Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe. Anthony Mtaka, ametoa siku tano kwa Mtaalam Mshauri wa Mradi wa Ujenzi wa
Barabara za Halmashauri ya Mji wa Bariadi (NOR PLAN) kuwasilisha mapitio ya
Mchanganuo wa Gharama (BOQ) ya Ujenzi wa barabara hizo katika Ofisi yake.
Mtaka alitoa agizo hilo
jana wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara
aliyoifanya katika Halmashauri ya Mji Bariadi, akiambatana na Wajumbe wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya
Bariadi.
Mtaka alisema ipo haja kwa Uongozi wa Mkoa
kuona mapitio hayo ili Ofisi ya Mkoa na watendaji wengine wayapitie na kuona
kama kuna vitu ambavyo si vya msingi au vyenye gharama kubwa wamshauri Mtaalam
mshauri na Mkandarasi kuviondoa ili kupunguza gharama ya mradi huo uliopangwa
kutekelezwa kwa shilingi bilioni 9.1 kwa kilomita 6.
“Katibu Mkuu TAMISEMI
alipokuja alikuagiza ufanye review ya BOQ na akataka uanishe kiasi gani cha
fedha kitaokolewa . Nakala hiyo tunapaswa tuipate sisi kama viongozi wa mkoa,
naagiza uilete hiyo review Ijumaa saa 4:00 asubuhi, halafu Katibu Tawala Mkoa atakaa na Wataalam wa
Sekretarieti na wadau wengine ambao kwa
pamoja watashauri nini kifanyike”alisema Mtaka.
Aidha, baada ya
Mhandisi wa Mkandari wa Mradi, Jassie And Company Ltd (JASCO), Ndg. Daniel Nila
kueleza kuwa gharama za ujenzi wa barabara hizo zilipangwa kuwa shilingi
bilioni 1.3 kwa kilomita moja, kutokana
na barabara hiyo kupangwa kujengwa kwa hadhi ya barabara ya uwanja wa ndege;
Mkuu wa mkoa aliwashauri kuangalia mazingira ya Mji wa Bariadi na kujenga
barabara inayoendana na mazingira ili kupunguza gharama zisizo za lazima.
Sanjari na hilo Mkuu wa
mkoa alitoa wito kwa Wakandarasi wazawa wanaopewa dhamana ya kutekeleza miradi
ya Serikali, kuweka uzalendo mbele na kutekeleza miradi kwa kiwango.
Kwa upande wake
Mhandisi Victor Malya kutoka Kampuni ya NOR PLAN (Mtaalam Mshauri wa Mradi), alisema
tangu Mradi wa ujenzi wa barabara za Mji Bariadi uanze kutekelezwa mwezi
Agosti, 2015 hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 50, ulitarajiwa kukamilishwa
mwezi Agosti 2016 lakini kutokana na
sababu mbalimbali ikiwepo mvua kubwa iliyonyesha mwezi Novemba na Desemba mradi
huo hautaweza kukamilika ndani ya muda uliopangwa katika mkataba.
Pamoja na maelezo hayo
kutoka kwa Mhandisi Malya, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alimtaka Mkandarasi wa mradi
huo (JASCO) kuongeza kasi ya utekelezaji
kufikia mwezi Oktoba mradi uwe umetekelezwa
kwa asilimia kubwa ili barabara hizo zikatumiwe na viongozi na wananchi wakati
wa maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016, kwa sababu
kama zitakuwa zimefungwa kama ilivyo
sasa zitasababisha usumbufu.
0 comments:
Post a Comment