Na
Stella Kalinga
Wafanyabiashara Mkoani
Simiyu wamehimizwa kusajili na kurasimisha biashara zao ili zitambulike na waweze kupata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo.
Wito huo umetolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ufunguzi wa Semina ya
Uhamasishaji ya majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)
katika Ukumbi wa Mikutano wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi.
Mtaka amesema katika
kuunga mkono Juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli za kuifikia Tanzania ya Viwanda, Wakala wa Usajili wa Biashara
na Leseni (BRELA) wana nafasi kubwa ya kuwaandaa Watanzania kupokea mabadiliko
hayo na kuona umuhimu wa kusajili biashara zao.
Aidha, Mtaka amesema Mkoa
wa Mkoani Simiyu umedhamiria kuwa Mkoa wa mfano kwa kutekeleza, ambapo kwa sasa umeanza kuzalisha chaki na
maziwa na umejipanga kuanzisha viwanda vidogo
na vya kati vitakavyozalisha bidhaa ambazo malighafi yake yanapatikana
nchini ambazo ni bandeji, pamba za hospitali, pamba za hospitali na maji ya
dripu.
Mtaka amesema katika
mwaka 2016/2017 mkoa wa Simiyu utatimiza azma yake ya kila wilaya kuzalisha
bidhaa moja (one district one product) na biashara hizo zote zitasajiliwa na
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
“Nimesema, nimechagua
Mkoa wa Simiyu kuwa Mkoa kiongozi wa kuiongoza nchi hii kufikia malengo ambayo
watu huko Duniani wanatarajia kuyaona kupitia Mhe. Rais wa Tanzania, ningetamani kuona mkoa wa Simiyu unakuwa
miongoni mwa mikoa mitano ya mfano na ya kutumainiwa kibiashara nchini, haya
malengo tutayafikia kwa kushirikiana na ninyi” alisema Mtaka.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Itilima, Mhe. Njalu Silanga amesema endapo Wafanyabiashara watasajili na
kurasimisha biashara na makampuni yao wataepuka hasara zisizo za lazima kwa
kuwa wataajiri watu watakaowasaidia kuendesha biashara na makampuni yao
kitaalamu.
Naye Afisa Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Frank Kanyus amesema
wanaendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wafanyabiashara kusajili majina ya
biashara na makampuni nchini na Mkoa wa Simiyu umekuwa mkoa wa nne kufikiwa na
fursa hii.
0 comments:
Post a Comment