Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka amekabidhi pikipiki za maafisa Ugani na Gari la Idara ya Kilimo wilayani Itilima na kusisitiza kuwa vyombo
hivyo vitumike kwa ajili ya kuwafikia wananchi ili kuongeza tija katika
uzalishaji wa mazao hususani zao la pamba.
Vyombo hivyo ambavyo awali
vilikuwa vimeegeshwa vimefanyiwa matengenezo kwa gharama za Halmashauri ya Wilaya
ya Itilima ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka, aliyoyatoa wakati wa ziara yake aliyofanya katika Halmashauri zote Mkoani humo
kwa lengo la kuhimiza kilimo.
Mtaka amesema zao la pamba
linachangia mapato ya Halmashauri kwa kiasi kikubwa Mkoani humo hivyo Wakurugenzi wanapaswa kuhakikisha vyombo
vya usafiri vinafanya kazi muda wote wa msimu ili wataalam waweze kuwafikia
wakulima(wananchi) na kuwasaidia kuzalisha kwa tija.
“ Mwaka 2016/2017 Itilima ilipata
milioni 500 kutokana na pamba lakini Idara ya Kilimo iliyosababisha Pamba kuleta
fedha hizo haikutengewa fedha kwenye
bajeti, haikuwa na gari wala pikipiki” amesema Mtaka.
“ Wakati wa kilimo hakuna magari kwa ajili ya kuwafikia wakulima, wakati
wa kukusanya ushuru magari yote yanakuwa mazima na yanawekwa mafuta ili
kufuatilia ushuru, maelekezo yangu kwa Halmashauri zote ni kwamba wakati wote wa
msimu wananchi kuanzia wanapoandaa mashamba ni lazima pikipiki na magari
yafanye kazi kwenye Idara ya Kilimo ” amesititiza Mtaka.
Wakipokea pikipiki na gari
la Idara Maafisa Ugani hao wameahidi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha
wanawafikia wakulima wote walio katika maeneo yao, ili kupitia utaalamu wao waweze
kuwasaidia kuongeza uzalishaji, ambapo wamekusudia kuongeza uzalishaji wa pamba
kwa mwaka 2017/2018 kutoka kilo 650 hadi 1200 kwa ekari.
Mkoa wa SIMIYU ni mkoa
unaozalisha pamba kwa wingi ambapo unazalishaji asilimia 60 ya pamba yote hapa
nchini
0 comments:
Post a Comment