Mamlaka ya Mawasiliano
hapa nchini (TCRA) imetoa elimu kuhusu huduma ya kuhama kutoka Mtandao mmoja wa
Simu kwenda Mtandao mwingine bila kubadili Namba ya Simu(Mobile Number
Portability- MNP) mkoani Simiyu.
Akizungumza na
waandishi wa Habari Mjini Bariadi Mhandisi Mwandamizi wa Mawasiliano Mwesigwa
Felician kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania( TCRA), amesema huduma hii ni
ya hiari na inampa uhuru na kumwezesha
mtumiaji wa huduma ya mawasiliano kuhamia mtandao wowote anaoutaka na kuendelea
kupata mawasiliano bila kulazimika kubadili namba yake ya simu.
“Namba ya simu ya Mteja
itabaki ile ile na itakuwa ni kitambulisho chake, yaani (NAMBA YAKO KITAMBULISHO
CHAKO) kokote atakapohamia watu watampata, hakuna haja ya kuwataarifu marafiki,familia,
wafanyakazi wenzake au washirika wenzake
katika shughuli zake kama ilivyo sasa. Tunatoa elimu hii kwenu waandishi wa
habari ili na ninyi muifikishe kwa wananchi kupitia kazi zenu” amesema Mhandisi
Mwesigwa.
Amesema huduma hii
inamwezesha mtumiaji wa huduma za mawasiliano kuchagua mtoa huduma mwenye
huduma bora zaidi(quality of service), huduma nzuri kwa wateja(customer care
services), ubunifu katika kutoa huduma zake hivyo kuongeza ushindani kwenye
sekta ya mawasiliano na kuchochea utoaji huduma bora na zenye gharama nafuu.
Ameongeza kuwa huduma
hii inatolewa kwa wateja wa malipo ya kabla(pre paid) na malipo baada ya
huduma(post paid) kupitia vituo vya mauzo au wakala anayetambuliwa mtoa huduma (Makampuni
ya Mawasiliano/Simu), ambapo watumiaji wa mawasiliano watakaohitaji huduma hiyo
watatembelea maeneo hayo ili kupewa utaratibu wa kuhama.
“Mtu anayetaka kuhama
kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine bila kubadiliha namba yake
anapaswa kufika katika Vituo vya mauzo au wakala wa mtandao anaotaka kuhamia, kupata
utaratibu na akiona ipo haja ya kuhama tena itamlazimu akae kwa mtoa huduma
huyo mpya kwa muda usiopungua siku 30 kabla ya kurudi kwa yule awali au kuhamia
kwa mwingine” amesisitiza Mhandisi Mwesigwa.
Kwa upande wake Naibu
Mkurugenzi wa Masuala ya Watumiaji wa Bidhaa za Mawasiliano, kutoka Mamlaka ya
Mamlaka ya Mawasiliano, Thadayo Ringo amesema huduma hii hapa nchini imeanza
Machi Mosi mwaka huu na mpaka kufikia mwezi Juni 2017 takribani wananchi 15,000
walikuwa wameshaitumia huduma hii.
Aidha, Ringo ameongeza
kuwa Tanzania ni nchi ya Tisa Barani Afrika kutoa huduma hii katika mawasiliano,
ambapo amebainisha nchi nyigine zinazotoa huduma ya kuhama kutoka mtandao mmoja
kwenda mwingine bila kubadili namba (MNP) kuwa ni Kenya, Rwanda, Botswana,
Afrika ya Kusini, Ghana, Senegal, Namibia na Misri.
Huduma hii ya kuhama kutoka mtandao mmoja kwenda
mwingine bila kubadili namba ya simu ya kiganjani, inatolewa kwa watumiaji ambao
namba zao zinatumika yaani hazijafungiwa au kusimamishwa kwa muda.
0 comments:
Post a Comment