Saturday, September 1, 2018

RC MTAKA AONGOZA HARAMBEE UJENZI WA BWENI LA WASICHANA MEATU ZAIDI YA MILIONI 84 ZAPATIKANA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe. Anthony Mtaka ameongoza Harambee ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo Wilayani Meatu ambapo jumla shilingi milioni 84,876,950/= zimepatikana, fedha taslimu ikiwa shilingi 18,776,000/= ahadi 66,100,000/= pamoja na mifuko 253 ya saruji, mbuzi 12  na ng’ombe 3.

Akizungumza na wananchi na viongozi wa Chama na Serikali Mtaka amewapongeza viongozi wa kata ya Mwanjolo kwa jitihada walizofanya kwa kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapata bweni, huku akiwasisitiza wananchi kuona umuhimu wa kuwekeza katika elimu ili kuuweka mkoa huo kwenye ushindani na mikoa mingine.

Aidha, ametoa wito kwa Madiwani wa kata zote mkoani humo kuiga mfano wa Kata ya Mwanjolo ambapo amesema viongozi na wananchi wanapaswa kuona uchungu na kuona haja ya kuwa na mabweni kwa watoto wa kike ili waondakane na vishawishi na changamoto nyingine zinazowakabili ili waweze kufikia malengo yao.

“Madiwani wetu hili jambo waige, haiwezekani hawa wasichana wadogo wanaenda kupanga kwenye vijiji pateni uchungu watoto wa kike wajengewe hosteli, Mungu ametupa ardhi, mifugo, nguvu za kufanya kazi, tukishikamana kama watu wa Mwanjolo, watoto wetu wa kike wote watapata mabweni”

“Mwanjolo wametuamasha, niwaombe waheshimiwa madiwani na viongozi wenzangu kwenye wilaya zote za Mkoa wa Simiyu moto huu uliowashwa hapa Mwanjolo uende kwenye kata zote, tuanze kujenga mabweni ya watoto wa kike wanapofaulu kwenda kidato cha kwanza wakae shule wasitembee njiani wakaanza kupewa lift za baiskeli na bodaboda” alisema Mtaka

Ameongeza kuwa kwa sababu elimu ni kipaumbe cha kwanza cha mkoa ni vema viongozi wote mkoani humo wakaweka dhamira kuwa kufikia mwaka 2020 wanafunzi wa kike wote wanaosoma shule za sekondari mkoani Simiyu wakae bweni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mhe. Luhaga Mpina ametoa wito kwa Wananchi hususani jamii ya wafugaji kuchangia na kuunga mkono jitihada mbalimbali za maendeleo ya elimu ili watoto wa jamii za kifugaji waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Wakati huo huo amewahimiza vijana wanaotoka katika jamii za kifugaji kusoma kwa bidii ili waweze kuzisaidia jamii zao kufuga ufugaji wenye tija utakaowaletea manufaa.

Nao wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Mwanjolo wamewashukuru viongozi na wananchi ambao wamechangia ujenzi wa bweni, ambapo wamesema endapo bweni hilo litakamilika litawasaidia kuondokana na vishawishi mbalimbali vilivyokuwa vikisababisha baadhi yao kupata ujauzito na kushindwa kumaliza masomo yao.

“Kukamilika kwa bweni kutatusaidia kutatua changamoto tunazokutana nazo sisi wasichana hasa suala la mimba, kuna wenzangu nilioanza nao kidato cha kwanza mwaka 2016 hawapo shuleni sasa hivi sababu ya mimba, naamini tukikaa bweni tutakuwa salama  na tutapata muda mwingi wa kujisomea kwa kuwa hatutatembea mwendo mrefu tena”  Eunice Kapombe mwanafunzi Kidato cha Tatu.

Kwa upande wao wazazi na walezi wa baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwanjolo wamesema ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo utakuwa msaada mkubwa kwa watoto wa kike katika kuwawezesha kufikia kwenye malengo yao,kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakikatisha masomo kutokana na mimba zinazosababishwa na vishwawishi wanavyopata kwa kutembea mwendo mrefu kwenda shule na baadhi yao kupanga vijijini.

Harambee ya ujenzi wa Bweni la Wasichana Shule ya Sekondari Mwanjolo iliyofanyika Shuleni hapo Agosti 31, 2018,  imehusisha viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya ya Meatu, Wadau mbalimbali wa Maendeleo na wananchi, ambapo mpaka kukamilika kwa Bweni hilo jumla ya shilingi 125,024,504.35 zitahitajika.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akichangia katika Harambee ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu, Mhe. Luhaga Mpina akichangia katika Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe. Pius Machungwa akipokea michango kutoka kwa Madiwani na baadhi ya watendaji wa Halmashauri hiyo katika Harambee ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.
Baadhi ya Wananchi wa Kata ya Mwanjolo wakichangia fedha katika Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.
Baadhi ya Wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Mwanjolo wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioshiriki katika Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati wakiwa katika Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani wakati wakiwa katika Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.

Mkuu Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  akiwaelezea viongozi wa kata ya Mwanjolo mbele ya wananchi na namna walivyofanikisha Harambee ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo, (kushoto) Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwanjolo, Bw.Abel Mpina,(wa pili kulia) Diwani wa Viti Maalum Kata ya Mwanjolo, Mhe. Consolata Lushu na kulia ni Diwani wa Kata ya Mwanjolo, Mhe. Jeremiah Jilya.
Baadhi ya Wananchi wa Kata ya Mwanjolo wakichangia fedha katika Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Mwanjolo, Mhe. Consolata Lushu (kulia) akimshukuru Mkuu Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka mara baada ya kuchangia shilingi milioni tano kwenye Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo
Mkuu Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akimshukuru Mzee maarufu kutoka Katika Kijiji cha Jinamo kwa kutoa mchango wake wa ng’ombe mmoja na fedha taslimu shilingi 100,000/= katika Harambee  ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo wilayani Meatu , ambayo ilifanyika Agosti 31, 2018 shuleni hapo.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!