Sunday, April 24, 2016

RC SIMIYU: WATENDAJI MWIBA HOLDINGS LIMITED, MARUFUKU KUWAHOJI WANANCHI KATIKA OFISI ZAO





Mkuu  wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka amepiga marufuku tabia ya askari na watendaji  wengine wa  mwekezaji MWIBA Holdings  Limited wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao wilayani Meatu, ya kuwakamata wananchi na kuwafanyia mahojiano katika Ofisi zao , na kuwataka kufuata sheria na kukitumia kituo cha polisi cha Makao kufanya mahojiano.

Mwenyekiti wa kijiji cha Makao na Diwani wa kata ya Mwangudo Mhe. .Anthony Philipo (kushoto) akiwasilisha malalamiko yake dhidi ya Mwekezaji MWIBA Holdings kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka (kulia) katika mkutano wa hadhara ambao ulifanyika katika kijiji cha Makao  hivi karibuni. Picha na Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa aliyasema hayo jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Makao kata ya Mwangudo wilayani Meatu katika mkutano wa hadhara, mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao dhidi ya Mwekezaji MWIBA Holdings Limited, ikiwemo unyanyasaji wa wananchi, kukiukwa kwa makubaliano ya mikataba ya utwaaji ardhi na mkataba wa uanzishwaji wa Lanchi.

Akiwasilisha malalamiko yake kwa Mkuu wa Mkoa mmoja wa wananchi wanaodaiwa  kupigwa na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji  katika ofisi za MWIBA Holdings Limited, Bibi. Asteria Godson mkazi wa kijiji cha Makao alisema, alichukuliwa nyumbani kwake na kupelekwa katika moja ya ofisi za mwekezaji huyo ambako alipigwa na kusababishiwa maumivu makali na kuvunjika mkono wa kulia ambao hadi sasa hata baada ya kupata matibabu, bado hauwezi kufanya kazi sawasawa.

“Mimi nilikuwa nimelala ndani kwangu wakaingia watu ambao sikuweza kuwatambua wakitaka niwaeleze mahali alipo mume wangu, nikawaambia mume wangu hayupo wakaanza kunipiga, walinipiga baadae wakanichukua mpaka ofisi za MWIBA huko nako walinipiga na kunifanyia vitendo vingi vya unyanyasaji. Kutokana na kile kipigo sasa hivi mkono wangu mmoja haufanyi kazi”alisema Asteria.

 Akipokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa, Afisa  Uhusiano wa MWIBA Holdings Limited Bwana Msafiri Clarenes alisema wamekubali na watatekeleza kama ilivyoelekezwa, ambapo alimuomba Mkuu wa Mkoa atoe maelekezo kwa wananchi wa Mako kuacha kuchungia mifugo katika eneo la uwekezaji.

Katika kukabiliana na tatizo la eneo la malisho ya mifugo, Mtaka alisema Serikali iliweka mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao unaeleza kuwa litatengwa eneo maalum kwa ajili ya machungo ambalo litatumika kipindi ambacho majani yatakuwa yamepungua kuanzia mwezi Julai hadi mvua zitakapoanza kunyesha.

Akitoa ufafanuzi juu ya eneo la kulishia mifugo Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Bwana Emmanuel Lugamila alisema, eneo hilo lipo ndani ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao na linatarajiwa kuwekewa alama za kudumu mwezi Juni,2016 ili wananchi waweze kulitambua.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amewaasa wananchi kuachana na tabia ya kupangisha mifugo ambayo ni maarufu katika Maeneo hayo kama LUBAGA, kwa kuwa ni chanzo cha migogoro kati ya wafugaji, badala yake viongozi wa vijiji wawatambue watu wenye mifugo katika maeneo yao na kuepuka kwenda katika maeneo ambayo hawaruhusiwi kuchungia.

Wananchi wa kijiji cha Makao wamekuwa na Mgogoro wa kimkataba na Mwekezaji MWIBA Holdings Limited ambao  unaendelea kutafutiwa suluhu kwa mujibu wa sheria.   

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!