Sunday, April 8, 2018

WADAU WATOA MSAADA WA FEDHA , CHAKULA KUWEZESHA KAMBI YA KITAALUMA KWA WANAFUNZI KIDATO CHA SITA SIMIYU


Wadau mbalimbali wa maendeleo wa Mkoa wa Simiyu wametoa shilingi Milioni 10 na Kilo 1200 za mchele, mafuta ya kula, sabuni , sukari na mahitaji mengine kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi wa kidato cha Sita walioweka Kambi ya kitaaluma wilayani Maswa kwa ajili ya kujiandaa na Mtihani wa Taifa utakaofanyika mwezi Mei.

Akizungumza wakati wa makabidhiano katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataja wadau hao kuwa ni Ofisi yake iliyotoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuongezea posho ya walimu mahiri 40 wanaowafundisha wanafunzi hao pamoja na kununua mahitaji maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike.

Amesema wadau wengine ni Mbunge wa Itilima Mhe.Njalu Silanga aliyetoa kilo 500 za mchele, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kilo 300, Mkurugenzi wa Itilima kilo 100 za mchele, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi kilo 100 za mchele, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi kilo 100 za mchele na Mkurugenzi Busega kilo 100 za mchele.

Aidha, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imeahidi kuchangia ng’ombe wawili na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu imeahidi kuchangia kilo 100 za mchele.

Mtaka amewashukuru wadau wote walioguswa kuwachangia wanafunzi hao wa kidato cha sita  na akatoa wito kwa wazazi, viongozi na watu kutoka makundi mbalimbali kujitokeza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Idara ya Elimu katika kuwasaidia wanafunzi hao, ili waweze kujiandaa na kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa mwezi Mei.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa mwaka huu mkoa wetu unaingia kwenye mikoa itakayofanya vizuri zaidi Kitaifa, niendelee kuwaomba wanafunzi mliopo hapa mzingatie masomo siku 10 mtakazokaa hapa ziwe na manufaa kwenu na ninyi walimu 40 wafundisheni watoto kwa vipaji vyote mlivyojaliwa na Mwenyezi Mungu ili wafanye vizuri kwenye mtihani wao wa mwisho” alisema Mtaka.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya kambi hiyo ya kitaaluma kumalizika ndani ya hizo siku10 ufanyike mtihani ili kuwapima wanafunzi na akaahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni tano kwa walimu wataotunga maswali yatakayofanana na yale yatakayokuwepo katika Mtihani wa Taifa kwenye masomo yao.

Akizungumza kwa niaba ya walimu mahiri 40 wanaowafundisha wanafunzi kambini hapo Mwalimu Makame S. Makame kutoka Shule ya Sekondari Bariadi,  amesema kwa namna walivyojitolea kuwafundisha wanafunzi hao wana imani kubwa kuwa mwaka 2018 utakuwa mwaka matokeo mazuri(Kidato cha Sita)  ya kihistoria kwa Mkoa wa Simiyu.

Mwanafunzi Martina Simba kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na wadau wengine wote kwa misaada waliyoitoa na kusisitiza kuwa, kukaa kwao kambini hapo siku kumi hakutakuwa bure bali ni mwanzo mzuri wa safari yao ya mafanikio ya kuwafikisha katika mikoa itakayofanya vizuri zaidi katika Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2018.

 Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu ilifunguliwa rasmi Aprili 3 ikiwa na jumla ya wanafunzi1003 kutoka shule 11 na walimu mahiri 40 kwa ajili ya kuwafundisha na inatarajiwa kufungwa Aprili 13, 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka katika Shule 11 mkoani humo walioweka kambi ya kitaaluma kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Mwezi Mei, mara baada ya kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali vilivyotolewa na wadau kwa ajili ya wanafunzi hao.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony akikata utepe kabla ya kakabidhi msaada wa vitu mbalimbali viliyotolewa na wadau kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka katika Shule 11 mkoani humo, walioweka kambi ya kitaaluma kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Mwezi Mei 2018. 
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory akizungumza na wanafunzi  wa Kidato cha Sita kutoka katika Shule 11 mkoani humo walioweka kambi ya kitaaluma kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Mwezi Mei mwaka huu.
Baadhi ya Walimu Mahiri wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka katika Shule 11 mkoani humo walioweka kambi ya kitaaluma kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Mwezi Mei mwaka huu.
Mwanafunzi Martina Simba kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa akitoa shukrani kwa Viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa msaada wa chakula na mahitaji mengine uliotolewa kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka katika Shule 11 mkoani humo walioweka kambi ya kitaaluma,kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Mwezi Mei mwaka huu.
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa wa Simiyu walioweka kambi ya kitaaluma kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Mwezi Mei mwaka huu,  wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati alipokuwa akizungumza nao leo katika Ukumbi wa Shule ya Wasichana Maswa wilayani Maswa.
Majaliwa Chibona mmoja wa walimu 40 mahiri wanaowafundisha wanafunzi wa kidato cha sita kutokashule 11 mkoani Simiyu, ambao wameweka kambi ya Kitaaluma kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika mwezi Mei 2018, akitoa shukrani kwa viongozi waliotoa misaada mbalimbali kwa wanafunzi na walimu ili kuwezesha kambi hiyo kufanikiwa.
Baadhi ya wanafunzi wasichana wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 mkoani Simiyu wakifurahia jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe(mwenye miwani) mara baada ya kukabidhiwa msaada wa chakula na mahitaji mbalimbali.


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!