Shirika la Kidini la
Madhebu ya Kikristo la Life Ministry limetoa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi
ya shilingi Milioni 40 kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Mjini Bariadi.
Akipokea vifaa tiba hivyo Mkuu
wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Life Ministry kwa msaada
huo na kuwahakikishia kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma za
afya kwa wananchi katika hospitali hiyo.
Aidha, amesema Serikali
iko tayari kushirikiana na madhehebu ya dini katika kuhakikisha kuwa afya za wananchi zinakuwa
salama, hivyo akawahakikishia kuwa milango
iko wazi kwa taasisi nyingine za dini zinazotaka kuunga mkono juhudi za Serikali
katika kuboresha huduma za afya.
Mtaka ameongeza kuwa
ili Madaktari na wauguzi waweze kutekeleza majukumu yao vizuri ni lazima
wawezeshwe vifaa, hivyo msaada huo utawatia moyo na kuongeza ari ya kufanya
kazi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Life Ministry hapa nchini, Dismas Shekalaghe amesema vifaa hivyo
vimetolewa kama sehemu ya kuisaidia jamii ambavyo vitawawezesha madaktari na
wauguzi kuwahudumia wananchi.
Shekalaghe ameongeza
kuwa wao wanaamini kuwa ili mtu aweze kumtumikia Mungu ni lazima awe na afya njema, hivyo kupitia
msaada huo wa vifaa wagonjwa watahudumiwa na kurudi katika hali zao kawaida na
kuendelea kumtumikia Mungu na kufanya shughuli za maendeleo.
Naye Mganga Mfawidhi wa
Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Dkt.Fredrick Mlekwa akitoa shukrani kwa Life
Ministry amesema, msaada huo umefika katika wakati muafaka ambapo amesisitiza
kuwa uongozi wa Hospitali umefarijika kupata vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia
kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Tumefarijika sana
kupata msaada huu na walengwa ambao ni wananchi watapata huduma bora kupitia vifaa hivi, naomba nitoe wito kwa Mashirika
mengine ya madhehebu ya dini kuendelea kutusaidia kwa kuwa Hospitali hii
inawahudumia watu wenye mahitaji mbalimbali” alisema Dkt.Mlekwa.
Baadhi ya Vifaa
vilivyotolewa na Life Minisry ni pamoja na viti vya kubebea wagonjwa(wheel
chairs), vifaa vya viungo bandia, vifaa vya huduma za meno, vifaa vya
vinavyotumika katika upasuaji, bandeji na mabomba ya sindano.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka(katikati), Mganga Mfawidhi wa Hospitali
Teule ya Mkoa, Dkt. Fredrick Mlekwa(kushoto) wakikabidhiwa viti vya kubebea
wagonjwa na Mkurugenzi wa Life Ministry Bw. Dismas Shekalaghe (kulia). ambavyo ni miongoni mwa vifaa vilivyotolewa Shirika hilo la Kikristo kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wachungaji wa madhehebu
ya Kikristo wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na Shirika la
Kikristo la Life Ministry kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, mjini Bariadi
Mganga Mfawidhi wa
Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Dkt.Fredrick Mlekwa akizungumza
wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na Shirika la Kikristo la
Life Ministry kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, mjini Bariadi.
Mkurugenzi
wa Life Ministry hapa nchini, Dismas Shekalaghe(wa pili kulia) wakati wa makabidhiano ya vifaa
tiba vilivyotolewa na Shirika hilo la Kikristo kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa
Simiyu, mjini Bariadi.
Baadhi ya Viti vya
kubebea wagonjwa(wheel chairs) vilivyotolewa na Shirika la Madhehebu ya Kikristo
la Life Ministry kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment