Na Stella Kalinga
Wanaume
ambao bado hawajafanyiwa tohara mkoani Simiyu wamehamasishwa kufanya hivyo ili kukabiliana na maambukizi
mapya ya Virusi vya Ukimwi Mkoani humo.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka katika ufunguzi wa
Mkutano wa wadau wa Mapambano dhidi ya Ukimwi na Uzinduzi wa Mpango mkakati wa
Mkoa huo uliofanyika jana katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yohana Mjini Bariadi.
Mtaka
amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika
nchini Afrika ya Kusini, Kenya na Uganda imethibitishwa pasipo shaka kuwa tohara kwa wanaume hukinga maambukizi ya
Virusi vya Ukimwi kwa asilimia 60, hivyo wanaume wajitokeze waweze kupata
huduma hiyo bure.
Akizungumza
kwa niaba ya Mratibu wa Mapambano dhidi Ukimwi Mkoa wa Simiyu, Mratibu wa
Mapambano dhidi ya Ukimwi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Daktari Wilfred
Magulu amesema ni asilimia 32 tu ya wanaume Mkoani Simiyu ambao wamefanyiwa
tohara.
Daktari
Magulu amesema Serikali imeweka mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi hususani wanaume
na kuwahamasisha ili wawe na mwamko na kuona umuhimu wa kufanyiwa tohara pasipo
gharama yoyote katika Hospitali zote na vituo vyote vya kutolea huduma za afya,
kwa lengo la kufikia asilimia 72 ya Kitaifa.
Sambamba
na hilo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema wataalam wa afya na
wadau wa Ukimwi kwa ujumla wanao wajibu wa kuwaelimisha wananchi juu ya kujikinga na maambukizi, umuhimu wa kupima
VVU na kuwajengea ujasiri wa kupokea matokeo ya vipimo vyao ili wanapogundulika
kuwa na maambukizi waanze matibabu mapema.
Mtaka
amesema wataalam hao wanatakiwa kuliepusha Taifa katika maambukizi mapya ya VVU
kwa kuwaeleza wananchi ukweli juu ya njia sahihi za kujikinga na maambukizi
mapya ikiwa ni pamoja na Matumizi sahihi ya kondomu.
“Waratibu
waelezeni watu umuhimu wa kujikinga na maambukizi, fanyeni utafiti kuona maduka
mangapi ya vijijini yanauza kondomu mkikuta hakuna wapimeni wananchi katika
hivyo vijiji muone hali ya maambukizi ikoje, Msisiishie kuyazungumza masuala
haya kwenye makongamano na warsha” , alisema Mtaka.
Ameongeza
kuwa Waratibu wa Mapambano dhidi ya Ukimwi katika Halmashauri zote za Mkoa huu wahakikishe
baa na nyumba zote za kulala wageni
zilizopo mijini na maeneo yote yenye watu wengi zinawekewa kondomu na elimu ya matumizi sahihi ya kondomu hizo
itolewe kwa wananchi.
Wakati
huo huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt.Mageda Kihulya amesema wananchi
wajijengee utaratibu wa kupima afya na wanapogundulika kuwa na maambukizi Virusi
vya Ukimwi watembelee vituo vya kutolea huduma za Afya ili waanze kupewa huduma
mapema.
Hali
ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi/UKIMWI ni asilimia 3.6 kama ilivyooneshwa
kwenye utafiti wa mwaka 2011-2012 ukilinganishwa na kiwango cha Kitaifa cha asilimia
5.1.
Mkutanowa
wadau wa mapambano dhidi ya Ukimwi Mkoani Simiyu umewashirikisha Wakuu wa
Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri, Wabunge, Viongozi
wa Madhehebu ya Dini, Waratibu wa Mapambano dhidi ya Ukimwi wa Wilaya zote na
Wakuu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na Mapambano dhidi ya
Ukimwi mkoani humo.
0 comments:
Post a Comment