Serikali mkoani Simiyu imeomba kuwepo kwa kikundi
cha ulinzi cha kijeshi katika Wilaya ya Busega ili kusaidia mapambano dhidi ya
vitendo vya uhalifu ikiwemo uvuvi haramu na kuwezesha ufugaji wa samaki ndani
ya Ziwa Victoria kufanyika kwa usalama.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati wa Hafla ya
kumpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini, Jenerali Venance Mabeyo iliyoandaliwa
na ndugu zake kijijini kwao Yitimwila ‘A’
katika Kata ya Kiloleri Wilayani Busega.
“Tumepata changamoto nyingi sana kwenye ziwa,
matukio mengi ya kihalifu liliwemo la uvuvi haramu , sisi kama mkoa tulikuja na
wazo kwamba tungehitaji tupate ‘detouch’ moja eneo la Ziwa ili ukanda huu baada
ya kufanya kazi kubwa ya kuchoma makokoro ya wananchi, tuwapeleke kwenye uvuvi
wa kisasa hususani ufugaji wa samaki ziwani, jambo ambalo Mheshimiwa Rais analipa
kipaumbele sana; na namna pekee ya
kufanya ufugaji ule wa samaki ziwani, suala la ulinzi na usalama ni muhimu
sana; ” alisema Mtaka.
Aidha,
Mtaka amesema pamoja na kufanya ufugaji wa samaki katika Ziwa Victoria, Serikali ya Mkoa
imefanya makubaliano na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF kuwawezesha wananchi wa
Busega kufanya kilimo cha Umwagiliaji kwa kutumia maji ya ziwa hilo ambayo ni
ya uhakika.
“Tumeongea
na NSSF kwa ajili ya kuanzisha mradi ambao hautazidi bilioni moja, tutaleta mbegu za aina ya
nyanya na pilipili zinazotakiwa ili wananchi wa Busega wazalishe kwa wingi.
Hatutakuwa tayari kuona wananchi wanalima
nyanya na kuuza ndoo moja shilingi 500,
tumepanga kuanzisha mradi wa
kuzalisha ‘chill sauce’ na ‘tomato source’ .”alisema Mtaka.
Ameongeza
kuwa Wataalam wa Wilaya na Mkoa kwa kushirikiana na Wataalam wa Wizara ya Maji
na Umwagiliaji , Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru wanafanya upembuzi
yakinifu kuona namna miundombinu ya umwagiliaji itakavyojengwa ili kuwawezesha
wananchi wa Busega kulima muda wote kupitia kilimo cha Umwagiliaji badala ya
kutegemea mvua.
Mtaka
amesema Serikali mkoani Simiyu imedhamiria kuhakikisha katika kipindi cha miaka
mitatu ijayo Mkoa hauingizi bidhaa kutoka mikoa mingine na badala yake wananchi
wake watazalisha na kutumia bidhaa zao wenyewe, hivyo ameomba Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) kuona namna ya kuweka vituo vya kuuza zana za kilimo katika maeneo
ya kanda ya Ziwa ili wananchi wapate zana bora za kisasa zitakazowasaidia
kulima kisasa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini, Jenerali Venance Mabeyo
amewataka wananchi wa Busega kubadili mtazamo wao na kutumia maji ya ziwa
Victoria kwa manufaa yao kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili wasikumbwe na
tatizo la upungufu wa chakula kunapotokea ukame.
Kuhusu
suala la ulinzi katika Ziwa Victoria amesema ombi la Serikali ya Mkoa la kuwa na kikundi cha
Ulinzi, viongozi watalitafakari kuona
namna ya kulishughulikia na akaeleza kuwa tayari Jeshi limeweka kikundi kidogo
cha kiulinzi kutoka Jeshi la wanamaji, lakini
kutokana na ukubwa wa Ziwa Victoria kikundi hicho hakiwezi kuhimili kufanya
doria maeneo yote na akaahidi kukiimarisha zaidi.
Jenerali
Mabeyo pia amewaasa vijana wa Busega na mkoa wa Simiyu kwa ujumla kujiunga katika
vikundi ili Serikali iwasaidie kutafuta mitaji ya kujishughulisha na Kilimo,
uvuvi na ufugaji badala ya kukimbilia JKT tu, japo amesema kwenda kwao JKT kunaweza
kuwasaidia kupata stadi mbalimbali za maisha.
Naye
Mwakilishi wa Baraza la Wazee wa Wilaya ya Busega, Bibi. Perazia Ndaki akisoma
risala ya wazee kwa Mkuu wa majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo amemuomba
Mkuu huyo wa majeshi kuona uwezekano wa kuanzisha Kambi ya jeshi la Kujenga
Taifa(JKT) katika mikoa ya kanda ya Ziwa na hususani Mkoa wa Simiyu ili
kuwasaidia vijana wengi kujiunga na kupata stadi mbalimbali zitakazowasaidia
kujiajiri katika uvuvi, kilimo na ufugaji.
Mbunge
wa Jimbo la Busega, Mhe.Raphael Chegeni amemuhakikishia Mkuu huyo wa majeshi
kuwa endapo ombi la kuanzisha kambi katika Mkoa wa Simiyu litaridhiwa, Wilaya
ya Busega itatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kambi hiyo ambalo lipo tayari.
Sanjali
na hilo viongozi mbalimbali wa dini walioshiriki katika hafla ya kumpongeza
Mkuu huyo wa Majeshi, wamesisitiza wananchi kuwaombea yeye pamoja na viongozi wote
wa Serikali wa ngazi zote ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika
kuwatumikia wananchi.
0 comments:
Post a Comment