Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb) amewataka
wakazi wa Lamadi wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, kurasimisha makazi yao katika
kipindi hiki ambacho zoezi la urasimishaji makazi kwa gharama nafuu linaendelea
wilayani humo.
Waziri
Lukuvi ametoa wito huo leo wakati wa zoezi la kuhamasisha urasimishaji makazi yalioendelezwa
kiholela na kukabidhi hati miliki 122 kwa wananchi wenye maeneo yaliyorasimishwa katika
Kijiji cha Lamadi.
Lukuvi
amesema Lamadi ni Mji wa Kibiashara hivyo
wakazi wake wanapaswa kujenga nyumba zao katika maeneo yaliyopimwa na kutolewa
hati ili waishi katika makazi rasmi na salama.
“Mhe.Rais
mpendwa wenu ametuagiza kuja Lamadi kurasimisha makazi yaliyokuwa holela ili
yawe makazi salama na rasmi, huu ni upendeleo maalum ametoa kwamba waliojenga
katika maeneo haya yanayoitwa makazi holela wengi ni maskini na siyo makosa
yao, inawezekana wakati wanajenga hakukukwa na viwanja vilivyopangwa na kupimwa
na Serikali” alisema
“Mhe.Rais
ameagiza watu wote wanaotaka kushiriki zoezi hili wachangamkie fursa hii,
ametoa ofa kuwa ninyi ambao mlijenga siku nyingi na mnataka kuongeza thamani ya
nyumba zenu mtoke kwenye mtaji mfu na kufanya majengo yenu yatumike kama mtaji
wa maendeleo” alisisitiza.
Lukuvi
amesema wananchi watakaporasimisha maeneo yao watapata fursa ya kutumia hati
miliki zao kupata dhamana ya mikopo katika benki mbalimbali kwa ajili ya
kujiendeleza kiuchumi.
Aidha,
amesema ofa hii ya kurasimisha maeneo ni ya muda tu, hivyo akawataka wakazi zaidi ya 5000
waliopimiwa viwanja vyao kulipia kabla ya tarehe 30 Juni 2017 ili waweze kupewa
hati miliki za maeneo yao na ambao bado hawajapimiwa waone umuhimu wa kupima na
kulipia viwanja vyao pia kabla ya muda huo.
Amesema
wananchi wanapaswa kusaidiana na Uongozi
wa Wilaya ya Busega katika kufanikisha zoezi
la urasimishaji kwa kuchangia gharama kidogo ili wapimiwe, warasimishiwe,
wawekewe alama za mipaka, wapewe ramani na kupewa hatimiliki za maeneo yao na
akawataka pia kurasimisha maeneo ya mashamba
na kuyatafutia hati.
Wakati
huo huo Mhe.Lukuvi amewataka wananchi wote waliopata hati na wale watakaendelea
kupewa kulipa kodi ya ardhi ya kila mwaka kwa Serikali na wale watakaokaidi kulipa
kodi hiyo hati zao zitafutwa.
Akizungumza
baada ya kupokea hati kutoka kwa Waziri Lukuvi, Mzee Musa Metusela Kole mkazi
wa Lamadi, ameishukuru Serikali kwa kurasimisha maeneo yao kwa gharama nafuu na
huduma nzuri kutoka kwa wataalam ambao waliwafuata wananchi katika maeneo yao na
akatoa wito kwa wananchi wengine kurasimisha maeneo yao ya makazi na mashamba
pia.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Ndg.Anderson Njiginya amesema
zoezi la urasimishaji ardhi kwa wakazi wa Lamadi limechangia kuongeza mapato yatokanayo
na ardhi kwa Serikali, kupunguza migogoro ya ardhi baada ya kupima na kuweka mipaka
ya kudumu katika viwanja na kuwawezesha wananchi kutumia hati za maeneo yao kwa
shughuli zao za kiuchumi.
Zoezi
la urasimishaji wa makazi katika Kituo cha Kibiashara Lamadi lilianza Mwezi
Julai 2016 hadi sasa ambapo shughuli ya utambuzi wa miliki umekamilika kwa
kupata viwanja 5223 na shughuli ya umilikishaji
Viwanja ilianza Aprili 11, 2017 ambapo hadi sasa hati 138 zimeandaliwa kati ya
hizo 122 zimekabidhiwa leo kwa wamiliki na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb).
0 comments:
Post a Comment