mkoani Simiyu jana, (katikati) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka.


Mhe. Nape aliyasema hayo jana wakati alipozungumza na wadau wa Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo wa Mkoa wa Simiyu katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wakati wa Ziara yake ya siku moja Mkoani humo.

Nape alisema  mara masafa hayo yatakapotangazwa katika Mkoa wa Simiyu, Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo wanzishe redio zao ili kuwawezesha kutoa taarifa mbalimbali za utendaji wa Serikali na kuzifanya kuwa vyanzo vya mapato katika Halmashauri zao.

“Katibu Tawala Mkoa wahamasishe wakurugenzi wa Halmashauri zako kuanzisha vituo vya redio, kila nilipopita nikakuta Halmashauri ina kituo cha redio wako mbali sana”, alisema Nape.

Akisoma taarifa ya Mkoa kwa Mhe. Waziri, Katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Mwamvua Jilumbi alisema Mkoa wa Simiyu una kituo kimoja cha Redio SIBUKA ambacho hurusha matangazo yake kutoka wilayani Maswa.

Wakati huo huo Waziri Nape Nnauye aliagiza Halmashauri ambazo hazina Maafisa Habari waajiri na wale walio nao wahakikishe Maafisa Habari wanaingia katika vikao vya maamuzi ili wawe na taarifa za kutosha hali itakayowajengea uwezo wa kuzisemea Halmashauri na Mkoa kwa usahihi.

Aidha, amesisitiza uongozi wa Mkoa kupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mkoa, kuimaarisha vyama vya  michezo na kuvisaidia kupata viongozi bora watakaosaidia kuendeleza michezo yote ndani ya mkoa.

Sambamba na kuimarisha vyama vya michezo Mhe. Nape alieleza azma ya Serikali katika kurasimisha shughuli za sanaa, ambapo kwa kufanya hivyo kutawasaidia wasanii kupata kipato.


Waziri Nape alifanya ziara ya siku moja mkoani Simiyu akitokea Mkoani Geita, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea mikoa mipya na mikoa ya pembezoni ili kujionea changamoto mbalimbali za sekta ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!