Wananchi
mkoani Simiyu kwa mara ya kwanza wameshuhudia Tamasha la Pasaka na kuomba Mwandaaji
wa Matamasha ya Nyimbo za Injili kuendeleza utaratibu huu wa kufanya matamasha
wakati wa sikukuu katika mikoa mbalimbali hususani Mkoa wa Simiyu.
Ombi
hilo la wakazi wa Simiyu limetolewa wakati wa Tamasha la Pasaka mkoani humo lililofanyika leo katika Uwanja wa
Halmashauri Mjini Bariadi na kuhudhuriwa
na mamia ya wananchi kutoka maeneo tofauti mkoani humo.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wananchi hao wamemshukuru Mwandaaji ya Tamasha hilo Mkurugenzi
wa Msama Promotion Ndg.Alex Msama pamoja na viongozi wa Serikali Mkoani Simiyu
kuona umuhimu wa kuandaa Tamasha hilo kwa kuwa nyimbo za injili zinazoimbwa na
waimbaji mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa zinawafanya watu wasifu na kumwabudu
Mungu na kuachana na mambo yasiyofaa.
“Tumelipokea
kwa furaha sana tamasha hili na tunaomba leo isiwe mwisho kila mwaka liwepo;
yaani kwetu ni kama zawadi maana tangu mkoa wetu uanze ni mara ya kwanza, hii ni
dalili kuwa Mkoa wetu unatambulika na unapendwa,tunawashukuru viongozi wetu na
tunamshukuru Msama kutuletea Tamasha la Pasaka” alisema Lilian Kagirwa mkazi wa
Bariadi Mjini.
Naye,
Daniford William mkazi wa Bariadi amesema wigo wa matamasha hayo utanuliwe na
kuwawezesha wananchi katika mikoa yote nchini kupata ujumbe wa Neno la Mungu
kupitia nyimbo za Injili katika nyakati tofauti kwa mwaka.
Mkuu
wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amesema Msama Promotion afanye utaratibu wa kuandaa tamasha lingine
kubwa mkoani Simiyu kwa kuwa wananchi hao wanampenda Mungu na wako tayari kumtukuza
Mungu kupitia matamasha kama hayo.
“
Nichukue nafasi hii kuwakaribisha Msama Promotion na waimbaji wote wa nyimbo za
injili mkoani Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, huu ni mkoa mpya lakini ni mkoa
wenye kasi kubwa ya maendeleo na niombe wakati mwingine mtuletee tamasha kama
hili siku ya Sikukuu ya Krismasi au
Pasaka ili watu wengi wapate nafasi ya kumtukuza Mungu kuzidi ilivyokuwa leo ”. alisema Kiswaga.
Aidha
,Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza wananchi kuendelea kuliombea Taifa na viongozi
wote ili kudumisha amani, upendo na mshikamano wa nchi.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Msama Promotion, Bwana Charles Mwakipesile amewashukuru
na kuwapongeza wananchi wa Bariadi kwa mapokezi mazuri na akaahidi kuwa Kampuni
hiyo itakuza vipaji vya baadhi ya waimbaji wa nyimbo za Injili walionekana kuwa
na uwezo mzuri kufanya vizuri katika medani ya muziki wa injili.
Tamasha
la Pasaka Mkoani Simiyu limehudhuriwa na Waimbaji wa Kitaifa na Kimataifa wakiwemo
Upendo Nkone,Beatrice Mwaipaja,Upendo Kilahiro, Martha Mwaipaja, Jesca Honore,
Sifael Mwabuka na kwaya mbalimbali
kutoka katika Makanisa ya Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment