Friday, February 22, 2019

WADAU WAIOMBA EWURA KUWASAIDIA WANANCHI WANAOTUMIA CHUPA ZA MAJI KUSAFIRISHA MAFUTA

Wadau wa Nishati na Maji  mkoani Simiyu wameiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi wanaotumia   chupa za maji kusafirisha  mafuta vijijini na badala yake watafute njia mbadala ili kuepusha majanga ya moto na uchakachuaji wa nishati hiyo.


Wadau hao wametoa ushauri huo katika mkutano baina ya watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) uliolenga  kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo, uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.

Wakizungumza katika mkutano huo wamesema kutokuwepo vyombo maalum vya  ubebaji wa mafuta ya taa , petroli na diseli ni Moja ya tatizo kubwa, hivyo ni vema  (EWURA) ikaja na njia mbadala ya kuwawezesha wananchi kusafirisha kwa usalama nishati hiyo.

“Tunaomba EWURA isaidie kuja na namna bora, vifaa vidogo vitakavyouzwa kwa bei rahisi ili wananchi waweze kusafirisha na kuhifadhi kwa urahisi kwa sababu yanawasaidia sana” amesema Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto Wilaya ya Bariadi, Maulo Kigahe.

Katika hatua nyingine wadau hao wamezungumzia suala la urasimu katika kuunganishwa kwa umeme kwa wananchi katika baadhi ya ofisi za Mameneja wa TANESCO  na kuomba EWURA ione namna ya kuwasaidia wananchi wasaidiwe kupata huduma kwa wakati.

“ Kuna wananchi wakitaka  kuunganishiwa umeme majumbani kwao wanadaiwa pesa mara shilingi laki tano, mara milioni moja hivi EWURA wanayajua matatizo haya? Tukizingatia kuwa umeme ni moja ya huduma muhimu kwa mwananchi tubadilike maana hata kule vijijini tulikozaliwa tunahitaji umeme” alisema Mkuu wa  Gereza Wilaya ya Bariadi, Kajungu Massami.

Naye Saibogi Mwandu mwananchi kutoka Bariadi amesema ni vema wafanyabiashara wadogo hususani wanaouza mafuta ya petroli kwenye chupa wakapewa elimu ya namna ya kutunza mafuta hayo kwani wengi wao wamekuwa wakitunza bidhaa hiyo ndani.

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Mawasiliano (EWURA) makao makuu Wilfred Mwakalosi amesema EWURA katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imeshabuni mwongozo utakaosaidia wawekezaji wa vijijini kuwekeza kwenye vituo vya gharama nafuu.

Akifunga mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe Festo Kiswaga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka wadau wote kuwa mabalozi wazuri wa EWURA ili wasaidie kufikisha elimu waliyoipata katika maeneo yao.

Awali akifungua mkutano huo, Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu umejipanga katika utekelezaji wa Sera ya Viwanda kwa kujenga viwanda ikiwemo kiwanda cha vifaa tiba, kiwanda cha chaki na vingine ambavyo vitahitaji huduma za nishati na maji , hivyo ameiomba EWURA kushirikiana na Taasisi zinazohusika na utoaji wa huduma hizo katika kuhakikisha zinatolewa katika viwango vinavyokidhi mahitaji ili Mkoa uweze kufikia malengo yake katika uzalishaji katika viwanda.
MWISHO.




Baadhi ya viongozi na wadau wakiwa katika Mkutano wa kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akifungua Mkutano wa kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka, uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) wa Kanda ya Ziwa Mhandisi. Loden Kitumbika akiwasilisha mada katika Mkutano wa kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo, uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.
Afisa Mawasiliano Mkuu kutoka  Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Bw. Wilfred Mwakalosi akiwasilisha mada katika Mkutano wa kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo, uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga(kulia) na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Ekwabi Mujungu wakifuatilia kwa makini mada zikiwasilishwa katika Mkutano wa kuelimisha wadau kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) Mkoani Simiyu, uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) wa Kanda ya Ziwa Mhandisi. Loden Kitumbika akitoa utangulizi wa lengo la Mkutano wa kuelimisha wadau kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo Mkoani Simiyu, uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.
Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu, wakiwa katika Mkutano wa kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.
Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau, wakiwa katika Mkutano wa kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!