Bodi ya Wadhamini
ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF imeridhia kutoa mkopo wa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya upanuzi
wa kiwanda cha chaki kilichopo wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu.
Kauli hiyo
imetolewa na Kaimu Meneja wa Mipango na Uwekezaji wa NSSF Bibi. Radhia Tambwe katika mahojiano maalum
na waandishi wa Habari mara baada ya kikao cha wadau wa uwekezaji Mkoani Simiyu
kilichofanyika Kata ya Lamadi wilayani Busega ambacho kimewahusisha wadau
mbalimbali wa uwekezaji mkoani humo.
Bibi.Radhia
amesema Bodi imefanya uamuzi huo baada ya kupitia maombi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Maswa na kuona kuwa mradi wa kiwanda cha chaki una tija kwa kuwa
umewashirikisha vijana hivyo kiwanda kitakapopanuliwa kitaongeza wigo wa ajira
kwa vijana, pato la wilaya na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza chaki
nje ya nchi.
Aidha,
amepongeza utekelezaji wa Kauli Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja” mkoani
Simiyu katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda ambapo amesema kupitia viwanda
vitakavyoanzishwa katika kila wilaya chini ya Kauli Mbiu hii mkoa utatengeneza
ajira kwa wananchi wa ndani na nje ya mkoa.
Bi.
Radhia pia ametoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono miradi ya ujenzi wa
Uchumi wa Viwanda Mkoani Simiyu kwa kuwa ni miradi yenye tija kwa kuzingatia
kuwa malighafi zinazotumika zinapatikana
hapa nchini na soko lake kubwa liko hapa nchini.
“Watanzania
tubadilike tusikubali kila mara kugeuzwa supermarket, tuzalishe bidhaa zetu na
kutumia bidhaa zetu wenyewe tujivunie tulivyonavyo ili tuweze kuendeleza nchi
yetu na hatimaye Tanzania na sisi tuwe nchi yenye uchumi wa kati” alisema.
Naye
Mkurugenzi wa Benki ya Azania Ndg.Charles
Jackson Itembe amesema benki hiyo iko tayari na inaunga mkono uwekezaji katika
sekta ya viwanda unaofanywa na Halmashauri za Mkoa wa Simiyu chini ya Kauli
mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja” kwa kutoa uwezeshaji kifedha katika
miradi iliyoaanishwa na Halmashauri husika kupitia mikopo.
Kwa
upande wake Mtaalam Mbobezi wa Viwanda, Ndg. Ndaki Munyeti amesema Mkoa wa
Simiyu umejipanga katika kuwashirikisha Wataalam mbalimbali katika kuchagua
teknolojia itakayotumika katika viwanda vilivyopo na vitakavyoanzishwa ambayo
ndiyo hatua muhimu katika ujenzi wa viwanda inayoweza kusaidia kupata bidhaa
bora na kufanya viwanda vikawa endelevu.
Awali
akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha wadau wa uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu
Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka amesema pamoja na NSSF na Benki ya Azania
kukubali kuunga mkono juhudi za Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Mkoani Simiyu amesema
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wameahidi kutoa fedha za
upembuzi yakinifu kwa mradi utakaotekelezwa katika kila wilaya(Wilaya Moja
Bidhaa Moja).
Mtaka
amewataka viongozi kila mmoja awajibike ipasavyo katika eneo lake kwa kuwa wale
walioteuliwa waliaminiwa na Mhe.Rais na waliochaguliwa waliaminiwa na wananchi
hivyo watimize wajibu wao kuhakikisha viwanda vinasimama na kero za wananchi
zinatatuliwa.
“Viongozi
wenzangu wa kuteuliwa tunapaswa kuwajibika, Mhe.Rais aliacha watu wengi
akatuamini akatuteua sisi, Waheshimiwa madiwani wananchi waliwaamini
kuwachagua, ni lazima tuioneshe dunia kuwa inawezekana; natamani mwaka 2020
tutengeneze kura siyo mikutano ya hadhara, kila atakapo pita Mhe.Rais kuwe na
kitu ambacho wananchi wanajivunia kupitia kazi zetu sisi” alisema.
Kikao
cha wadau wa uwekezaji kiliwahusha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa,
Watalaam wa Sekretarieti ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya,Wenyeviti na Makamu wenyeviti
wa Halmashauri,Wakurugenzi wa Halmashauri,Wajumbe wa Kamati za Fedha za
Halmashauri, Maafisa Mipango, Wachumi, Wataalam kutoka Benki ya Azania, NSSF na
Watalaam wa Viwanda na Masoko.
Katika
kikao hicho maandiko ya miradi ya uanzishwaji viwanda kutoka katika Halmashauri
zote sita za Mkoa wa Simiyu yaliwasilishwa kwa wadau hao ambayo ni upanuzi wa
kiwanda cha chaki na kiwanda cha kutengeneza vifungashio vya karatasi (Maswa),
upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa Meatu, kiwanda cha kutengeneza sabuni za maji,
mche na unga Itilima, kiwanda cha kutengeneza tomato sauce na chili sauce (Busega)
kiwanda cha kusaga nafaka na kufungasha
unga pamoja na unga lishe (Bariadi Mjini) na kiwanda cha kutengeneza bidhaa za
Ngozi (Halmashauri ya Wilaya Bariadi) lengo likiwa ni wadau wa Taasisi za fedha
na watalaam kwa pamoja kupitia maandiko hayo kujiandaa na utekelezaji.
Upanuzi
wa Kiwanda cha Chaki ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli alilolitoa kwa Uongozi wa Wilaya ya Maswa baada ya
kutembelea kiwanda hicho wakati wa ziara yake mwezi Januari wilayani Maswa
Mkoani Simiyu, ambapo aliagiza uongozi huo kukopa fedha kwa ajili kupanua
kiwanda hicho ili kuongeza uzalishaji.
0 comments:
Post a Comment