Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka ameiagiza Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Wilaya ya Bariadi kumpelekea taarifa ya miradi ya maji
inayotiliwa shaka ya kujengwa chini ya kiwango, ndani ya siku tano kuanzia tarehe 04.05.2016.
Mtaka alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri
ya Wilaya ya Bariadi, katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Bariadi.
“Siwezi kuvumilia na kuendelea kuona fedha za
Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na miradi mingine
kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zinatumika vibaya au miradi ya maendeleo
kutekelezwa chini ya kiwango. DC na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama nataka
uniletee taarifa ya miradi yote ya maji katika wilaya ya Bariadi inayotiliwa
shaka ya kutekelezwa chini ya kiwango,Jumatatu asubuhi, ili tuchukue hatua”
alisema Mtaka.
Mtaka aliwataka viongozi na watendaji kila mmoja kutimiza
wajibu wake katika kusimamia na kuhakikisha miradi yote ya Serikali inatekelezwa
kwa kiwango, kulingana na thamani ya fedha
ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alisema
hatasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kuhusika kwa namna moja
ama nyingine katika utekelezaji wa miradi hiyo chini ya kiwango hata kama ni
kada wa Chama Tawala, kwa sababu amedhamiria kutekeleza ilani ya Chama cha
Mapinduzi ambacho kimeaminiwa na kupewa ridhaa ya kuongoza nchi na wananchi
wenyewe, ambapo aliahidi atasimamia ipasavyo ili wananchi waendelee kukiamini
Chama cha Mapinduzi na Serikali yake.
0 comments:
Post a Comment