Friday, April 13, 2018

WANAFUNZI 7361 KIDATO CHA NNE SIMIYU KUWEKA KAMBI YA KITAALUMA MWEZI JUNI


Wanafunzi 7,361 wa kidato cha nne kutoka katika shule za sekondari Mkoani SIMIYU wanatarajia kuweka kambi maalum ya kitaaluma ili kujiandaa na Mtihani wa Taifa na kuweza kuinua kiwango cha ufaulu mkoani humo.

 Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipokuwa akifunga Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi 1005 wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 Mkoani humo, waliokuwa chini ya Wakuu wa Shule 11 na walimu mahiri 40, wilayani Maswa.  

Lengo la kambi hii lilikuwa ni kutekeleza sehemu ya mkakati wa Mkoa huo wa kufuta daraja la nne na sifuri kwa kuwaandaa wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani humo na Mtihani wa Taifa unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Mei.

Mtaka anasema baada ya kumalizika kambi hiyo ni matumaini ya Mkoa wa Simiyu kuona wanafunzi wanafaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na kufuta sifuri huku akitangaza kuanza kwa kambi ya wanafunzi wa kidato cha nne.

“Tumemaliza kambi ya Kidato cha Sita, natangaza rasmi leo kuwa tutakuwa na  Kambi ya Kidato cha Nne na Darasa la Saba mwezi Juni Mwaka huu, wanafunzi 7361 wa kidato cha nne watakaa kwenye kambi siku 21, kila wilaya itakaa na wanafunzi wake na mimi kama Mkuu wa Mkoa nitayafungua makambi hayo” alisema

“Baada ya kambi hiyo tutachukua wanafunzi bora watano katika kila shule baada ya mtihani wa Mkoa kufanyika ambao watatengeneza kambi kiwilaya pia,  ili tuchakate na kupata wanafunzi bora watakaotengeneza daraja la kwanza kwenye mkoa” alisisitiza

Aidha, Mtaka amesema anashauriana na Maafisa Elimu kuona uwezekano wa  kutengeneza kambi kwa ajili ya wanafunzi 10 ambao wanafanya vibaya kwa kila shule ili waweze kusaidiwa  na baaaye Mkoa uweze kuondokana kabisa na sifuri.

Ameongeza kuwa pia mwezi Juni wanafunzi 36,156 wa darasa la saba wataweka kambi na kambi zote mbili zitafunguliwa kwa pamoja, hivyo akatoa taarifa kuwa wadau wote wa elimu na watu wenye mapenzi mema watakapoombwa kuchangia ili kuwezesha kambi hizo wakubali kuunga mkono suala hilo.

Afisa Elimu wa Mkoa wa SIMIYU, Julius Nestory ameahidi kuwa kufikia mwaka 2020 kutakuwa na Mapinduzi makubwa ya Sekta ya Elimu katika Mkoa huo.

Wanafunzi wa kidato cha sita waliomaliza kambi iliyochukua takribani siku kumi wamesema kukutanishwa pamoja kumewasaidia hasa kwenye mada na maswali yalikuwa yanawasumbua, hivyo kwa sasa wamejiandaa vizuri na watafanya  vizuri katika Mtihani wao wa mwisho.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa SIMIYU amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itatoa Shilingi Milioni Mbili kwa mwanafunzi atakayeingia katika kumi bora Kitaifa, Shilingi Milioni Tano kwa shule itakayokuwa miongoni mwa shule kumi bora na mwalimu mahiri atakayewezesha Alama A atapata Shilingi Laki mbili.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 Mkoani humo wakati wa kufunga  Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao 1005 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 Mkoan humo wakati wa kufunga  Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao 1005 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 Mkoani humo wakati wa kufunga  Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao 1005 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa.
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoa Shule 11 Mkoani Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka katika zoezi la kufunga Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao 1005 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baaadhi ya viongozi wa Chama na Serikali, Maafisa Elimu na wanafunzi baada ya   kufunga  Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita 1005 Mkoani humo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baaadhi ya viongozi wa Chama na Serikali, Wakuu wa Shule na wanafunzi baada ya   kufunga  Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita 1005 Mkoani humo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baaadhi ya viongozi wa Chama na Serikali, Walimu mahiri na wanafunzi baada ya   kufunga  Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita 1005 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!