Saturday, May 23, 2020

SIMIYU TUMEJIPANGA KIKAMILIFU KUWAPOKEA KIDATO CHA SITA KUANZA MASOMO JUNI MOSI: SAGINI


Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema mkoa huo umejipanga kikamilifu kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita kwa ajili ya kuanza masomo Juni Mosi, 2020 kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe  Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo 23 Mei,2020 Sagini amesema Simiyu iliandaa mkakati maalum kwa kushirikiana na wadau kuwawezesha wanafunzi kujisomea hivyo, mkoa utahakikisha muda uliotolewa na Wizara ya elimu kufanya maandalizi ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita (Juni Mosi-Juni 28) unatumika vizuri na walimu na wanafunzi kwa ajili ya rejea na kukamilisha mada.

“Sisi kama mkoa elimu ni kipaumbele cha kwanza  hivyo tumejipanga kikamilifu kuwapokea vijana wetu wa kidato cha sita, ikumbukwe pia kuwa kama mkoa tuliandaa mkakati wa kuwasaidia wanafunzi kujisomea hususani madarasa ya mitihani wakati walipokuwa likizo ya tahadhari ya Corona; tutahakikisha muda uliotolewa na wizara ya elimu kujiandaa na mtihani wa Taifa unatumika vizuri kufanya marejeo na kukamilisha mada zilizobaki,”alisema Sagini.

Aidha, Sagini amesema viongozi katika maeneo yote watahakikisha tahadhari zote zinazotolewa na Wizara yenye dhamana na Afya katika  kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona zinazingatiwa katika shule zote za kidato cha sita Mkoani Simiyu.

Vile vile Sagini ametoa wito kwa wazazi na walezi mkoani Simiyu kuendelea kuwahimiza na kuwasimamia watoto wao walioko majumbani kujisomea wakati huu ambao wengine bado wako likizo mpaka shule zitakapofunguliwa, huku akisisitiza kuwa mkakati wa mkoa wa kuwawezesha wanafunzi kujisomea wakati wakiwa likizo utaendelea kutekelezwa.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amesema pamoja na utekelezaji wa mkakati maalum wakati likizo, kabla ya serikali kutangaza kufunga shule wanafunzi wa kidato cha sita walikuwa katika kambi ya kitaaluma, ambapo takribani mada zote zilikuwa zimeshakamilika na wanafunzi walikuwa wakipewa majaribio na kurudia mada ambazo hazikueleweka vizuri.

Naye  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza amesema  idara ya elimu katika Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na waratibu elimu kata  wamejipanga kuhakikisha kuwa wanakamilisha mahitaji yote ya kujisomea kwa wanafunzi wa kidato cha sita yanaandaliwa na kukamilika kwa wakati ili kuwawezesha kujiandaa na mtihani wa Taifa.


Kwa upande wake mmoja wa wazazi wenye wanafunzi wa kidato cha Sita mjini Bariadi, Bw. Chambwite Sadala amesema anaunga mkono uamuzi wa Mhe. Rais wa wanafunzi wa kidato cha sita kurudi shuleni, hivyo akatoa wito kwa wanafunzi hao kwenda kufanya bidii katika kujisomea katika muda waliopewa ili waweze kufanya vizuri na hatimaye kufikia malengo yao.

Mkoa wa Simiyu una jumla ya shule 13 za sekondari za Kidato cha tano na Sita, ambapo kwa mwaka 2020 jumla ya wanafunzi 953 wa kidato cha Sita wanatarajiwa kufanya mtihani wa Taifa kuanzia tarehe 29 Juni 2020 kama ilivyotangazwa na Waziri wa elimu, sayansi na teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.
MWISHO
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Mei 23, 2020 kuhusu utayari wa mkoa katika kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita kwa ajili ya kuanza masomo Juni Mosi, 2020 kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.



Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju akitoa ufafanuzi wa jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)  Mei 23, 2020 kuhusu utayari wa mkoa katika kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita kuanza masomo Juni Mosi, 2020 kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!