Wednesday, September 28, 2016

NAIBU WAZIRI JAFO AFANYA ZIARA MKOANI SIMIYU

Na Stella Kalinga
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI  Mhe. Suleiman Jafo (Mb) amefanya ziara ya siku mbili Mkoani Simiyu

Akizungumza na  Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi  katika Ukumbi wa Alliance Mjini Bariadi,  Mhe. Jafo amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kukaa na wakuu wao wa Idara ili kupanga malengo yanayopaswa kutekelezwa kulingana na bajeti walizopanga katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Jafo amesema watumishi wengi wa Umma wamekuwa wakifanya kazi wa mazoea  hivyo wanapaswa kuweka malengo yanayopimika ili kila mwisho wa mwaka wapimwe kulingana na matokeo ya kazi zao kwa mujibu wa mifumo iliyopo ikiwa ni pamoja na Mfumo wa wazi wa mapitio na Upimaji Utendaji kazi (OPRAS) .

Aidha, Jafo amesema Wakurugenzi wanapaswa kuibua na kuvitumia  vipaji kwa watumishi walio tayari kuwatumikia wananchi kupitia taaluma zao badala ya kuwakatisha tamaa na kwa kudidimiza na kutotambua mchango wao.

Wakati huo huo Mhe. Jafo amewataka Wakurugenzi  kusimamia suala la upandaji madaraja kwa watumishi ili lifanyike kwa haki badala ya uonevu na upendeleo.

“Kuna baadhi ya maeneo watu wameajiriwa mwaka 2002,wengine 2003 lakini wanafanana mishahara na watu walioajiriwa mwaka 2012,2013 hawajawahi kupanda madaraja toka wameajiriwa, kwa kuwa kupanda daraja ni kwa upendeleo,mpaka mtumishi ajikombekombe kwa mkuu wa idara. Wakurugenzi kalisimamieni hilo, wakuu wa idara fanyeni kazi yenu, tengenezeni mnyororo wa ushirikiano vizuri ili watu wapande madaraja kwa haki zao.

Sanjari na hilo, Mhe. Jafo amewataka watumishi kutumia elimu na uzoefu walionao kubuni mambo mbalimbali yatayoleta mabadiliko katika maeneo yao na akawataka kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili thamani ya kila mmoja ionekane.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amewataka watumishi wa Mkoa huo kila mmoja kwa nafasi yake  kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri  huyo na  wafanye kazi zenye tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri yuko Mkoani Simiyu kwa ziara ya siku mbili ambapo atatembelea wilaya ya Busega, Bariadi, Itilima na Maswa na kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo na kuzungumza na Watumishi wa Serikali za Mitaa.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo(Mb) akizungumza na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Bariadi Mjini Bariadi, katika ziara yake Mkoani Simiyu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo(Mb) (kushoto)akizungumza na Watumishi wa Sekretaieti ya Mkoa, Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Bariadi (hawapo pichani)  Mjini Bariadi, katika ziara yake Mkoani Simiyu, (wa pili kushoto) Katibu Tawala Mkoa huo, Jumanne Sagini.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka, akizungumza kabla ya kumkaibisha  Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo(Mb)  azungumze na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Bariadi Mjini Bariadi.

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini (wa pili kushoto) akimkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Robert Lweyo (kulia) ili atoe neno la shukrani kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo(Mb)  baada ya kuzungumza na  Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Bariadi Mjini Bariadi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Robert Lweyo (wa pili kulia) akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo (Mb)  baada ya kuzungumza na  Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Bariadi (hawapo pichani)  Mjini Bariadi

Baadhi ya Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo(Mb) (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.




0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!