Wednesday, June 14, 2017

BARAZA LA UWEZESHAJI LATOA TUZO KWA MKOA WA SIMIYU KWA KUTEKELEZA SERA YA VIWANDA

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limetambua mchango wa Mkoa wa Simiyu katika  Utekelezaji wa Sera ya Viwanda na kutoa Tuzo ya kikombe na Cheti.

Tuzo hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji lililofanyika Mjini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka amesema Tuzo hizi ni  hamasa kwa Viongozi na wananchi wa Simiyu kuongeza jitihada zaidi katika Utekelezaji wa Sera ya Viwanda kuelekea kwenye Uchumi wa Kati.

Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “WILAYA MOJA BIDHAA MOJA” ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha kutengeneza Chaki kilichopo wilayani Maswa na Kiwanda cha kusindika Maziwa wilayani Meatu, ambapo upembuzi yakinifu unaendelea kwa ajili ya upanuzi wa viwanda hivi ili kuongeza uzalishaji.

Aidha, upembuzi yakinifu utafanyika katika Halmashauri nyingine kwa ajili ya kuanzisha viwanda mbalimbali kikiwemo kiwanda cha sabuni za maji, za unga na mche wilayani Itilima, Kiwanda cha kutengeneza Tomato Sauce na Chill Sauce Wilaya ya Busega na kiwanda cha kusaga nafaka  na kupaki unga Bariadi Mjini.

Vingine ni kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kitakacojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Kiwanda cha kutengeneza vifungashio kitakachojengwa Wilayani Maswa.


Pamoja na viwanda hivyo, Serikali imekusudia kujenga Kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba,  ambacho kitasaidia Taifa kuokoa fedha zilizokuwa zikitumika kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kulia) na Katibu Tawala Mkoa,Ndg.Jumanne Sagini(kushoto) wakiwa na tuzo za Kikombe na cheti ambazo zimetolewa kwa Mkoa wa Simiyu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji kutambua utekelezaji wa Sera ya Viwanda kwa mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akikabidhiwa Tuzo ya Kikombe kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ambayo ilitolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji kutambua utekelezaji wa Sera ya Viwanda kwa mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(aliyeshika kikombe) katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama(wa tatu kulia) na baadhi ya Viongozi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!