Waziri
wa Kilimo Mhe.Dkt. Charles Tizeba amewataka wamiliki wa viwanda vya kuchambua
pamba(ginners) kupeleka pamba mbegu kwenye kiwanda cha kuchakata(kutoa manyoya)
mbegu za pamba cha Quton na akasema watakaogoma kupeleka hawatanunua pamba
msimu ujao.
Waziri
Tizeba ameyasema hayo jana alipotembelea kiwanda hicho katika Kata ya Kasoli
wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwa lengo la kujionea hali ya uzalishaji wa
mbegu ya pamba inavyoendelea.
Amesema
suala la wenye viwanda vya kuchambua pamba(ginners) kupeleka pamba mbegu katika
kiwanda cha kuchakata mbegu za pamba(kuondoa manyoya) siyo la hiari na walishapewa
maelekezo, hivyo wanapaswa kupeleka pamba mbegu katika kiwanda cha Quton ili
zitolewe manyoya na baadaye zipelekwe kwa wananchi.
“
Nimeambiwa watu wa Quton wanashindwa kufanya kazi kwa shift tatu kwa siku kwa
sababu walio na mbegu kwenye viwanda vyao vya kuchambua pamba hawataki kuleta
pamba hapa, wakati wanayo maelekezo na hii siyo hiari mbegu ikishatengwa na
Bodi ya Pamba si yao” alisema Tizeba.
“Mkurugenzi
wa Bodi ya Pamba nakuagiza wapelekee ujumbe huu kwamba ginner atakayegoma kuleta
pamba mbegu hapa Quton hanunui pamba mwaka kesho, wanapaswa walete mbegu zitolewe
manyoya ziende kwa wananchi ili wapate mbegu bora, katika hili sitabembelezana
na mtu” alisisitiza Tizeba.
Aidha,
Mhe.Waziri amesema mahitaji ya mbegu ya pamba iliyotolewa manyoya kwa nchi
nzima ni takribani tani 8000, hivyo ili kufikia kiwango hicho katika siku
zilizobaki kuelekea msimu wa kilimo cha pamba, kiwanda cha Quton kinapaswa
kufanya kazi saa 24 kwa kuwa uzalishaji wa sasa wa tani 60 hadi 65 kwa saa 16
kwa siku hautaweza kufikia lengo hilo.
Wakati
huo huo Waziri Tizeba ametoa wito kwa wananchi Mkoani Simiyu kutopanda pamba sasa
kwa kuhofia mvua kukatika mapema, badala yake wasubiri taarifa rasmi ya Mamlaka
ya Hali ya Hewa juu ya hali ya mvua katika ukanda huo itakayotolewa muda mfupi
ujao,ambayo baadaye itatumika kuwashauri wakati muafaka wa kupanda, japo
alieleza kuwa taarifa ya jumla ya utabiri wa hali ya hewa inaonesha mvua
itanyesha juu ya wastani.
Pia
Mhe.Waziri amewahakikishia wananchi kuwa bei ya mbolea imeshuka, hivyo
akawataka wataalam wa Kilimo kuwaelimisha wananchi juu ya bei elekezi ya mbolea
kwa kila wilaya, ili wasiuziwe kwa bei kubwa na akasisitiza kuwa bei ya mbolea
na mbegu mwaka 2018 itapungua zaidi kwa kuwa Serikali imefuta takribani kodi 80
katika kilimo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu
unazalisha pamba kwa wingi, ambapo katika msimu wa mwaka 2016/2017 umezalisha
takribani asilimia 65 ya pamba ya nchi
nzima, hivyo akaomba wananchi wa mkoa huo wasaidiwe kupewa mikopo ya zana bora
za kilimo na pembejeo nyingine kupitia mfuko wa pembejeo ili kuongeza
uzalishaji zaidi.
Naye
Mkurugenzi wa Kampuni ya Quton Tanzania Limited Ndg. Pradyumansinh Chauhan amemuomba
Waziri wa Kilimo kuhamasisha wananchi kutumia mbegu za pamba zilizotolewa
manyoya ili kuongeza uzalishaji kwa kuwa hazishambuliwi kwa urahisi na magonjwa
na zinapunguza kiasi cha mbegu kinachotumika shambani ambapo kilogramu sita tu hutumika
kwa hekali wakati zenye manyoya hutumika hadi kilogramu 15.
Waziri
wa Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba (wa tatu kushoto) akisikiliza maelezo kutoka
wa Meneja Uzalishaji wa Mbegu,Pheneas Chikaura(kulia) katika Kiwanda cha Kuzalisha
mbegu za pamba cha Quton wakati wa ziara yake kiwandani hapo Wilayani Bariadi
Mkoani Simiyu.
Mkuu
wa Wilaya ya Bariadi, Mhe Festo Kiswaga(kulia) akiwasilisha taarifa ya Wilaya
yake kwa Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba (wa tatu kushoto) wakati
alipofanya ziara katika Wilaya hiyo Mkoani Simiyu.
Waziri wa
Kilimo, Mhe.Charles Tizeba akikaribishwa na Mkurugenzi wa Quton Tanzania
Limited Ndg.Pradyumansinh Chauhan, alipotembea Kiwanda cha kuzalisha Mbegu za
Pamba cha Quton kilichopo kata ya kasoli Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Waziri wa
Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba(kushoto) akisalimiana na Kaimu Katibu Tawala
Mkoa wa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa
ajili ya ziara ya siku moja Mkoani humo.
Waziri wa
Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba(kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM
Wilaya ya Bariadi, Mhe.Juliana Mahongo mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa
ajili ya ziara ya siku moja Mkoani Simiyu.
Kaimu Katibu
Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah akitoa taarifa ya Mkoa kwa Waziri wa
Kilimo, Dkt.Charles Tizeba (kulia) wakati alipofanya ziara katika
Wilaya ya Bariadi Mkoani humo.
Baadhi ya
Viongozi na Wataalam wa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa
Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba(hayupo pichani)
wakati alipozungumza nao kabla ya kutembelea Kiwanda cha Kuchakata mbegu za
pamba(zilizotolewa manyoya) cha Quton katika Kata ya Kasoli Mkoani Simiyu
kujionea uzalishaji wa mbegu za pamba.
Mkurugenzi wa
Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Alliance Ginnery, Ndg. Boazi Ogola(wa pili
kushoto) akimuongoza Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba (aliyeweka mkono
kifuani) na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa Simiyu kuelekea
kuona kiwanda hicho wakati wa ziara ya Waziri huyo Mkoani Simiyu.
0 comments:
Post a Comment