Thursday, April 19, 2018

RC MTAKA: WALIMU WA KIKE WASAIDIENI WANAFUNZI WA KIKE KUPATA ELIMU YA KUJITAMBUA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa  wito kwa walimu wote wa kike mkoani humo kuwasaidia wanafunzi wa kike katika elimu ya kujitambua ili iwasaidie kuepukana na vishawishi vinavyoweza kupekelekea mimba za utotoni.

Mtaka ameyasema hayo jana katika Kongamano la Elimu ya Masuala ya Jinsia kwa Walimu na Wanafunzi wa Kike wa baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Makao Makuu, kilichofanyika katika Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial Mjini Bariadi.

Amesema si masuala yote ya yanayohusu maisha yamewekwa katika mitaala, hivyo walimu wanapaswa kusimama katika nafasi zao kama wazazi ili kile wanachotamani kuwafundisha watoto wao au ndugu zao kwa lengo la kuwalinda na tabia zisizofaa, wakifanye pia kwa wanafunzi wao wa kike ili wawasaidie wasiharibike.

Ameongeza kuwa Viongozi  na Watendaji mbalimbali wa Serikali Mkoani humo wanatamani wanafunzi wote wa kike wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza wamalize masomo na kufikia ndoto zao pasipo vikwazo vyovyote ikiwemo mimba za utotoni.

“Tungehitaji kuona wanafunzi wa kike wa mkoa wetu wanajitambua, tusingehitaji kuwa na wanafunzi wa kike wanaopata mimba wakakatisha masomo yao na ndoto zao, natamani watoto wa kike wa Simiyu suala la elimu liwe Kipaumbele chao cha kwanza” alisema Mtaka

“Msaada wa kwanza wa watoto wetu wa kike ni walimu wetu wa kike, mwalimu anayewasimamia vizuri watoto wa kike  na kuwasaidia wasiharibike hata watoto wake nyumbani hawawezi kuharibika, ‘uki-ignore’ (ukipuuza) kwamba mwanafunzi hakuhusu kesho utakuta mwanao ndiye anayeharibikiwa” alisisitiza.


Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amesema ipo haja na hoja kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike kwa shule zote za Sekondari za Kata ili watoto wa kike wasipange wala kutembea mwendo mrefu. 

Kwa upande wake Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Mary Mrio amesema walimu wa kike wakiwasaidia na kuwa marafiki kwa watoto wa kike ni rahisi watoto kuwaeleza matatizo yanayowakabili na akawataka wanafunzi kuwa wawazi kwa walimu wao wa kike ili wasaidiwe.

Naye Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la AMREF kupitia Mradi wa UZAZI UZIMA ametoa wito kwa watoto wa kike mkoani Simiyu kutokubali kutumiwa kama mitaji na wazazi wao kwa kukatishwa masomo na kuozeshwa mapema,  ili kukabiliana na  changamoto ya mimba za utotoni  katika kufikia ndoto zao.

Katika hatua nyingine wanafunzi wa kike wameiomba Serikali kuona namna ya kuwashirikisha wazazi na walezi wao katika makongamano ambayo yanatumika kutoa elimu ya masuala ya jinsia ili nao wawe na uelewa juu ya masuala hayo na kujua namna ya kuwasaidia watoto wao.

“Kwenye makongamano kama haya ingekuwa vizuri tukiwahusisha baadhi ya wazazi ili nao wapate elimu kama hii tunayopata sisi, maana sisi watoto wa kike kuna wakati unaweza  ukawa unaumwa  ila ukimweleza mzazi anasema hutaki kufanya kazi” Florencia Ndakama mwanafunzi wa Kidato cha Tatu Shule ya Sekondari Bariadi

Akitoa taarifa juu ya ushiriki wa wanafunzi na walimu wa kike katika kongamano hilo, Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory amesema jumla ya walimu 228 na wanafunzi 1506 kutoka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mjini Bariadi wameshiriki.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na walimu na wanafunzi wa kike kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Mjini Bariadi katika Kongamano la Elimu ya Masuala ya Jinsia lililofanyika jana katika Shule ya Sekondari ya  Kusekwa Memorial Mjini Bariadi.
Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari kidinda akichangia jambo katika Kongamano la Elimu ya Masuala ya Kijinsia kwa walimu na wanafunzi wa kike kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Mjini Bariadi, lililofanyika jana katika Shule ya Sekondari ya  Kusekwa Memorial Mjini Bariadi, (kulia) Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia kutoka shirika lisilo la Kiserikali la AMREF.
Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari kidinda akichangia jambo katika Kongamano la Elimu ya Masuala ya Jinsia kwa walimu na wanafunzi wa kike kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Mjini Bariadi, lililofanyika jana katika Shule ya Sekondari ya  Kusekwa Memorial Mjini Bariadi.
Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Nipashe, Bibi.Happy Severine akitoa mada katika Kongamano la Elimu ya Masuala ya Jinsia kwa walimu na wanafunzi wa kike kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Mjini Bariadi, lililofanyika jana katika Shule ya Sekondari ya  Kusekwa Memorial Mjini Bariadi

Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Mary Mrio akitoa mada katika Kongamano la Elimu ya Masuala ya Jinsia kwa walimu na wanafunzi wa kike kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Mjini Bariadi, lililofanyika jana katika Shule ya Sekondari ya  Kusekwa Memorial Mjini Bariadi.

Afisa Vijana wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Bibi.Zena Mchujuko akitoa mada katika Kongamano la Elimu ya Masuala ya Jinsia kwa walimu na wanafunzi wa kike kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Mjini Bariadi, lililofanyika jana katika Shule ya Sekondari ya  Kusekwa Memorial Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!