Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anthony Mtaka amewasisitiza wakulima Mkoani humo kulima mazao ya biashara yenye tija hasa zao la pamba kwa
kuzingatia Mkoa huo upo katika mchakato wa utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda cha
bidhaa za afya zitokanazo na zao la pamba.
Msisitizo huo ameutoa jana wilayani Maswa katika ziara yake ya kuhamasisha kilimo kuelekea msimu wa kilimo na kueleza kuwa wakulima wanapaswa kuutumia vema msimu
huu kwa kulima zao la pamba ambalo litawapatia fedha nyingi.
Mtaka alieleza kuwa wakulima wa Maswa na Mkoa mzima wageuze ujenzi wa
kiwanda cha bidhaa za afya kuwa ni fursa ya kujiongezea kipato kwa kuzalisha
zaidi zao la pamba ambalo ndilo litakuwa malighafi kuu katika uzalishaji
wa kiwanda hicho.
Aidha alisema katika msimu msimu huu mpya wa mwaka 2017/2018
wakulima hao wanatakiwa kuondoa mazalia ya pamba yaliyobaki mashambani mwao na
kisha kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo hicho.
"Katika msimu huu ninawaomba wakulima wote waondoe mazalia ya zao la
pamba yaliyobaki mashambani kwa kuyachoma moto ili wasije kuharibu na
kuambukiza magonjwa katika mbegu mpya na bora watakazozitumia...pia katika
kupanda mpande kwa kuzingatia sentimeta 90 hadi 40 zilizoainishwa kitaalamu
kutoka mstari hadi mstari....alisema Mtaka
Aidha wakulima hao hawakusita kueleza kero zao na kuitupia lawama bodi ya
pamba kwa kushindwa kusimamia zao hilo huku wakidai kutoichafua kwa
kuweka maji na mchanga katika zao hilo.
Irene Joseph mkulima kutoka katika kata ya Kadoto alifafanua kuwa wakulima
wamekuwa wakionewa na kusingiziwa visingizio vingi juu ya uchafuzi wa zao
hilo ,huku akieleza tuhuma hizo kuwa si za kweli na kubainisha kuwa bodi
ya pamba inapaswa kutimiza wajibu wake katika
kulisimamia zao la pamba na kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima .
Naye afisa kilimo wa Wilaya ya Maswa Christopher Simwimba amewataka wakulima
kutumia mbolea ya samadi katika kuongeza rutuba kwenye mashamba yao .
Afisa huyo aliongeza kusema kuwa wakulima wanatakiwa kubadilika na kulima
kisasa ili waweze kuendana na falsafa ya serikali ya viwanda ambapo wakulima
ndio wanategemewa wao kuwa ni wazalishaji wa malighafi za viwandani.
Naye mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt Seif Shekilage alisema kuwa katika kuhakikisha
wanaboresha na kuliinua zao la pamba Halmashauri yake imeweza kuwasaidia
vikundi vya vijana na wanawake wanajihusisha na kilimo kuwapatia mkopo wa
Milioni 50 kwa vikundi 16 vinavyotarajia kulima zao la pamba kwa msimu huu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katikati (wa tatu kushoto)
akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Maswa Paul Jidai,(
kushoto ) Kaimu Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dk Seif Shekalage akitoa ufafanuzi wa namna Wilaya
yake ilivyojipanga kuongeza uzalishaji wa zao la pamba.
Wakulima kutoka katika kata 36 za Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wakiwa
katika mkutano wa pamoja Viongozi wa Mkoa
na Wilaya(hawapo pichani) ukiwa na lengo la kujadili na kupokea
maelekezo ya kilimo katika msimu mpya wa 2017/2018.
0 comments:
Post a Comment