Saturday, May 26, 2018

RC MTAKA:TUTAWALINDA NA KUWATUNZA WANAFUNZI KIDATO CHA NNE, DARASA LA SABA WATAKAOKAA KAMBI ZA KITAALUMA MWEZI JUNI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe.Anthony Mtaka amewahakikishia wazazi wote mkoani humo kuwa Serikali itawalinda na kuwatunza watoto wote kwa muda wa siku zote watakaokuwa katika Kambi za Kitaaluma kwa Kidato cha Nne na Darasa la Saba, ambazo zinazotarajiwa kuanza rasmi mapema mwezi Juni mwaka huu kwa mkoa mzima.


Mtaka ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wenyeviti wa Kamati na Bodi za Shule katika Shule ya Msingi Mshikamano Wilayani Meatu katika kikao maalum kilicholenga  kujadiliana juu ya maandalizi ya Kambi hizo Wilayani humo.

Amesema Serikali imebeba dhamana ya  kuwaweka wanafunzi kambini kwa lengo la kuwaandaa vema ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na kuongeza ufaulu, hivyo haitawafumbia macho wale wote watakaoonekana kwa njia moja ama nyingine kuharibu jitihada hizo.

“Nawaambia hapa wananchi wa Meatu, kambi za wanafunzi wetu za kitaaluma mziogope kama ukoma, sisi hatuwezi kubeba dhamana ya watoto wa watu kwenda kwenye makambi halafu aje mtu anajipitisha pitisha kwenye kambi kufuatilia na kutaka kuwarubuni watoto wetu wa kike, nawaeleza hapa mtakuwa halali ya polisi” alisema Mtaka.

Ameongeza kuwa wakati wote wanafunzi watakapokuwa kambini Serikali itawawezesha walimu kupata stahili zao kutekeleza majukumu yao na kwa kushirikiana na wadau wengine itatoa mahitaji maalum kwa wanafunzi wa kike, hivyo akawataka wazazi kujiandaa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao ambacho ni sehemu ya kile ambacho kingetumika wakiwa nao nyumbani.

Aidha, Mtaka amewataka wazazi, walimu kushikamana na Serikali katika kufikia azma ya kufanya mapinduzi ya Elimu mkoani Simiyu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake badala ya kuwatupia lawama walimu pekee kila wanafunzi wanapofanya vibaya katika mitihani yao, kwa kuwa ufaulu wa mwanafunzi unategemea  ushirikiano katika ya walimu, wazazi na wanafunzi.

Kwa upande wao Wenyeviti wa Bodi na Kamati za Shule wamepongeza kuwepo kwa kambi hizo za Kitaaluma na wakakiri kuwa kambi hizo zinaweza kuwa suluhu ya kuondokana na daraja la nne na sifuri kwa kidato cha nne na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba na wakatoa maoni yao.

“ Binafsi nampongeza Mkuu wa mkoa kwa kuja na wazo hili la kufanya makambi ya kitaaluma kwenye mkoa wetu, napendekeza kambi hizi zisiishie kwenye hizo siku 21 za mwezi wa sita tu,  wazazi tushikamane tuchange chakula watoto wetu wakae kambi hata mwezi wa tisa” alisema Mchungaji Fabian Kuzenza.

“Naunga mkono kuwepo makambi ya kitaaluma na namsukuru Mkuu wa Mkoa kuzungumza na sisi,  hii imetusaidia kuwa na uelewa wa pamoja naomba pia atusaidie wajumbe wetu wa kamati za shule wapewe mafunzo wawe na uelewa mpana wa masuala mbalimbali, ili wawe wanawaeleza wazazi mambo wanayoyafahamu” Elias Kamweji Mwenyekiti Kamati ya Shule ya Msingi Paji.

Mwezi Juni mwaka huu Wilaya zote mkoani Simiyu zitafungua Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne na Darasa la Saba kwa muda wa siku 21 na katika siku hizo wanafunzi wote watafanya mtihani wa majaribio kwa ajili ya maandalizi ya Mitihani ya Kitaifa iliyo mbele yao
MWISHO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Wenyeviti wa Kamati na  Bodi za Shule za Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) , katika kikao maalum cha maandalizi ya Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na Darasa la Saba zinazotarajiwa kufanyika mwezi Juni kwa siku 21, kilichofanyika Shule ya msingi Mshikamano
Baadhi ya Wenyeviti wa Bodi na Kamati za Shule wa Wilaya ya Meatu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao maalum cha maandalizi ya Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na Darasa la saba zinazotarajiwa kufanyika mwezi Juni kwa siku 21, kilichofanyika Shule ya msingi Mshikamano

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani ( wa kwanza mstari wa mbele)  na viongozi wengine wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka( hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na Wenyeviti wa Kamati na  Bodi za Shule za Wilaya hiyo  (hawapo pichani) , katika kikao maalum cha maandalizi ya Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na Darasa la Saba, kilichofanyika Shule ya msingi Mshikamano.
Mchungaji Fabian Kuzenza akichangia hoja katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na Wenyeviti wa Kamati na  Bodi za Shule za Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) , katika kikao maalum cha maandalizi ya Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na Darasa la Saba zinazotarajiwa kufanyika mwezi Juni kwa siku 21, kilichofanyika Shule ya msingi Mshikamano,
Bi. Minza Sibaba Mjumbe Bodi ya Shule Nyanza akichangia hoja katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na Wenyeviti wa Kamati na  Bodi za Shule za Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) , katika kikao maalum cha maandalizi ya Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na Darasa la Saba zinazotarajiwa kufanyika mwezi Juni kwa siku 21, kilichofanyika Shule ya msingi Mshikamano.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza akifafanua jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na Wenyeviti wa Kamati na  Bodi za Shule za Wilaya hiyo, katika kikao maalum cha maandalizi ya Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na Darasa la Saba zinazotarajiwa kufanyika mwezi Juni kwa siku 21, kilichofanyika Shule ya msingi Mshikamano.
Baadhi ya Wenyeviti wa Bodi na Kamati za Shule wa Wilaya ya Meatu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao maalum cha maandalizi ya Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na Darasa la saba zinazotarajiwa kufanyika mwezi Juni kwa siku 21, kilichofanyika Shule ya msingi Mshikamano.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!