Na Stella Kalinga
Hatimaye
Hospitali ya Somanda iliyokuwa inamilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Bariadi
yakabidhiwa rasmi kwa Katibu Tawala Mkoa
wa Simiyu na kuwa Hospitali Teule ya
Rufaa ya Mkoa huo.
Makabidhiano
hayo yamefanyika kati ya Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Bariadi Melkizedek Humbe na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini
mjini Bariadi, mbele ya Uongozi wa Mkoa,
Halmashauri na baadhi ya watumishi wa Hospitali.
Katika
Makabidhiano hayo Katibu Tawala Mkoa amekabidhiwa baadhi ya watumishi na Mali
kutoka katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ambapo Sagini amesema watumishi
hao pamoja na wale waliokuwa wakisimamiwa na Katibu Tawala Mkoa hapo awali,
wote watasimamiwa na Sekretarieti ya mkoa wa Simiyu, chini ya uangalizi wa
Mganga Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa
Akizungumza
kabla ya makabidhiano hayo Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini
amewaasa watumishi wa Hospitali hiyo
kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanatoa huduma kwa wagonjwa kulingana na
taratibu, maadili na miongozo ya taalum ya kitabibu.
Sagini
amesema baadhi ya watumishi wa Idara ya afya wamekuwa wakitumia lugha mbaya
isiyowaridhisha wateja wao na hivyo kushindwa kuwapa huduma wanayostahili kwa
kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakikatishwa tamaa.
“Nisingependa
kusikia kuna watumishi wanatumia lugha mbaya kwa wagonjwa, wengine
wanapowahudumia mama wajawazito wanawatolea maneno makali ambayo hayawapi
faraja, tabia hiyo isionekane kabisa katika Hospitali yetu, zingatieni maadili ya kazi zenu na muwape
wananchi huduma wanayostahili ili waendelee kuwaamini’ alisema Sagini.
Aidha,
Sagini alimtaka Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Teule ya Mkoa, Dkt. Fredrick
Mlekwa ashirikiane na viongozi wengine kuhakikisha
Hospitali hiyo inatoa huduma bora zinazolingana na hadhi iliyonayo kwa sasa ili
wananchi wa Mkoa wa Simiyu wanufaike kwa kupata huduma bora za Rufaa.
Wakati
huo huo Mkurugenzi wa Halmasahuri ya Mji amewataka Watumishi waliokabidhiwa kwa
Katibu Tawala Mkoa watumie fursa hiyo kufanya kazi kwa bidii zaidi ili huduma itakayotolewa iendane na hadhi ya
Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Halmashuari ya Mji wa Bariadi, Mhe. Robert Lweyo
ametoa wito kwa Serikali kuu kuhakikisha inajenga majengo bora yatakayokuwa na
hadhi ya Hospitali ya Mkoa.
Naye
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Teule ya Rufaa ya Mkoa, Dkt. Fredrick Mlekwa
amesema Wananchi wa Halmashauri zote katika Mkoa wa Simiyu watarajie huduma bora
zitakazokidhi kiwango.
Kabla
ya Hospitali ya Somanda kuwa Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa ilikuwa
inahudumia wananchi kutoka katika Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri
Wilaya jirani za Bariadi, Itilima na baadhi
ya vijiji vya vya Wilaya ya Busega,
lakini kuanzia sasa itahudumia Halmashauri zote sita ikiwemo Maswa na Meatu kwa
huduma za Rufaa.
0 comments:
Post a Comment