Wanufaika wa Mradi
wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini TASAF III hususani wanaopewa ruzuku ya
utimizaji wa masharti ya elimu na afya wamehimizwa kuwapeleka watoto kliniki na
kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shuleni.
Wito huo umetolewa
na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kutoka TASAF Makao Makuu, Ndg. Christopher
Sanga katika kijiji cha Migato wilayani Itilima wakati wa ziara ya tathmini ya
utekelezaji mradi wa TASAF wilayani humo.
Sanga
amesema Serikali ina mpango mzuri kwa wananchi wa kuhakikisha watoto wote wenye
umri wa kwenda shule wanapelekwa shule na pia watoto wote wenye umri chini ya
miaka mitano wanapelekwa kiliniki na kupata huduma za afya zinazotakiwa, hivyo akawaasa
kutorudisha nyuma juhudi za Serikali.
Aidha,
amesema lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha nguvu kazi inajengwa kwa kutoa
elimu na kuangalia afya za watoto wakiwa bado wadogo ili watakapobainika kuwa na
matatizo ya kiafya wapatiwe matibabu mapema kwa lengo la kuimarisha afya na kutoathiri ukuaji wao.
Ameongeza
kuwa utafiti uliofanyika kuhusu utekelezaji wa awamu zilizotangulia za Mpango
wa TASAF ulionesha kuwa, kumekuwa na miundombinu mingi ya elimu na afya lakini
kaya maskini zimekuwa hazipeleki watoto katika huduma hizo, hivyo Serikali
ikatoa ruzuku ya elimu na afya na kuwawekea masharti wazazi ili kuhakikisha
wanawapeleka watoto katika huduma hizo.
Amesisitiza
kuwa Mpango wa TASAF unafuatilia mahudhurio ya watoto wanaopata ruzuku ya utimizaji
wa masharti ya elimu na ili ruzuku hiyo iendelee kutolewa kwa wanafunzi hao ni
lazima mahudhurio yao yasiwe chini ya asilimia 80 kwa muhula, wasipohudhuria
kuna adhabu inayotolewa ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa ruzuku hiyo.
“
Miongoni mwa madhara ya watoto kutohudhuria masomo katika muhula husika kwa
kaya zinazonufaika na TASAF kwa kupata ruzuku ya elimu ambayo inasaidia kaya
hizo, ni kupungua kwa ruzuku na inapopungua uwezo wa kaya katika kujikimu na
kufanya mabadiliko ya kiuchumi
unaathirika” amesema Sanga.
Kwa
upande wake Bibi. Ngolo Buzenganwa mkazi wa kijiji cha Migato ambaye ni
mnufaika wa Mpango wa TASAF III amewataka wazazi wenzake kufuatilia maendeleo
ya watoto wao na kukagua daftari zao mara kwa mara ili ruzuku inayotolewa
isipunguzwe na iwasaidie kuwawezesha kupata mahitaji muhimu ya shule kwa ajili
ya watoto wao.
Katika
hatua nyingine wanufaika wa Mpango wa TASAF III wameshukuru mpango huo kwa
kutatua changamoto ya upungufu wa maji kwa kuwachimbia visima vya maji kupitia
programu ya kazi za ajira za muda na kuomba kuongezewa idadi ya visima hivyo
katika awamu nyingine ya utekelezaji wa mradi.
“Tunaishukuru
sana TASAF kutuletea maji kwa visima hivi, tulikuwa tunatembea muda mrefu sana
zaidi ya saa moja kufuata maji, lakini sasa hivi maji yapo karibu tena ni maji
safi na salama” amesema Maila Limbu mkazi
wa Migato.
Naye
Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima,Goodluck Masige amesema
Serikali Wilayani humo imeweka mpango wa kuviwekea pampu visima vyote 194
vilivyochimbwa kupitia mradi wa TASAF ili kuwarahisishia wananchi kupata maji
kwa urahisi zaidi kuliko teknojia inayotuika sasa ya kuvuta kwa kamba.
Wilaya
Itilima ni moja ya Wilaya tano zinazofanyiwa tathmini ya utekelezaji wa Mpango
wa Kunusuru kaya Maskini (TASAF III) katika awamu hii, tathmini inayofanywa na
wataalam kutoka TASAF Makao Makuu, Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo
(wadau washiriki wa mradi) ambao ni UNDP, UNFPA, ILO pamoja na Umoja wa Nchi za
Ulaya(EU).
0 comments:
Post a Comment