Wednesday, May 31, 2017

WACHUNGAJI ,WAGANGA WA JADI WACHEZA MPIRA KULENGA KUPINGA MAUAJI YA WENYE UALBINO

Mkoa wa Simiyu umeweka historia ya Mchezo wa Mpira wa Miguu baina ya wachungaji na waganga wa jadi ikiwa ni makubaliano ya kutoa ujumbe wa kupinga mauaji ya watu wenye Ualbino na vikongwe kwa kupiga maarufuku Ramli Chonganishi ambazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa mauaji hayo.

Mchezo huo kati ya wachungaji na waganga wa jadi umefanyika  siku moja kabla ya kufanyika burudani kubwa ya utamaduni wa asili almaarufu Mbina ambayo hufanyika kila mwaka Mei 31,baada ya wakulima kumaliza msimu wa kilimo .

Pande zote mbili kwa  pamoja zilikubaliana  kuwa utaratibu wa kufanya vikao na michezo utakuwa endelevu na utafanyika kila mwaka kwa kuzunguka katika wilaya zote ili kuhakikisha mauji ya watu wenye ualbino na vikongwe yanakomeshwa kabisa.

 Askofu wa K.K.K.T Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt.Emmanuel Makala amesema Kanisa liko tayari kukemea kwa wazi mauaji ya watu wenye ualbino na linaunga mkono juhudi za Serikali za kulinda amani na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Naye Mtemi Charles Balele Doto ambaye ni Katibu wa Umoja wa Watemi Kabila la Wasukuma amesema waganga wa jadi kazi yao ni kutoa huduma za tiba asili kwa watu na siyo kufanya ramli chonganishi zinazopelekea mauji ya watu wenye ualbino, akawataka wanaofanya hivyo waache mara moja kwa kuwa ni wababaishaji na wanadhallisha ya huduma ya tiba asili.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo kukamilika,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amewapongeza kwa uamuzi huo ambao unatoa Taswira mpya kwa mkoa wa Simiyu  wa kuondokana na dhana iliyokuwepo ya mauaji na kuwa mkoa wa kimaendeleo na kuagiza michezo mbalimbali kufanyika kila mwezi ili kuendeleza vipaji vya mbalimbali vya wanamichezo.

Aidha, amesema Mkoa huo una agenda ya “Wilaya Moja, Bidhaa Moja, Kiwanda Kimoja ama ununue au ukodishe Simiyu, Watanzania Tupende vya kwetu”hivyo akawataka wananchi kuchangamkia fursa hizo kwa maendeleo yao na kuachana na imani potofu kuwa Viungo vya Mtu mwenye ualbino vitawapa utajiri.

“Simiyu tunajenga viwanda utajiri wako wewe usiue albino utajiri wako lima pamba uuze kwenye kiwanda cha nguo, jiandae kuwa wakala, soma vizuri uwe mfanyakazi, jiandae kuzalisha malighafi ya Viwanda vya Rais wetu Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli”  alisema.

“Tarehe 09 Mwezi Juni tunapokea hundi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha chaki Maswa, Tarehe 12 Juni tunaanza upembuzi yakinifu wa viwanda vyetu viwili; upanuzi wa kiwanda cha maziwa Meatu na kiwanda cha kusindika nyanya na pilipili ili tutengeneze tomato sauce na chili sauce. Bariadi tutajenga kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba, Itilima tutajenga kiwanda cha kutengeneza sabuni zote hizi ni fursa” alisema

Mtaka ameongeza kuwa wazazi wote walio na watoto wenye ulemavu wa aina yoyote wasiwafiche wawatoe kwa Serikali imewatengenezea mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kulinda haki zao.

Wakati huo huo amewataka wananchi kuvitumia vituo vya kutolea huduma za Afya kwanza kila wanapohitaji matibabu badala ya kukimbilia kwa Waganga wa jadi hali inayopelekea wengi wao kuchelewa kupata  huduma wanapoteza maisha na kuingia katika ramli chonganishi kwa kuamini kuwa wamerogwa.

Katika Mtanange huo uliofanyika katika uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi  Waganga wa kienyeji walikubali kichapo cha Magoli mawili kwa nunge(sifuri) kutoka kwa watumishi wa Mungu(Wachungaji).
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kulia)akimkabidhi Askofu wa K.K.K.T Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt.Emmanuel Makala vitabu vya Neno la Mungu vilivyotolewa na Kanisa Waadventista Wasababto (SDA) Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kulia) akimkabidhi Askofu wa Kiongozi wa Waganga wa Kienyeji, Mayunga Kidoyayi vitabu vya Neno la Mungu vilivyotolewa na Kanisa Waadventista Wasababto (SDA) Bariadi.
Askofu wa K.K.K.T Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt.Emmanuel Makala akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka azungumze na wananchi, wachungaji na waganga wa jadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi, wachungaji na waganga wa jadi mara baada ya mchezo wa mpira wa miguu kati ya wachungaji na waganga wa jadi kumalizika.
Baadhi ya Wachungaji wakijiandaa kuingia uwanjani kwa ajili ya mtanange dhidi ya waganga wa jadi kwa lengo la kupinga mauaji ya watu wenye ualbino, vikongwe na ramli chonganishi.
Baadhi ya wananchi wakishangilia ushindi wa kichapo cha magoli mawili cha wachungaji dhidi ya waganga wa jadi.
Waimbaji wa Kwaya ya Umoja kutoka K.K.K.T Bariadi wakiimba wimbo maalum wa kupinga mauaji ya watu wenye Ualbino kabla ya Mchezo wa mpira wa miguu kati ya wachungaji na waganga wa jadi kuanza.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka alipozungumza na wananchi, wachungaji na waganga wa jadi mara baada ya mchezo wa mpira wa miguu kati ya wachungaji na waganga wa jadi kumalizika.
Wachezaji wa timu ya wachungaji(kulia) na waganga wa jadi (kushoto) wakiwa wamejipanga kabla ya kuanza mchezo ambao ulilenga kupinga mauaji ya watu wenye ualbino.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!