Saturday, July 28, 2018

SIMIYU YAJIPANGA KUONGEZA UFAULU MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2018

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa huo umedhamiria kuongeza ufaulu na kufikia nafasi ya kwanza hadi ya tisa (single digit) katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2018.


Mtaka ameyasema hayo katika kikao kati yake na Wakuu wa Shule za Sekondari mkoani Simiyu chenye lengo la kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne baada ya kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2018.

“Ni lazima twende kwenye ‘single digit’ matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, haiwezekani tufanye vizuri kidato cha sita tushindwe kufanya vizuri kidato cha nne, uthubutu tuliuonesha kuwa tunataka kuwa mkoa unaofanya vizuri kielimu tumaanishe, mwaka jana watu walikuwa wanahamisha watoto wao lakini mwaka huu wanaomba kuhamia” alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka amewashauri wazazi kuwapunguzia kazi wanafunzi wa madarasa yote ya mitihani kwa shule za msingi na sekondari mkoani humo, ili kuwapa nafasi ya kupata muda mwingi wa kujisomea na kujiandaa na mitihani.

Wakati huo huo amewaagiza Wakuu wa Shule zote za Serikali za bweni mkoani Simiyu Sekondari kuongeza muda wa kuzima taa usiku kutoka saa nne usiku hadi saa sita kwa wanafunzi wa Kidato cha nne na sita, ili kutoa nafasi kwa  wanafunzi kupata muda mwingi wa kujisomea.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi wamemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka na kulipokea  agizo lake la kuzitaka  Shule zote za Serikali za Sekondari kuongeza muda wa kuzima taa usiku kutoka saa nne usiku hadi saa sita kwa wanafunzi wa Kidato cha nne na sita ili waweze kupata muda mwingi wa kujisomea.

“Tunamshukuru Mkuu wa mkoa kwa kuagiza wanafunzi wasizimiwe taa hadi saa sita usiku, hapa shuleni kwetu ratiba ya kujisomea inaanza 11:00 hadi saa 12:00 asubuhi, baadae tunaanza vipindi, usiku tunaanza kusoma kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 6:00 usiku, hii inatupa muda zaidi wa kujisomea” alisema Erick Kamala mwanafunzi wa Kidato cha Sita, Shule ya Sekondari Bariadi.

Katika hatua nyingine wanafunzi wameomba kambi za Kitaaluma kwa madarasa ya mtihani ziwe ajenda ya kudumu ya  Mkoa kwa kuwa wamekiri kambi zilizopita zimechangia mkoa huo kuwa na matokeo mazuri.

“ Tunaomba kambi ziendelee kuwepo kwa madarasa ya mitihani, mwezi wa sita tulipokuwa kambi mimi nilijifunza vitu vingi kwa walimu na wanafunzi wa shule za jirani tuliokuwa nao kambini, naomba tuwekewe tena kambi mwezi wa tisa kabla ya mtihani wa Taifa” alisema Faudhia Haruni mwanafunzi wa kidato cha nne  shule ya sekondari Bariadi.

“Kambi za kitaaluma zitatusaidia kubadilishana uzoefu na mbinu za kujibu mitihani na kukabiliana na (topic) mada zenye changamoto, tumeona wenzetu zimewasaidia sana nanina uhakika na sisi tutafanya vizuri zaidi ya mwaka huu” alisema William Charles  mwanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Bariadi.

Aidha, katika kikao cha wakuu wa shule na mkuu wa Mkoa wa Simiyu, wakuu wa shule walieleza mikakati yao katika kuhakikisha mkoa huo unafanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne kama ilivyokuwa kwa Kidato cha Sita mwaka 2018, ikiwa ni pamoja na kuendeleza kambi hizo za kitaaluma.

“ Kambi za Kitaaluma zinawasaidia sana wanafunzi na ni suala ambalo wazazi wanalikubali, mwaka jana niliwatoa wanafunzi wangu kuwapeleka shule ya Itinje wengine Mwamalole lakini wazazi ndiyo waliochangia” alisema Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwamalole, Mwl.Marco Mwendamkono.

“ Sisi tumelipokea wazo lako Mkuu na hatuna muda wa kupoteza, kila siku saa 12:00 asubuhi, wanafunzi wanaanza kujisomea saa 12:30 asubuhi mwalimu anatoa swali la siku baaada ya hapo ni usafi, saa 1:30 asubuhi hadi saa 8:50 wanakuwa darasani, baada ya kula saa 10:00 jioni tena wanaingia darasani hadi saa 12:00 jioni; baada ya chakula ni ibada na kuanzia saa 2:00 hadi saa 6:00 usiku kujisomea lakini wanaohitaji kuendelea baada ya hapo hawazuiwi” Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, Mwl. Konga Jackson.

Mkoa wa Simiyu katika matokeo ya mtihani waTaifa kidato cha sita mwaka 2018 umefanya vizuri na kushika nafasi ya 10 kifaifa kutoka nafasi ya 26 mwaka 2017, huku kambi za kitaaluma zikitajwa na wadau mbalimbali kuwa miongoni mwa mikakati iliyoifikisha katika nafasi hiyo.
MWISHO


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa wa Kidato cha nne na sita Shule ya Sekondari Bariadi mara baada ya kufunga kikao chake na wakuu wa shule kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(katikati)  akizungumza na Wakuu wa Shule kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2018.
Erick Kamala mwanafunzi wa Kidato cha Sita, Shule ya Sekondari Bariadi akichangia hoja katika kikao katika wanafunzi wa shule hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkula akichangia hoja katika kikao kati ya Wakuu wa Shule na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kilichofanyika Mjini Bariadi, kwa lengo la kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2018.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi, Mwl. Deus Toga akizungumza na katika kikao kati ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kilichofanyika shuleni hapo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Shule ya Itilima, akichangia hoja katika kikao kati ya Wakuu wa Shule na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kilichofanyika Mjini Bariadi, kwa lengo la kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2018.

Mwanafunzi wa Kidato cha Sita, Shule ya Sekondari Bariadi akichangia hoja katika kikao katika wanafunzi wa shule hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kilichofanyika Mjini Bariadi.
Faudhia Haruni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Bariadi, akichangia hoja katika kikao katika wanafunzi wa shule hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kilichofanyika Mjini Bariadi.
Afisa Taaluma wa Mkoa, Mwl.Onesmo Simime akizungumza na wanafunzi katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo na wanafunzi wa Kidato cha Nne na Sita wa Shule ya Sekondari Bariadi, kilichofanyika shuleni hapo.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne na Sita wakishangilia baada ya kupokea agizo la Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa Wakuu wa Shule za Sekondari za Serikali(za bweni) kuwataka wasiwazimie taa wanafunzi hadi saa sita usiku ii kuwaongezea muda wa kujisomea, katika kikao kilichfanyika shuleni hapo.
Mwanafunzi wa Kidato cha Sita, Shule ya Sekondari Bariadi akichangia hoja katika kikao katika wanafunzi wa shule hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa wa Kidato cha nne na sita Shule ya Sekondari Bariadi mara baada ya kufunga kikao chake na wakuu wa shule kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2018.


Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwamalole, Mwl.Marco Mwendamkono. akichangia hoja katika kikao kati ya Wakuu wa Shule na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kilichofanyika Mjini Bariadi, kwa lengo la kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2018.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!