Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka Viongozi Mkoani humo wasitoe
kauli za kukatisha tamaa watumishi walio chini yao ili waweze kutekeleza
majukumu yao vema ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika Agenda ya Mkoa ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda
chini ya Kauli Mbiu"WILAYA MOJA BIDHAA MOJA”.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi katika
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) duniani yaliyofanyika kimkoa Lamadi Wilayani
Busega.
Mtaka amesema Serikali Mkoani humo ina agenda katika Ujenzi wa Uchumi wa
Viwanda ambayo ni kujenga Viwanda ambavyo malighafi yake yanapatikana hapa
nchini.
Amesema Serikali Mkoani imedhamiria
kujenga Mkoa utakaoonesha dira katika
Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda, utaotekeleza Ilani ya CCM, Dira ya Taifa,Mpango wa
Taifa wa Miaka mitano, utakaotekeleza maono na matamanio ya Mhe Rais na ili kutekeleza yote haya Viongozi wanahitaji kuungwa mkono na watumishi wa Serikali.
“Sisi kama Mkoa tunahitaji kujenga Mkoa wetu kuwa mkoa wa Viwanda kwa vitendo siyo kwa maneno,
ili tuweze kujenga uchumi wa Viwanda ni lazima tuungwe mkono na wafanyakazi,
ili tuungwe mkono na wafanyakazi ni lazima kauli zetu ziweze kujenga morali kwa
wafanyakazi; hauwezi ukawa unataka kujenga uchumi wa viwanda Simiyu halafu
unakuwa ni Mkurugenzi au Mkuu wa Idara mwenye lugha za hovyo kwa wafanyakazi ni
vitu visivyowezekana” alisema
Ameongeza kuwa chini ya Kauli Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja” Serikali
imepanga kuwa Wilaya ya Busega iwe na kiwanda cha kutengeneza Tomato sauce,Chilli Sauce na
bidhaa zote za mbogamboga ambazo
zitauzwa katika mikoa ya Mwanza,Mara,Geita,Shinyanga,Kagera,Singida,Kigoma na
Dar es Salaam.
Aidha amesema katika wilaya ya Itilima zitatengenezwa sabuni za maji,unga
na za miche, wilaya ya Maswa Halmashauri itapata mkopo wa shilingi Bilioni 1.5
kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki na wilaya ya Meatu itapata shilingi
bilioni 1.3 kwa ajili ya kupanua kiwanda cha maziwa ili maziwa ya unga
yazalishwe pia.
Wakati huo huo Mtaka amesema Upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa
Kiwanda cha Vifaa Tiba vitokanavyo na zao la Pamba umeanza kufanyika ambapo
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF), Benki ya TIB, Bohari ya Dawa ya
Taifa(MSD),Shirika la Viwanda nchini (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
wamekuwa msaada mkubwa kuhakikisha ujenzi huu unafanyika.
Aidha, ameeleza kuwa mpaka sasa
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, Benki ya Azania na Taasisi ya SELF
iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango wameonesha utayari wa kuunga mkono Mkoa
wa Simiyu katika utekelezaji wa Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa Moja.
Ameongeza kuwa vitajengwa viwanda katika Halmashauri zote ili wananchi wote
wanufaike na uwepo wa viwanda hivyo kwa ajira na maendeleo ya uchumi hivyo
akawataka watumishi wa Umma wachangamkie fursa hizo wakati Serikali ikitekeleza
miradi yote hiyo kujenga Uchumi wa Viwanda.
“ Simiyu tunatekeleza na tunataka mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu, kila
wilaya atakayopita Mhe,Dkt.John Magufuli katika Mkoa wetu akute kura
tulizoziandaa , hamasa ya wananchina imani thabiti,vijana na wakina mama ambao
mazao yao yatakuwa yameongezewa thamani na viwanda vilivyo ndani ya wilaya zao”
alisema.
Mtaka pia amewataka waajiri wote Mkoani humo kuacha tabia ya kuwakopa
watumishi hodari zawadi zao wakati wa
Siku ya Wafanyakazi, na badala yake wahakikishe wanawapa kile wanachostahili na
akawataka watumishi wote kutekeleza
majukumu yao kwa weledi ambapo amesema ambao watafedhehesha taaluma zao
watachukuliwa hatua.
Kwa upande wake Mratibu wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi)
Ndg. Catherine Nyingi akisoma risala kwa niaba ya watumishi wote amempongeza
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka kwa kukomesha vitendo vya
udharilishaji kwa Waumishi wa Umma vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya wananchi
dhidi ya watumishi wa Umma vikiwemo uchapaji wa viboko hadharani, kuhukumiwa na
mahakama za kimila (dagashida) na kupewa adhabu mbalimbali ikiwepo ya kutozwa
fedha.
Nyingi pia amesema Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi linaomba Serikali
iongeze kima cha chini cha mshahara, ishughulikie upandishaji wa madaraja,
kulipa madeni ya watumishi na waajiri wapeleke michango ya watumishi wao katika
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi mwaka 2017 ambayo ni
yameadhimishwa kwa mara ya tano saa mkoani Simiyu ni “UCHUMI WA VIWANDA UZINGATIE,
HAKI, MASLAHI NA HESHIMA YA WAFANYAKAZI”
0 comments:
Post a Comment