Saturday, June 24, 2017

TAARIFA YA RUFAA YA VYETI FEKI KUTOLEWA JUNI 30

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro   amesema taarifa ya rufaa ya watumishi waliobainika kuwa na vyeti feki itatolewa Juni 30, mwaka huu.

Dkt Ndumbaro ameyasema hayo leo wakati alipozungumza na viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya, ambao ni wasimamizi wa Watumishi wa Umma Mkoani Simiyu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi nchini.

Amesema katika zoezi la uhakiki la awamu ya kwanza Watumishi zaidi ya 9000 walibainika kuwa na vyeti feki ambapo kati yao ni asilimia kumi tu (10%) ndiyo waliokata rufaa.

“ Taarifa itawasilishwa tarehe 30 mwezi huu na baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya rufaa hizo  maelekezo yatatolewa namna ya kuhitimisha ajira za watu wenye vyeti feki” amesema

Aidha , amesema baada ya taarifa ya rufaa kuwasilishwa Serikali itatangaza vibali vya nafasi za ajira kwa watumishi watakaojaza nafasi zitakazoachwa wazi na zile zilizotengwa.

Wakati huo huo Katibu Mkuu huyo amewataka viongozi wasisite kuwachukulia hatua watumishi wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma na kuwapongeza wanaofanya kazi kwa bidii ili kuwapa motisha.

“Kusiwe na masuala ya kuhamisha watumishi wanaosumbua, kama mtu anasumbua malizana naye pale pale fuata taratibu mfungulie mashtaka,  ili tujenge utumishi wa Umma wenye uadilifu na weledi, lakini pia wale wanaofanya kazi vizuri wapongezeni mkiwaacha mtawakatisha tamaa” alisema.

Kuhusu suala la Watumishi kupandishwa vyeo Dkt.Ndumbaro amesema lifanyike kama motisha kwa watumishi wanaofanya kazi vizuri kwa kuzingatia ufanisi katika utendaji wa kazi,bajeti, masharti mengine ya upandaji vyeo kwa watumishi likiwepo la kufanya kazi kazi kwa muda usiopungua miaka mitatu katika cheo kimoja.

Katika hatua nyingine Dkt. Ndumbaro amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuwasimamia Maafisa Utumishi wanaosimamia mfumo wa mshahara wa LAWSON kuhakikisha wanaunganisha taarifa za mfumo huo na takwimu za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA kwa ufasaha na kuwakumbusha watumishi kuangalia taarifa zao ili wazihakiki ikiwa ziko sahihi na halali.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Watumishi wa Umma mkoani Simiyu, Katibu Tawala Mkoa ameahidi kutekeleza na  kuhakikisha watendaji wengine wanatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu ili Utumishi wa Umma ufanyike katika maadili, ufanisi na weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg.Mariano Mwanyigu ameshauri Serikali iangalie kwa upya umri wa kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, kwa mujibu wa sheria miaka 60 na kuona uwezekano wa kupunguza miaka ili kutoa nafasi kwa vijana wengi walio nje ya mfumo kupata ajira.

Kikao hicho ambacho pia kimetumika kutoa taarifa, maagizo na maelekezo mbalimbali kimewashirikisha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri na Maafisa Utumishi wanaoshughulikia Mfumo wa mshahara wa  LAWSON.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro  akizungumza na baadhi ya Watumishi wa Mkoa wa Simiyu mjini Bariadi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumisi nchini.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro  aweze kuzungumza na baadhi ya watumishi wa Umma(viongozi) mkoani humo.
Baadhi ya viongozi na watumishi wa Umma ngazi ya Wilaya na Mkoa wakisikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa umma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg.Mariano Mwanyigu akitoa maoni wakati wa kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Watumishi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa umma.
Mkuu wa Idara ya Utawala ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Diocle Rutema akitoa maoni wakati wa kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Watumishi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani Halmashauri ya Wilaya ya Itilima akitoa maoni yake wakati wa kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Watumishi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi na Makatibu Tawala Wilaya mara baada ya kufanya kikao na watumishi mjini Bariadi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Meatu na Itilima mara baada ya kufanya kikao na watumishi mjini Bariadi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Busega na Mji wa Bariadi mara baada ya kufanya kikao na watumishi mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!