Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi Wilayani Bariadi mkoani humo
kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF).
Mtaka ametoa wito
huo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngulyati wilayani
Bariadi wakati wa ziara yake yenye lengo la kusikiliza kero mbalimbali za
wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Amesema
azma ya Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2020 Watanzania wote wawe wamejiunga na
Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) au Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hivyo
akawahamasisha wananchi ambao bado hawajajiunga na CHF kujiunga kwa kuwa
gharama yake ni nafuu.
“Watu
wa Ngulyati ni wafanyabiashara wazuri, wafanyakazi wazuri, wakulima wazuri
ningetamani kuwaona wote hapa mnakuwa na kadi za Mfuko wa Afya ya Jamii ambazo
zinapatikana kwa gharama ya shilingi 10,000, hii ni sawa na kuku mmoja tu mnapata
matibabu watu sita kwa maana ya baba,
mama na watoto wa nne” amesema.
Ameongeza
kuwa Serikali inaendelea kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya ili
wananchi waweze kupata huduma bora, ambapo Serikali kupitia Mradi wa RBF(Result
Based Financing/Kulipa kulingana na Matokeo) imetoa fedha kwa ajili ya
kuboresha huduma.
Akitoa
ufafanuzi wa fedha hizo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi,
Ndg.Abdallah Malela amesema, kupitia mradi wa RBF Halmashauri hiyo imepokea
shilingi milioni 260, zilizogawanywa katika vituo vilivyopo 26 vya kutolea
huduma za afya ambapo kila kituo kimepokea shilingi Milioni 10 ili kuboresha
utoaji wa huduma za Afya.
Aidha,
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga
kufuatilia na kuhakikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi anawasilisha
kwake taarifa ya fedha za Mradi wa RBF alizopokea na kazi zilizofanyika katika
vituo vya kutolea huduma.
“Mhe.
DC umesikia hapa hawa watu wamepokea fedha toka mwezi saba mwaka huu na leo
ndio wamekaa kikao cha mpango, maana
yake ni kwamba mwezi wa nane wananchi hawajapata huduma zilizokusudiwa na
Wizara ya Afya, na naamini yanayofanyika kwenye kituo hiki yapo katika vituo
vyako vyote, sasa nimuombe Mkurugenzi wa Mji Jumatatu atuletee taarifa ya mpango uliotekelezeka” amesema Mtaka.
Mkuu
wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
kuwa atalifuatilia suala hilo pamoja na kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa
katika ziara hiyo na ameahidi kuwachukulia hatua watumishi watakaoshindwa
kutimiza wajibu wao katika kuwahudumia wananchi.
Kuhusu
suala la taratibu za uwekaji wa umeme wa REA awamu ya III kwa wananchi na
Taasisi za Umma ambalo liliwasilishwa na wananchi akiwemo Mwl. Daudi Jackson,
Mkuu wa Mkoa, Mhe.Anthony Mtaka amesema atakutana na Meneja wa TANESCO Mkoa siku
ya Jumatatu Septemba 04, ili wajadili namna na kushughulikia suala hilo.
Katika
hatua nyingine Mtaka amemtaka Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kuhakikisha Mhandisi wa Ujenzi wa
Halmashauri anafika eneo la ujenzi wa Soko la Ngulyati Jumatatu tarehe 04
Septemba kukutana na viongozi wa Kijiji na Kata, kwa ajili ya kuanza mpango wa
ujenzi wa soko hilo ili kutatua kero ya ukosefu wa soko na kuwawezesha wananchi
kupata sehemu ya kuuzia bidhaa zao.
Wakati
huo huo Mtaka amewataka wananchi kutumia vizuri msimu wa kilimo, kulima mazao yanayostahimili
ukame na akawasisitiza kutunza chakula walichokipata katika msimu uliopita kwasababu
Serikali haitakuwa na chakula cha msaada.
Kaimu Mganga Mkuu wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi akitolea ufafanuzi masuala mbalimbali ya Afya
yaliyoulizwa na wananchi wa Kata ya Ngulyati wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka aliyoifanya kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na
kuzitafutia ufumbuzi.
Diwani wa Kata ya
Ngulyati Mhe.Mganga Ndamo Kanagana akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngulyati
wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka aliyoifanya kwa
lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Baadhi ya Viongozi wa
Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Bariadi wakisikiliza kwa makini ufafanuzi na
maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) juu ya
kero na hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi wakati wa ziara yake
aliyoifanya katika kata ya Ngulyati wilayani Bariadi kwa lengo la kusikiliza
kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Kikundi cha Burudani
cha Msanii Polepole kutoka Ngulyati kikitoa burudani ka wananchi na viongozi
katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) aliyoifanya
katika kata ya Ngulyati wilayani Bariadi kwa lengo la kusikiliza kero za
wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Baadhi ya wananchi wa
Kata ya Ngulyati wilayani Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati wa ziara yake yenye lengo la
kusikiliza kero mablimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
0 comments:
Post a Comment