Naibu
Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe.
Luhaga Mpina amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua
viongozi wanaoshindwa kusimamia utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli la kufanya usafi wa Mazingira
kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Mhe.
Mpina aliyasema hayo alipozungumza na viongozi na wananchi mara baada ya kushiriki
kufanya usafi katika kituo cha Afya cha Mwandoya wilayani Meatu, zoezi ambalo
lilienda sambamba na uzinduzi wa upandaji wa miti ya matunda katika mkoa wa
Simiyu, ambapo Mkoa wa Simiyu umepokea jumla ya miche 18, 400 ya miembe na
michungwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mpina
alisema viongozi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Mkoa wanao wajibu wa kusimamia
usafi wa mazingira katika maeneo yao, kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa kuhakikisha
wananchi wanafanya usafi kuanzia saa 12:00 hadi saa 3:00 asubuhi, ikiwa kuna wananchi
watakaobainika kushindwa kutekeleza agizo hilo wachukuliwe hatua.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe. Pius Machungwa alisema viongozi wa
Wilaya ya Meatu na mkoa wa Simiyu kwa ujumla wataendelea kuunga mkono juhudi za
serikali katika kuhakikisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira
zinaendelezwa.
Wakati
huo huo Mhe. Mpina amewahimiza wananchi kupanda miti yenye manufaa , hususani
miti ya mbao na matunda kwa sababu itawasidia kupata fedha, chakula na
malighafi kwa ajili ya viwanda mbalimbali nchini na hivyo kuinua uchumi wa
mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu , Bw. Joseph S. Nandrie alikiri mkoa
kupokea jumla ya miche ya miembe na machungwa 18,400 ambayo imeshasambazwa katika
Halmashauri zote sita na akaahidi kuifuatilia miti hiyo na kuhakikisha
inatunzwa.
Aidha
Mpina alieleza azma ya Serikali katika kuhakikisha miti inapandwa nchi nzima
ili kurejesha uoto wa asili uliopotea, kuongeza uwezo wa kunyonya hewa ya ukaa
ambayo imeongezeka duniani kote kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumeandaa
Mpango wa kitaifa wa upandaji wa miti, na kwa kuanzia tumetenga shilingi bilioni
20 kwa mwaka kwa ajili ya upandaji miti nchi nzima, kwa kupanga huko tunataka kila
wilaya iwe na kitalu kikubwa cha miti inayoandaliwa kwenda kwa wananchi kwa
urahisi. Tunataka kufikia mwaka 2020 watu wakose mahali pa kupanda miti kwa kuwa
kila mahali patakuwa na miti” alisema Mpina.
Mhe.
Mpina alitoa miche hiyo 18,400 kwa Mkoa wa Simiyu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi
aliyoitoa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa , aliyoifanya
Mkoani Simiyu mapema mwezi Machi, 2016 na ameahidi kuongeza miche hadi kufikia
30,000.
0 comments:
Post a Comment