Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian
Manoza amesema Matumizi ya Mbegu bora na Kilimo cha Mkataba
ni suluhu ya wakulima wa pamba inayoweza kuwasaidia kuongeza
uzalishaji.
Manoza ameyasema hayo wakati akitoa
taarifa ya Wilaya ya Meatu kuhusu kilimo cha Pamba kwa Wakuu wa Mikoa nane
ya Kanda ya Magharibi inayolima pamba waliotembelea eneo hilo kutoka Simiyu,
Shinyanga, Geita, Mwanza, Kagera, Kigoma, Singida na Tabora katika ziara yao
kuona mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora ya pamba(UKM08) katika kata ya
Mwabusalu wilayani Meatu.
Amesema kupitia kilimo cha mkataba
wananchi watakuwa na uhakika wa kupata pembejeo bora za kilimo zikiwemo mbegu
bora, mbolea na viuadudu kutoka kwa watu au makampuni yatakayoweka
mikataba nao.
“Tunatarajia kuongeza uzalishaji ili
kupata kata nyingi zaidi, tumewasisitiza wananchi kuwa kilimo hiki cha mbegu
bora lazima kiendane na kilimo cha mikataba, wale wanaohitaji kununua pamba
lazima waingie mikataba na wakulima ili wapate faida walizokuwa hawazipati;
baadhi yao wamekuwa wakihangaika hawana uwezo wa kununua mbegu, viuadudu na
kuhudumia mashamba, lakini wakiingia mikataba hao watakaonunua pamba watatoa
huduma zote hizo kwa wakulima” alisema.
Ameongeza kuwa pamoja na kilimo cha
mkataba na matumizi ya mbegu bora ili kuboresha uzalishaji wa pamba
Wataalam wa Kilimo wanapaswa kuwapa wakulima huduma zote muhimu za
ugani ili wazingatie taratibu zote za kuandaa mashamba, upandaji
na utunzaji wa pamba.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Meja
Jenerali Ezekiel Kyunga ameitaka Bodi ya Pamba nchini kuboresha utaratibu wa
kilimo cha mkataba ili kiweze kuwanufaisha wakulima badala ya kuwakatisha tamaa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Mhe.Aggrey Mwanri amesema ni vema Bodi ya Pamba ikaweka utaratibu
utakaowawezesha wakulima kupata mbolea na zana bora za kilimo kwa
mkopo ambao watarejesha baada ya mavuno.
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba,
Marco Mtunga amesema wakulima wa pamba kwa miaka ya nyuma wamekuwa
wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mbegu bora na
kutopanda kwa kuzingatia mistari, hivyo katika msimu wa mwaka 2017 jumla ya
tani 8000 za mbegu bora zitazalishwa kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima na
jitihada zinaendelea kufanywa kupitia kilimo cha mkataba kuhamasisisha wakulima
kulima kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.
Aidha, Mtunga amesema ili kuongeza
uzalishaji wa pamba wakulima wahamasishwe kulima kilimo cha mkataba na
ili kilimo cha mkataba kiwe na tija kwao Bodi hiyo
inaendelea kutimiza wajibu wake kusimamia masharti yaliyowekwa
katika utekelezaji wa mikataba hiyo kati ya wachambuzi na wakulima wa
pamba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida,
Mhe.Dkt.Rehema Nchimbi amesisitiza kuwepo kwa mikakati ya kilimo cha
umwagiliaji katika zao la pamba ikiwepo uchimbaji wa mabwawa makubwa
yatakayowasaidia wakulima wakati wote badala ya kutegemea mvua tu.
Naye Bw.Charles
Thobias Mkulima wa kata ya Mwabusalu ambaye ametumia mbegu bora ya pamba
ya (UKM08) amesema mbegu hiyo imekuwa mkombozi kwa wakulima kwa kuwa
kulingana na mazao yalivyo sasa shambani, mavuno yataonge zeka
kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na msimu uliopita.
Utekelezaji wa Mpango wa uzalishaji wa Mbegu
bora katika kata ya Mwabusalu Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu
umehusisha jumla ya wakulima 1,709 katika vijiji vinne ambao kwa pamoja
wameweza kulima jumla ya ekari 6,506 na unafadhiliwa na Programu ya Kuendeleza
Kilimo cha Pamba chini ya usimamizi wa Bodi ya Pamba.
0 comments:
Post a Comment