Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wakazi wa Bariadi Mkoani humo wakati wa uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani. |
Waimbaji
wa Kwaya ya AICT Bariadi Mjini wakiimba wimbo maalum wenye ujumbe wa Usalama
Barabarani wakati wa uzinduzi wa
wiki ya nenda kwa usalama barabarani mjini Bariadi.
|
Wanafunzi wa Shule ya Msingi SOMANDA B wakionesha igizo wakati wa sherehe za maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani mjini Bariadi. |
Baadhi
ya wananchi wa Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo,
Mhe. Anthony Mtaka alipowahutubia wakati
uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mjini Bariadi.
|
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Simiyu, Edson Mwakiaba akiwasilisha taarifa ya Mkoa ya Usalama wakati uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mjini Bariadi. |
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. AnthonyMtaka akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
viongozi wa Mkoa huo na Waimbaji wa kwaya ya Kanila la AICT Bariadi.
|
Na Stella Kalinga
Katika
kukabiliana na ongezeko la ajali za barabarani, wamiliki wa bodaboda wametakiwa
kuhakikisha madereva wanaowakabidhi pikipiki wamepata mafunzo ya uendeshaji na
usalama barabarani
Wito
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka wakati wa uzinduzi
wa wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani uliyofanyika kimkoa mjini Bariadi mkoani humo.
Mtaka
amesema wamiliki wa bodaboda wanapaswa kutambua kuwa hiyo ni fursa kiuchumi
hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kuwa wanawakabidhi pikipiki watu wenye ujuzi
ambao watazilinda dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na ajali zisizo za
lazima.
“Wamiliki
wa bodaboda mnawekeza fedha nyingi katika kununua bodaboda lakini wengi wenu
mnawakabidhi madereva ambao hawana
mafunzo na wanakuwa sababu ya ajali za barabarani. Hakikisheni wamepewa mafunzo
na ambao hawana wasaideni wapate ili kuepuka kupoteza pikipiki zenu na nguvu
kazi ya Taifa kwa ajali ambazo siyo za lazima”alisema Mtaka.
Aidha,
Mtaka amewataka madereva wanaoendesha bodaboda kuheshimu kazi hiyo kwa kuwa
inawapatia kipato hivyo wanapaswa kujifunza na kuzingatia matakwa ya sheria za
usalama barabarani.
Akisoma
taarifa ya Hali ya Usalama Barabarani Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani
Mkoa wa Simiyu, ASP.Edson Mwakihaba amesema katika kipindi cha Mwezi Januari
hadi Desemba 2016 jumla ya ajali 111 zimetokea mkoani humo ambazo zimesababisha
watu 71 kupoteza maisha na wengine 39
kujeruhiwa.
ASP Mwakihaba amesema vyanzo vya ajali hizo ni
elimu duni kwa waendesha bodaboda ambao wanabeba abiria bila kupata mafunzo na
kutovaa kofia ngumu, matumizi yasiyo sahihi ya vyombo vya moto katika kubeba
mizigo ya hatari na kuzidisha uzito ulioruhusiwa, ubovu wa barabara na vyombo
vya usafiri,ukosefu wa maegesho na makosa ya kibinadamu.
Vyanzo vingine ni pamoja na kukosekana kwa alama za
barabarani,mapungufu ya sheria ya salama barabarani ambayo makosa mengi
hayaendani na viwango vya adhabu, kukosekana kwa vyuo vya kutolea elimu kwa
madereva na magari mengi ya minadani kuchanganya abiria na mizigo.
Mwakihaba
amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikana na wadau mbalimbali limejiwekea
mikakati mbalimbali katika kukabiliana na ajali za barabarani ikiwa ni pamoja
na kutoa elimu kwa watumia vyombo vya moto na wananchi kwa ujumla juu ya sheria
za usalama barabarani, kukagua madereva na vyombo vya moto kabla ya safari.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka imelitaka Jeshi la Polisi
Kikosi cha Barabarani kutowaruhusu madereva kuendesha magari ya abiria wanapogundulika kuwa na kilevi pale
wanapopimwa kabla ya kuendesha vyombo vyao.
Sambamba
na hilo Mkuu huyo wa Mkoa amelitaka jeshi la Polisi Kikosi cha usalama
Barabarani kuwapima madereva wa bodaboda na bajaji hususani wale walio katika
miji mikuu ya wilaya badala ya kujikita kwa madereva wa magari pekee.
Kauli
Mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Mwaka 2016 ni“Hatutaki
ajali,tunataka kuishi” na hii ni
mara ya nne tangu kwa maadhimisho haya kufanyika mkoani Simiyu tangu kuanzishwa
kwake.
0 comments:
Post a Comment