Mkoa wa Simiyu
unatarajia kufanya majaribio ya kufundisha wanafunzi kwa kutumia mtandao
kupitia programu itakayotengenezwa na watalaam wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA).
Hayo yamesemwa na Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka katika Maadhimisho ya Wiki ya Elimu Mkoani
humo yaliyofanyika kimkoa mjini Mwanhuzi Wilayani Meatu, chini ya Kauli Mbiu “TUWEKEZE
KATIKA ELIMU KWA USTAWI WA JAMII YENYE UTAALAMU WA SAYANSI NA VIWANDA KUELEKEA
UCHUMI WA KATI TANZANIA”
“Tunataka tufanye
majaribio, tuanze kwa kuunganisha shule
zetu za mjini wataalamu wetu wa ICT (TEHAMA) watengeneze programu,baadhi ya
madarasa kama darasa la saba tuanze
kufundisha kwa kutumia mtandao” amesema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya
wanafunzi walioshiriki katika maadhimisho ya wiki ya elimu wamesema iwapo teknolojia
hiyo itafanikiwa kutumika itawasaidia katika masomo yenye upungufu wa walimu
hususani wa sayansi, ambapo wameiomba Serikali kuendelea kutatua changamoto ya
upungufu wa vyumba vya madarasa na vifaa vya maabara ili kuwawezesha kujifunza vema
masomo hayo kwa nadharia na vitendo.
Kwa upande wake Afisa
Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Julius Nestory amesema maadhimisho ya wiki ya Elimu
yaliyoanza Mei 24 ni moja ya tathmini ya malengo yaliyowekwa Mei 2016 na
miongoni mwa mafanikio ya malengo hayo ni ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi
ya 180 chakula cha mchana kutolewa katika shule za kutwa lililotekelewa kwa
asilimia 43.
Katika hatua nyingine
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka amesema Serikali imepanga kupitia
Watalaam hao wa TEHAMA pia kwa kutumia teknolojia nyepesi, itengenezwe programu
itakayosaidia kutoa taarifa za uwepo wa watumishi mahala pa kazi.
Aidha ameongeza kuwa
katika kipindi hiki ambacho Serikali Mkoani Simiyu imejipanga kufanya mapinduzi
ya Viwanda, imedhamiria kuwatumia Watalaam wa TEHAMA kutengeneza mfumo wa
taarifa na takwimu sahihi za kila sekta zikiwemo za kilimo, mifugo, elimu ili
mtu akitaka taarifa yoyote ya Simiyu azipate kwa urahisi (awe nazo mkononi).
“Miaka minne ijayo
hatutakuwa na Simiyu mnayoiona leo, kama kuna mtu anafikiri ni maneno atupe
muda; tunataka tuwapunguzie Watanzania kufanya rejea nchi nyingine waje kwenye
mkoa wetu. Tarehe 09/05/2017 Maswa wanapokea hundi ya shilingi Bilioni 1.5 kwa
ajili ya ujenzi wa kiwanda cha chaki Maswa, Meatu upembuzi yakinifu unaanza
tarehe 12/06/2017 ujenzi wa kiwanda cha maziwa” amesema.
Wakati huo huo Mkuu
huyo wa Mkoa amesema Serikali inalitafutia ufumbuzi wa kudumu suala la bei ya pamba
ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wakulima kwa kuwa wafanyabiashara wananunua
pamba kwa bei ya chini kwa kigezo cha kuwa bei katika soko la dunia iko chini.
Mtaka amesema Simiyu
inaoongoza kwa kulima pamba lakini Halmashauri na wananchi hawanufaiki kwa
kiwango kinacholingana na uzalishaji uliopo, hivyo watatafutwa watalaam ambao
watachunguza bei ya pamba katika soko la dunia na akasisitiza kuwa
mfanyabiashara yeyote atakayeona pamba haina faida kwake aache katika Msimu wa
mwaka 2018 Halmashauri zitanunua.
Wiki ya Elimu
huadhimishwa kila mwaka mwezi Mei ikiwa na lengo la kuwakutanisha wadau wa
elimu, kuona shughuli mbalimali za elimu, kufanya tathmini ya mipango ya elimu
ya mwaka uliopita na kuweka mipango ya mwaka mwingine.
Katibu Tawala Mkoa Simiyu
Jumanne Sagini akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Meatu waliokuwa
wakionesha kwa vitendo matumizi ya vifaa vya maabara, wakati wa maadhimisho ya
wiki ya elimu kimkoa wilayani Meatu.
0 comments:
Post a Comment