Saturday, April 20, 2019

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AWATAKA KIDATO CHA SITA SIMIYU WASIKUBALI NDOTO ZAO KUKATISHWA


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde ametoa wito kwa wanafunzi wa kidato cha sita Mkoani Simiyu kutokubali mtu yeyote kufifisha wala kukatisha ndoto zao badala yake wasome kwa bidii.

Mavunde ametoa wito huo wakati akizungumza na wanafunzi zaidi ya 1000 kutoka  shule kumi na mbili za sekondari za  kidato cha sita walioko katika kambi ya kitaaluma, shule ya sekondari ya wasichana Maswa.

Mavunde amesema Taifa lolote duniani linajengwa na vijana na hasa vijana wasomi hivyo wanapaswa kusoma kwa bidii, ili wasiwaangushe, wazazi na jamii inayowazunguka  ambayo inawategemea, huku akipongeza uongozi wa mkoa kuanzisha kambi za kitaaluma ambazo zimeoneka kuusaidia mkoa kupanda katika ufaulu.

“wanafunzi msikubali ndoto zenu zikatishwe, someni kwa bidii mfikie ndoto zenu, Taifa wazazi na jamii inayowazunguka inawategemea, msiwaangushe viongozi wenu waliofanya mkawa hapa, Mkoa wa Simiyu ndio umetuonesha kuwa kumbe kambi za kitaaluma zinawezekana” alisema Mhe. Mavunde.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony  Mtaka amewapongeza walimu wote kwa kazi nzuri wanayoifanya  na kueleza  lengo la kuanzishwa kambi za kitaaluma ambazo amesema zimeonekana kuwa na mwamko mkubwa kwa wanafunzi.

“Sisi tulitafakari watoto wetu wanatoka kwenye mazingira ya kawaida tukajiuliza kwa nini wasikae kwenye madarasa yaliyo na sakafu na dari safi wakasoma, tumejaribu kwenye shule za O’level (kidato cha nne) tumeona mwamko wa watoto kusoma” alisema Mhe. Mtaka.

Kwa upande wao viongozi na wadau mbalimbali wa elimu waliowatembelea wanafunzi hao pia walipata nafasi ya kuwausia wanafunzi hao wa kidato cha sita na kuwasisitiza juu ya umuhimu wa kufanya bidii ili kufikia malengo  yao.

“ Tunajadiliana hapa ili kuwa na uelewa wa pamoja, ninataka kuwaambia kuwa hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati mbaya iwe  katika masomo hata katika maisha,” alisema Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisha.

“Mnaweza kutimiza ndoto zenu bila kujali mahali mtu anapotoka, najua wengi wetu hapa tumetoka katika familia za kawaida, tumesoma shule za kawaida kabisa lakini tulifanikiwa, hata ninyi mnaweza ni suala la kuamua tu” alisema Happiness Lugiko Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Naye Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la kusini, Mch. Mark Malekana amesema ili wanafuzi hao waweze kufikia ndoto zao wanapaswa kuwa na dhamira ya kushinda, wasome kwa bidii, wawe na nidhamu, washinde hofu wanapokuwa kwenye mitihani na wamwamini Mungu.

Mwanafunzi Kelista Joseph kutoka shule ya sekondari Itilima amesema maswali mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyafanyia kazi yatawasaidiana mwishowe watafanya vizuri  na wanaamini kama walivyoahidi toka siku ya kwanza ya kambi kwamba watapata ‘Division One’ wote.

Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita mwaka 2019 Mkoani Simiyu inatarajiwa kufungwa rasmi Aprili 28, 2019 na baadaye wanafunzi watarejea katika shule zao kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa unaotarajia kuanza Mei 06, 2019.

MWISHO

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde  akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita walio katika kambi ya Kitaaluma Mkoani Simiyu wakati aliwapowatembelea wanafunzi hao wilayani Maswa, Aprili 19, 2019.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akipokea mchango wa shilingi milioni moja kutoka kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde aliochangia kwa ajili ya kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha sita inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa.
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoani Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde wakati alipowatembelea wanafunzi hao Aprili 19, 2019. katika kambi ya Kitaaluma inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa.
Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza na baadhi ya wanafunzi  wa Kidato cha Sita shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali walipowatembelea wanafunzi  walio katika kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wote wa kidato cha sita Mkoani Simiyu inayoendelea katika shule hiyo.
Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani) wakati viongozi mbalimbali wa Serikali walipowatembelea shuleni hapo.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Happiness Lugiko  akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani)wakati viongozi mbalimbali wa Serikali walipowatembelea shuleni hapo.
Baadhi ya viongozi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waanfunzi wa kidato cha sita mwaka 2019 mkoani Simiyu, walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi hao walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
 Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akimshika ng’ombe aliyetolewa na Mhe. Pili Ndimila Diwani wa Viti maaluma Wilayani Maswa, kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha sita mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Mhe. Anthony Mtaka(wa tatu kushoto) akimtambulisha Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani) wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo.
Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la kusini, Mch. Mark Malekana akiwaombea wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita waliokatika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita waliokatika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Kalista Joseph Mwanafunzi  wa Kidato cha Sita kutoka Shule ya Sekondari Itilima akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Mmoja wa wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka Shule ya Sekondari Simba wa Yuda akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(wa nne kushoto) na vingozi wengine wa dini na wa serikali wakizungumza na baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi hao walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Baadhi ya viongozi na wanafunzi wakishuhudia ng’ombe wawili waliotolewa na wadau wa elimu kwa ajili ya kuchangia kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha sita inayoendelea katika shule y sekondari Maswa.
Baadhi ya viongozi wa dini na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi hao walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.


Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya(mwenye miwani) na  Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakiwa na baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa BRELA, Bw. Bakari Mketu akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani)wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na viongozi wa  dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya akisalimiana na Silya Jasamila(19)binti aliyenusurika kuozeshwa na baba yake mzazi mara baada ya kuhitimu kidato cha nne , ambaye kwa sasa anatunzwa na kulelewa na viongozi wa Serikali katika Shule ya sekondari Maswawakati akisubiri kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wakati balozi huyo alipowatembelea wanafunzi wa kidato cha sita walio katika kambi ya kitaaluma shuleni hapo Aprili 19, 2019

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde(wa pili kushoto) akiteta jambo na   Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati viongozi mbalimbali wa serikali na dini walipowatembelea wanafunzi wa Kidato cha sita mkoani Simiyu(hawapo pichani) Aprili 19, 2019 katika kambi ya Kitaaluma inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka na kulia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Happiness Lugiko.
Kutoka kulia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe na Afisa Elimu Mkoa, Mwl. Ernest Hinju wakifurahia jambo wakati wa ziara ya viongozi mbalimbali katika kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha sita inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichanaMaswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka(mwenye kipaza sauti) akimtambulisha Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la kusini, Mch. Mark Malekana kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakiimba wimbo wa Tanzania Tanzania, wakati viongozi wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!