Viongozi wa jeshi la
Polisi Mkoa wa Simiyu wameaswa kuwawajibisha askari polisi watakaokiuka maadili
ya kazi yao ikiwemo kutoa siri za jeshi la polisi kwa wahalifu.
Hayo yamesemwa na Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka alipozungumza na Viongozi na Askari
wa Jeshi la Polisi Mkoani Simiyu jana, katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bariadi
Mjini Bariadi, katika kikao cha kujitambulisha na kutoa maelekezo ya Serikali
kwa Jeshi la polisi.
Mtaka amesema viongozi
hao wasisite kuwawajibisha askari watakaoonekana kuvujisha siri za jeshi hilo
kwa kuwa kufanya hivyo kunalifedhehesha Jeshi la Polisi.
“Hatuwezi kukukubali
kudhalilisha taaluma ya jeshi la polisi, hivi askari anayetoa siri za jeshi OCD unamwangalia wa nini, hii ni fedheha. Jeshi la
Polisi linaonekana la ovyo kwa sababu ya askari wachache wasiotaka kutii na kufuata maadili; raia anashindwa kutoa
taarifa katika chombo cha dola kwa sababu anaogopa chombo cha dola kitamuuza,
aibu hii haivumiliki wachukulieni hatua” alisema Mtaka.
Aidha, Mkuu huyo wa
Mkoa amewataka viongozi wa Jeshi la
Polisi kufanya kazi kwa bidii na kusimamia haki ili askari watekeleze majukumu
yao sawa sawa.
Pamoja na kuwaasa Mtaka
alitoa pongezi kwa jeshi la polisi kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika
maeneo tofauti ya mkoa wa Simiyu ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuwakamata
majangili waliotungua helikopta wilayani Meatu ,kufanya oparesheni za
kuteketeza mashamba ya bangi na kazi nyingine za ulinzi na usalama wa raia na
mali zao.
Kwa upande wake Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ASP. Onesmo Lyanga, alisema hatasita kuwachukulia
hatua viongozi na askari wa jeshi la
polisi wababaishaji, hivyo akawataka wafanye kazi zao kwa bidii.
Is the Sumiyu RPC having a rank of an ASP or ACP?
ReplyDelete