Na Stella Kalinga
Madiwani
na watendaji wa Halmashauri wameaswa kuacha kuingiza maslahi binafsi katika
ujenzi wa miradi ya barabara ili kufanya miradi kusimamiwa na kujengwa katika
kiwango kinachostahili.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka katika kikao cha
Bodi ya Barabara kilichofanyika katika Ukumbi wa kanisa Katoliki Mjini,
Bariadi.
Mtaka
amesema ili miradi ya ujenzi wa barabara isimamiwe vizuri na iweze kujengwa kwa
viwango vinavyotakiwa madiwani na watendaji wasiwe sehemu ya wazabuni au
wakandarasi wa miradi hiyo, ili waweze kuwasimamia wakandarasi wa miradi hiyo
na kuwachukulia hatua pale wanapotekeleza miradi chini ya kiwango.
Aidha,
Mtaka amewataka Wenyeviti wa Halmashauri kusimamia kwa umakini vikao vya
mabaraza ya madiwani vya kuamua matengenezo ya barabara ili kipaumbele cha
kwanza kiwe ni kwa barabara ambazo zimeharibika sana.
“Wenyeviti
wa Halmashauri waongozeni madiwani kuepuka ubinafsi katika miradi ya barabara
ambapo kila Diwani anataka apewe fedha kidogo kidogo ya kujenga au kukarabati
hata kama fedha hiyo ni kidogo sana. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni barabara ambazo
zimeharibika sana au hazipitiki kabisa katika Halmashauri” alisema Mtaka.
Sanjali
na hilo Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa ngazi zote kutoa elimu kwa
wananchi juu ya utunzaji wa alama za barabarani zinazowekwa na Wakandarasi na
Wakala wa Barabara(TANROADS) pamoja na kuacha kupitisha mifugo barabarani
ambayo inasababisha mmomonyoko wa udongo ili barabara zidumu.
Naye
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amesisitiza Wahandisi wa
Halmashauri kuhakikisha wanaweka alama katika mipaka ya hifadhi ya barabara ili
iwe rahisi kutambua na kuepuka maeneo hayo kuvamiwa na kutumiwa tofauti na yalivyokusudiwa.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Mhe. Satanslaus Nyongo amesema
Wakala wa Barabara(TANROADS) kwa kushirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Simiyu,
wafanye jitihada za kuzungumza na Waziri mwenye dhamana na ujenzi wa Barabara
ili kipande cha barabara cha Maswa hadi Bariadi chenye kilomita 50 kitengewe
fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami; kwa kuwa barabara ya
Mwigumbi-Maswa-Bariadi –Lamadi itakapokamilika itaweza kuunganisha Mkoa wa
Simiyu na mikoa mingine hivyo kuufungua kiuchumi.
Akizungumzia
barabara hiyo Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Barabara(TANROADS) Mhandisi Albert
Kent amesema kipande cha Lamadi-Bariadi kimekamilika, mkandarasi anaendelea na
ujenzi wa kipande cha Mwigumbi-Maswa na kipande cha Maswa hadi Maswa kitajengwa
kulingana na kadri kaitakavyotengewe fedha katika bajeti, kwa kuwa utekelezaji
wa mradi huo unategemea upatikanaji wa fedha.
Mkoa
wa Simiyu una mtandao wa barabara zenye jumla ya kilomita 4,730.95 ambazo
zimegawanyika katika makundi yafuatayo:-Barabara kuu kilometa 334.72, barabara
za Mkoa kilometa532.30, barabara za wilaya kilometa 2420.5 na barabara za vijijini
1451.53; kati ya hizi kilomita 141.76 zina kiwango cha lami, kilomita 2453.59
kiwango cha chanagarawe na kilometa 2134.7 za kiwango cha udongo.
Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Dkt. Titus Kamani akizungumza na Wajumbe wa Bodi
ya Barabara kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kupanga na kujadili
maendeleo ya Barabara katika Mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment