Baadhi ya Wakurugenzi wa Mifuko na Mashirika ya Serikali hapa nchini
wametembelea na kukagua maeneo yanayokusudiwa kutumika katika ujenzi
wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza bidhaa zinazotumika
hospitalini zitokanazo na zao la pamba na kiwanda cha maji tiba(drip)
mkoani SIMIYU.
Maeneo yaliyotembelewa ni kijiji cha
Nyamikoma Halmashauri ya Wilaya Busega
,kijiji cha Isenga Halmashauri ya Wilaya
Bariadi na Mtaa wa Katenga Halmashauri
ya Mji wa Bariadi.
Akizungumza katika kikao cha
majumuisho ya ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya
Viwanda Tanzania(TIRDO), Profesa Mkumbukwa Mtambo amesema kuanzishwa kwa
viwanda hivyo kutasaidia kuokao fedha takribani shilingi bilioni 19
zinazotumika kununua maji tiba na shilingi bilioni 29 kununua bidhaa za
hospitali zitokanazo na pamba kwa mwaka, ambavyo vyote kwa sasa vinanunuliwa
nje ya nchi.
Profesa Mtambo ameongeza kuwa
pamoja na kuokoa fedha viwanda hivyo vitatoa ajira za moja kwa moja kwa
Watanzania 1600 na ajira nyingine 5000 hivyo vitachangia katika kupunguza
changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Tanzania kwa
ujumla.
Aidha, amefafanua kuwa upembuzi
yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hivi vyote viwili utkaofanywa na TIRDO unatarajia
kuanza wiki sita kuanzia sasa, hivyo akawaeleza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa
mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo watawasilisha taarifa itakayosaidia pia
kuwaandaa wakulima kuzalisha pamba itakayohitajika kwa ajili kiwanda cha bidhaa
za afya zitokanazo na pamba.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya
Dawa(MSD), Laurean Rugambwa amesema jumla ya lita 1,500,000 za maji tiba(drip) hutumika
hapa nchini kwa mwaka, ambayo huagizwa nje ya nchi hivyo ameuhakikishia uongozi
wa Mkoa kuwa bidhaa zitakazozalishwa katika viwanda hivyo zitapata soko la
uhakika kwa kuwa zitanunuliwa na Bohari hiyo kwa ajili ya matumizi ya vituo mbalimbali
vya kutolea huduma za Afya hapa nchini.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Bernard Kaonga amesema wanaunga mkono ujenzi wa viwanda hivyo
na wamekubali kuingia kwenye ubia na TIRDO pamoja na wadau wengine kama wadau
wakubwa wa afya, kwa kuwa viwanda hivyo vitasaidia kupunguza gharama ya
kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema ni vizuri Mkoa ukapata mapema taarifa ya
Upembuzi yakinifu wa kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba ili
kuendana na maandalizi ya msimu wa kilimo cha pamba, ambapo amesisitiza kuwa
mkoa huo umejipanga kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni 70 mpaka kilo
milioni 130 kwa mwaka 2018.
Ameongeza kuwa viwanda hivi
vitakuwa na manufaa makubwa kwa wanachi wa mkoa huo ikiwepo suala la ajira kwa watu zaidi ya 6500 wanatarajiwa kuajiriwa
katika kiwanda kitakachozalisha bidhaa za hospitali zitokanazo na zao la pamba.
“Kwa watu wa Simiyu kupata mradi
utakaoajiri watu 1500 moja kwa moja, ajira nyingine 5000 pamoja na ajira za
kwenye (ginneries) viwanda vyetu vya kuchambua pamba tutakuwa tumefanya kitu;
ni lazima tutengeneze kura mpya za Mhe.Rais mwaka 2020, maana wapiga kura wengi
wa mwaka 2020 watakuwa wapya ambao hitaji lao kubwa ni ajira na katika umri
wetu huu ni lazima tujibu” amesema Mtaka.
Naye Katibu Tawala Mkoa Simiyu,
Ndg.Jumanne Sagini amesema Wakurugenzi wa Halmashauri, Madiwani, Viongozi wa Serikali za Vijiji na Mitaa na
wananchi maeneo yote yaliyotembelewa wamekubali kutoa maeneo hayo kwa ajili ya
uwekezaji wa viwanda, hivyo ni vema maamuzi ya mahali viwanda hivyo viwili
vitakapojengwa yakatolewa mapema na wawekezaji hao ili yaweze kuandaliwa hati miliki.
Wabia wakuu katika Ujenzi wa
Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za hospitali zitokanazo na pamba na kiwanda cha
kutengeneza maji tiba(maji ya drip) Mkoani Simiyu ni pamoja na Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya(NHIF),Bohari ya Dawa(MSD),Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),Shirika
la Viwango nchini(TBS), Benki ya Maendeleo(TIB),Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi(WCF), NEMC,TEMDO na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda
Tanzania(TIRDO) ambao ndiyo wasimamizi wa Miradi hiyo.
0 comments:
Post a Comment