Friday, March 8, 2019

NAIBU WAZIRI MGUMBA: MEATU MMECHAGULIWA KUZALISHA MBEGU ZA PAMBA ZIGATIENI KANUNI ZA KILIMO BORA TUPATE MBEGU BORA

Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba amewataka wakulima  wa pamba kata ya Mwabusalu wilayani meatu Mkoani Simiyu iliyochaguliwa kuzalisha mbegu za pamba kuzingatia kanuni za kilimo bora lengo likiwa kupata mbegu bora zitakazotumika katika maeneo yanayolima zao hilo hapa nchini.


Ameyasema hayo akiwa  kwenye ziara ya kikazi wilayani hapo  yenye lengo la kukagua shughuli za kilimo, kusikiliza kero za wakulima katika kujiletea maendeleo wakati akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye  kata ya mwabusalu iliyopo wilayani hapo.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo Mgumba, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani  amesema kuwa bado wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima waliopewa dhamana ya kuzalisha mbegu za pamba kutochanganya mazao huku akiongeza kuwa mbegu hiyo itazalishwa ya kutosha.

“Mbegu inazalishwa hapa Mwabusalu na baadaye inapelekwa maeneo mengine yanayolima pamba nchini, isingependeza kukawa na maotea kwenye eneo ambalo limepewa dhamana ya kuzalisha mbegu, tunaendelea kuwaelimisha wakulima na kuhakikisha kuwa maotea yasiwe sehemu ya pamba itakayonunuliwa kwa ajili ya mbegu” alisema Dkt. Chilongani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini,  Marco Mtunga  amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Meatu na Kamati yote ya Ulinzi na Usalama isimamie operesheni ya kuondoa maotea kwenye mashamba ya pamba iliyokuwa imesitishwa ili kulinda ubora wa mbegu na mfumo wa kuzalisha mbegu za pamba.

“Tulikuwa tunaendesha operesheni ya kuhakikisha mashamba yote ya kuzalisha mbegu hapa Mwabusalu yanazingatia taratibu za kuzalisha mbegu, ilisitishwa kutokana na vitisho vya wana Mwabusalu kutaka kuwapiga waliokuwa wakipita kwenye mashamba kuondoa maotea, Mhe. DC kuanzia kesho Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya isimamie zoezi hili ili tusipoteze mfumo wa kuzalisha mbegu bora” alisema Mtunga”

Baadhi ya wakulima wa pamba katika Kata ya Mwabusalu wameiomba Serikali kuendelea kuwapata pembejeo kwa wakati na kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuwaongoza katika kuzingatia kanuni za kilimo bora badala ya kuwapotosha  ili waweze kulima kwa tija na kutoka kwenye umaskini.

“Ninaomba Serikali iendelee kutoa madawa na mbolea kwa wakati ili tuweze kuzalisha kwa tija maana mwaka huu tumeongeza uzalishaji na tunatarajia mavuno mengi kwa kuwa pamba haijashambuliwa sana na wadudu kama mwaka jana” alisema Charles Thomas mkulima Mwabusalu

“Baadhi ya viongozi wa kisiasa waache kuhubiri habari mbaya kwenye kilimo cha pamba  maana hawahubiri suala la kufuata sheria, mfano wanapotuambia tuchanganye pamba na mazao mengine wakati wataalam wanasema haitakiwi je wanatusaidia kutoka kwenye umaskini au wanataka tuendelee kuwa maskini” alisema Bupolo Mahangi

Akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa kwenye mkutano huo Naibu Waziri Mgumba amewataka baadhi ya wanasiasa kuwa sehemu ya kutoa elimu na kuwaongoza wakulima hao kuzingatia kanuni za kilimo bora ili waweze kulima kwa tija, kuzalisha mbegu bora na kuongeza mavuno.

Naibu Mgumba jana amemaliza ziara yake  ya kikazi ya siku mbili mkoani Simiyu kwa kutembelea  mradi wa kilimo cha umwagiliaji, kutembelea mashamba ya pamba na kuzungumza na wananchi wilayani Maswa, akiwa wilaya Meatu alitembelea shamba la kuzalisha mbegu za pamba na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo la Mwabusalu lililopo wilayani hapo.
MWISHO

Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba akitembelea moja ya shamba la mfano la pamba katika Kata ya Mwabusalu Wilayani Meatu, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi Machi 07, 2019  wilayani humo
 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga akitoa maelezo juu ya namna pamba inavyopaswa kuhudumiwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba Machi 07, 2019  katika Kata ya Mwabusalu Wilayani Meatu.
Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mwabusalu wilayani Meatu, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi Machi 07, 2019  wilayani humo.
 Sehemu ya shamba la pamba la mfano lililopo katika Kijiji cha Mwabusalu kata ya Mwabusalu wilayani Meatu Mkoani Simiyu.




0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!