Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka jana amezindua Kamati ya Mkoa ya Baraza la Ushauri
la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na
Nishati (EWURA) ya mkoa huo.
Akizungumza na
wajumbe wa Kamati ya Baraza hilo na wadau walioshiriki katika hafla ya uzinduzi
, iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mtaka alisema kamati ya
baraza hilo inapaswa kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi
ya watumiaji wa huduma za nishati na maji, hasa upatikanaji na uboreshaji ili huduma hizo ziendane na thamani ya fedha
wanazotoa watumiaji.
Mtaka alisema
wajumbe wa kamati ya baraza la ushauri la watumia huduma za EWURA, wanao wajibu
wa kuelimisha na kusambaza taarifa sahihi kwa watumiaji wa huduma za nishati na
maji ili wajue masuala yanayowahusu hususani haki na wajibu wao.
“Mwenyekiti kamati
yako itoe taarifa za mara kwa mara kwa watumiaji wa huduma za nishati na maji
hasa yanapotokea mabadiliko kama kupanda au kushuka kwa bei ya maji , mafuta na
umeme, kukatika kwa maji au umeme na taarifa nyingine muhimu kwa watumiaji wa
huduma hizi ili wawe na ufahamu wa kutosha”, alisema Mtaka.
Aliahidi kuwa Serikali ya Mkoa na vyombo vyake
itashirikiana na Kamati ya baraza hili la Mkoa katika kuwajengea mazingira
mazuri ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano na kuhakikisha
malengo ya kuanzishwa kwake yanafanikiwa.
Aidha, Mkuu huyo
wa Mkoa aliwataka wafanyabiashara wa mafuta kuwashushia bei wananchi pale
inapotokea bei za bidhaa hiyo kupungua katika soko badala ya kuendelea
kuwaumiza kwa kisingizio cha kutopunguza bei kwa kuwa walichukua mzigo wakati
bei ikiwa juu.
Kamati ya Mkoa
ya Baraza la Ushauri la Watumia huduma zinazodhibitiwa na EWURA Mkoa wa Simiyu
inaundwa na wajumbe watano: Suzan Sabuni (Mwenyekiti), Kubagwa
Madabila(Katibu), Kulwa Mtebe (Mtunza Hazina), Magreth Kayanda (Mjumbe) na
Martha Zongo (Mjumbe).
0 comments:
Post a Comment