Thursday, April 27, 2017

RC MTAKA APONGEZA JESHI LA POLISI KUPUNGUZA MATUKIO YA UHALIFU

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka  amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoani humo kwa kupunguza matukio ya uhalifu hali iliyobadili taswira ya mkoa na kuufanya usikike katika masuala  maendeleo.

Mtaka ametoa pongezi hizo katika kikao chake na Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani humo kilichofanyika leo  Mjini Bariadi.

Amesema askari wa Jeshi la Polisi wamefanya kazi kubwa katika kubadili taswira ya mkoa wa Simiyu ambapo kwa sasa viongozi na wananchi wamekuwa wakijadili masuala ya maendeleo ukiwemo Uchumi wa Viwanda kwa sababu ya amani na utulivu uliopo.

“Simiyu ya zamani ni tofauti kabisa na ya sasa,  zamani tulikuwa tukiangalia TV, tukisikiliza redio au kusoma magazeti habari zilikuwa ni mauaji ya vikongwe, kukatana mapanga na mauaji ya watu wenye ualbino.  Pamoja na viongozi wa Dini kuomba Mungu kwa ajili ya mkoa wetu lakini Jeshi la polisi pia limefanya kazi kwa nafasi yake pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama ” alisema Mtaka.

 Aidha, amesema Serikali imedhamiria kuujenga Mkoa wa Simiyu kuwa Mkoa mpya wa kiuchumi jambo ambalo linapaswa kujulikana na wadau wote muhimu wa maendeleo wakiwemo viongozi na askari wa Jeshi la Polisi ambao aliwataka kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji na maendeleo mkoani humo.

“ Chini ya Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa Moja, Sasa hivi Maswa wanatengeneza chaki, Meatu wanasindika Maziwa na tunapanua kiwanda cha maziwa kwa kufanya uwekezaji mkubwa ambapo pia tutatengeneza maziwa ya unga kwa ajili ya watoto, tutaanza kilimo cha umwagiliaji Busega pamoja na kuanzisha kiwanda cha kutengeneza Tomato sauce; hapa kila wilaya ina jambo la kufanya, hizi zote ni fursa  ninyi askari na viongozi changamkieni fursa zilizopo” alisisitiza.

Ameongeza kuwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, Mkoa wa Simiyu unatarajia kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa asilimia 40%  kwa kuwa vitaanzishwa viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali yanayopatikana hapa nchini katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Wakati huo huo Mtaka amewataka askari wa jeshi la polisi kutekeleza majukumu kwa kuzingatia maadili ya kazi yao ikiwa ni pamoja na kupima nguvu ya kutumia kukabiliana na raia katika matukio mbalimbali na kuepuka fedheha ya kuwa watoa taarifa kwa wahalifu.

Vile vile amewataka askari wote kuwa waangalifu katika lugha wanayotumia wakati wakiwa wanatekeleza majukumu yao.

Wakati akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mkoa kwa nasaha mbalimbali alizotoa kwa Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mshongi amewataka viongozi na askari kufanya kazi zao kwa weledi huku wakizingatia maadili yao.

Katika kikao hicho viongozi na askari wa Jeshi la Polisi wamewasilisha maoni, mapendekezo na maombi mbalimbali kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ikiwa ni pamoja na kuomba Mamlaka za Serikali za Mitaa kupima na kuwauzia viwanja kwa bei nafuu ili wajenge na kuendeleza Mkoa huo.
Baadhi ya Askari Polisi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika  kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mshongi akizungumza katika kikao cha Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi.
 Baadhi ya Viongozi wa Jeshi la Polisi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi. 
Baadhi ya Askari Polisi wakiimba Wimbo wa Maadili mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) kabla ya kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa Jeshi la Polisi wakiimba wimbo wa Maadili ya Polisi mbele ya  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) kabla ya kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Stafu Jonas Mahanga Mmoja wa Viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani Simiyu akichangia jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo na Viongozi na Askari Polisi kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
WP Anna akichangia jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo na Viongozi na Askari Polisi kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Viongozi wa Jeshi la Polisi wa Mkoa huo ( baadhi hawapo pichani) kabla ya kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
PC Simon kutoka Wilayani Busega  akichangia jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo na Viongozi na Askari Polisi kilichofanyika leo Mjini Bariadi.0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!