Sunday, October 8, 2017

RC MTAKA: SIMIYU SASA TUNAJADILI MAENDELEO YA WANANCHI SIYO MAUAJI YA VIKONGWE NA ALBINO

Mkoa wa Simiyu kwa sasa haujadili tena masuala ya mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi(albino) badala yake unajidili maendeleo ya wananchi wa mkoa huo.

Hayo yamesemwa  jana na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ufungaji wa Makambi ya Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA) yaliyoyofanyika katika Uwanja wa Kidinda mjini Bariadi.

“Miaka hii miwili tumejenga mkoa ambao hatujadili mauaji ya albino, mauaji ya vikongwe, watu kukatwa mapanga, tunajadili Wasukuma Wanyantuzu wanaoenda kwenye maendeleo, ndiyo maana leo mtaona kumejengwa magorofa na nyumba nyingine bora, siyo watu wanaoamini kuwa mtu akiua watu anakuwa tajiri” amesisitiza Mtaka.

Ameongeza kuwa waumini hao wanapaswa kuwa mabalozi katika kufanya mambo ya maendeleo  na wakati huo huo wapinge na kukemea mambo maovu katika jamii na kuwa mfano wa kuigwa kwa watu wengine.

Aidha, ametoa wito kwa waumini hao kuchangamkia fursa za miradi mbalimbali itakayotekelezwa mkoani humo ukiwemo mradi wa kilimo katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mwasubuya Wilayani Bariadi, ambapo panakusudiwa kulimwa mpunga kupitia kilimo cha kisasa chenye tija.

Wakati huo huo amewataka waumini hao kuyafanyia kazi na kuyatafsiri kwa vitendo mafundisho waliyopewa wakati wa makambi yakiwemo ya ujasiriamali, ili mwaka 2018 watu watakaoshiriki katika makambi kama hayo waone matokeo ya bidhaa zilizotengenezwa kutokana na ujuzi walioupata mwaka huu.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato na wananchi wote kwa ujumla kuwaombe viongozi wa Serikali hususani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli, kwa kuwa anafanya kazi kubwa katika kudhibiti wizi na kutetea rasilimali za nchi hii ili ziwanufaishe Watanzania wote.

“Wapo watu wanauliza ni kwa nini Mhe.Rais aombewe, nawaomba tumuombee Mhe.Rais kwa sababu anafanya kazi kubwa kutetea rasilimali za Watanzania, anafanya maamuzi mazito ambayo yanawaumiza baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijinufaisha wao na kuwaumiza wenzao; yanagusa biashara za watu ambao wakati mwingine wangetamani Serikali hii ife hata kesho, ni lazima tumuombee Mhe.Rais” amesema Mtaka.  

Akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka,  Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato wa Southern Nyanza Conference inayojumuisha Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga na Geita, Mch.Sadock Butoke  amesema, Makambi hayo yamekuwa ya mafanikio kwani pamoja na waumini hao kufundishwa Neno la Mungu, wamefundishwa masomo  ya Afya, Ujasiriamali na kaya na familia ambayo yatawaimarisha kimwili na kiroho.

Naye Mbunge wa Viti Maalum(CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe.Leah Komanya amewashukuru viongozi wa dini kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuisaidia Serikali kwa kuwaelekeza waumini wao kufanya mambo mema na kuwa na hofu ya Mungu, hali inayopelekea wananchi wengi kutojihusisha na vitendo viovu.

Makambi ya Waumini wa Kanisa la Waadventisha Wasabato yaliyofungwa rasmi jana Jumamosi na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka yamedumu kwa takribani wiki tatu na yalifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato(hawapo pichani) jana wakati wa kufunga Makambi yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato wa Southern Nyanza Conference inayojumuisha Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga na Geita, Mch.Sadock Butoke akizungumza na waumini wa Kanisa hilo (hawapo pichani) jana, wakati wa kufunga Makambi yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akiimba (mwenye koti)pamoja na waimbaji wa Kwaya ya Kanisa la Waadventisa Wasabato Kurasini(Kurasini Choir) ya Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga Makambi ya waumini wa Kanisa hilo yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mbunge wa Viti Maalum(CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe.Leah Komanya akizungumza na Waumuni wa Kanisa la Waadventista Wasabato (hawapo pichani) jana wakati wa kufunga Makambi ya waumini hao yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akifurahia jambo wakati wa kufunga Makambi ya Waumuni wa Kanisa la Waadventista Wasabato(hawapo pichani) jana,  yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi; anayefuata, Mwenyekiti wa UWT(CCM) Mkoa wa Simiyu, Katibu Tawala Wilaya ya Bariadi, Albert Rutaihwa na Mbunge wa Viti Maalum(CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe.Leah Komanya.
Baadhi ya Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) alipozungumza nao jana wakati wa kufunga makambi yao yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(mwenye koti na tai) akiwa katika picha ya pamoja na waimbaji wa Kwaya ya Kurasini SDA mara baada ya kufunga makambi ya Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato jana,  yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(mwenye  tai ya bluu bahari) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Mkoa huo, waimbaji wa Kwaya ya Kurasini SDA(wenye sare) na baadhi ya Viongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Southern Nyanza Conference mara baada ya kufunga makambi ya Waumini wa Kanisa hilo jana yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(mwenye koti na tai) akiagana na waimbaji wa Kwaya ya Kurasini SDA mara baada ya kufunga makambi ya Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.
Vijana wa Pathfinder wakimvisha skafu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kwa ajili ya kufunga makambi ya Waumini wa kanisa la Waadventista Wasabato jana yaliyofanyika katika Uwanja wa Kidinda Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!