Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Eng. Ramo Makani amesema Wafugaji Nyuki wanayo fursa kubwa ya
kujikita katika uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kuchakata, kufungasha
na kuongeza thamani mazao ya nyuki na kutengeneza vipodozi kutokana na mazao ya
nyuki.
Mhandisi
Makani ameyasema hayo jana wakati
alipozungumza na wafugaji wa nyuki na wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya
kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa yaliyofanyika katika Kijiji cha Isengwa Wilaya
ya Itilima Mkoani Simiyu, chini ya Kauli Mbiu “UFUGAJI NYUKI KIBIASHARA
UNACHANGIA KATIKA UKUAJI WA VIWANDA”
Amesema
Mazao ya Nyuki ni malighafi ya Viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya vyakula
vinavyotumia asali, viwanda vya dawa na vipodozi na viwanda vya utengenezaji
vinavyotumia nta katika kuzalisha maturubai, dawa za kung’arisha viatu na
bidhaa nyingine, hivyo wafugaji wanao
wajibu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki na ujuzi wa kuyaweka katika
ubora na kuyaongezea thamani.
Aidha, ametoa wito kwa wafugaji
wa nyuki kuungana katika vikundi vyenye usajili ili waweze kuzalisha asali kwa
wingi na yenye kufanana, kwa kuwa ikiwa watazalisha kila mmoja kwa utaratibu
wake, asali hiyo haiwezi kuchanganywa na itakuwa na ubora na sifa tofauti,
lakini ikiwa wataungana na kuzalisha asali nyingi kwa pamoja wakaipima kwa
viwango vya ubora unaotakiwa wataweza kupata soko.
Sanjali na hilo amesema Serikali
itahakikisha inawaunganisha wafugaji nyuki na walaji wa ndani na nje na akabainisha
kuwa kwa miaka zaidi ya 11 imekuwa na ushirikiano na soko la Ulaya ambapo
sampuli za asali kutoka maeneo mbalimbali zimepelekwa Ulaya na taarifa za
maabara zinathibitisha kuwa asali ya Tanzania ni salama kwa afya ya mlaji.
Aidha, amesema katika kuongeza
uzalishaji wa mazao ya nyuki Serikali pia inaendelea kutoa elimu kwa wafugaji
wa nyuki kuachana na matumizi ya mizinga
ya asili ambayo ni duni na inachukua nafasi kubwa wakati uzalishaji wake ni
mdogo na kuwahamasisha kuanza kutumia mizinga ya kisasa.
“
Nawaagiza Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki nchini na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania kupitia jukwaa hili, kwamba mbuni njia rafiki ya
kuweka msisitizo katika utoaji wa elimu, uhamasishaji na kupima mafanikio kila
mwaka; taarifa ya utekelezaji wa maagizo haya itolewe mara kwa mara, taarifa ya
kwanza baada ya agizo hili itolewe katika siku ya maadhimisho kama haya mwaka
kesho 2018” aliagiza Naibu Waziri.
Katika hatua nyingine Mhe. Makani
amepongeza juhudi zinazofanywa na Mradi wa LVEMP II katika kuboresha mazingira na
kubainisha kuwa pamoja na kuhifadhi rasilimali za asili za Bonde la Ziwa
Victoria ambayo husaidia kutunza vyanzo vya maji na mazingira hayo yanafanywa kuwa mazingira
bora kwa ufugaji nyuki, ambapo katika wilaya ya Itilima kuna vikundi 22 vyenye
mizinga 2080 ya nyuki vinavyofadhiliwa na LVEMP.
Akitoa salamu za Mkoa kwa niaba
ya Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Chele Ndaki amesema idadi ya wafugaji na
mizinga ya nyuki imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo kwa sasa kuna jumla ya
vikundi 91 vyenye jumla ya mizinga 5824 na akaahidi kuwa mkoa utaendelea
kusimamia uboreshaji wa mazingira ya ufugaji nyuki na kusimamia vikundi vinavyoanzishwa
katika Halmashauri., ili wafugaji wanufaike na kujiimarisha kiuchumi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Ndg.Herberth Haule amesema
shughuli ya ufugaji wa nyuki inasaidia
katika uhifadhi wa mazingira na kujenga
uchumi kwa wananchi hususani vikundi vinavyojishughulisha na kazi hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Misitu na
Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Ezekiel Mwakalukwa amesema
Tanzania ni miongoni mwa nchi Tano za Afrika zinazoruhusiwa kuuza asali yake
katika soko la Ulaya na nchi ya China.
Nao wafugaji wa nyuki na
wajasiriamali wa mazao ya nyuki wameiomba Serikali pamoja na wadau wengine
kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza vifungashio kwa kuwa suala hilo ni
changamoto kwao ambayo inawalazimu
kuagiza vifungashio nje ya nchi kwa kutumia gharama kubwa.
Maadhimisho ya Siku ya Kutundika
Mizinga ya Nyuki Kitaifa kwa mwaka 2017 yameadhimishwa kwa mara kwanza Mkoani
Simiyu yakiwa ni maadhimisho ya tano kufanyika hapa nchini, ambapo kwa mara ya
kwanza yalifanyika mwaka 2013 Mkoani
Singida.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Eng. Ramo Makani (Mb)(kulia)akitundika Mzinga katika Banda la Nyuki la Kikundi cha Wafugaji Nyuki cha Malela wakati wa Maadhimisho ya siku ya kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa yaliyofanyika jana katika Kijiji cha Isengwa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Eng. Ramo Makani (Mb)(kulia)akitundika Mzinga katika Banda la Nyuki la Kikundi cha Wafugaji Nyuki cha Malela wakati wa Maadhimisho ya siku ya kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa yaliyofanyika jana katika Kijiji cha Isengwa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
0 comments:
Post a Comment