Thursday, October 13, 2016

VIJANA WAASWA KUACHA KULALAMIKA

Na Stella Kalinga
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana kuacha kuilalamikia Serikali na badala yake  wachukue hatua za utekelezaji.

Waziri Mhagama aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa Kongamano la Vijana Mkoa wa Simiyu lililofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili Nafasi ya Vijana katika Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda nchini.

 Waziri Mhagama amesema vijana wanapaswa kuacha kukaa vijiweni na wabuni miradi mbalimbali ya maendeleo ili Serikali iwawezeshe kwa kuwapatia mikopo ya kuendeleza Miradi hiyo kama walivyofanya vijana wa Wilaya ya Meatu na Maswa Mkoani Simiyu, ambao walipewa mikopo na wizara  na kuanzisha kiwanda cha chaki na maziwa.

“ Vijana acheni kulalamika , onyesheni uwezo wenu Serikali iko tayari kuwaunga mkono; tumetoa mkopo wa shilingi 38,000,000 kwa vijana wa Maswa waliokuwa tayari wameshafungua kiwanda cha kutengeneza chaki, Meatu walipewa shilingi 31,000,000 wamefungua kiwanda cha kusindika maziwa, Simiyu wameweza na mikoa mingine chukueni hatua” alisema Mhagama.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mhagama Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka alisema mkoa wake kupitia kauli mbiu ya “Wilaya moja bidhaa moja”umedhamiria kuzalisha bidhaa ambazo malighafi yake yanapatikana hapa nchini.

Mtaka alisema katika kutimiza azma ya Kila wilaya kuzalisha bidhaa moja wilaya ya Maswa imeanza kutengeneza chaki, Meatu kusindika maziwa na wilaya ya Itilima, Busega na Bariadi zinaendelea kubuni na kuendeleza mradi.  

Pamoja na kuzalisha chaki na maziwa mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine unajipanga kuanzisha kiwanda cha kuzalisha mahitaji yatokanayo na pamba kama vile bandeji, pamba za masikioni, pamba za hospitali kwa kuwa Mkoa huo ni wa tatu kwa uzalishaji wa pamba nchini.

Aidha, Mkoa una mkakati wa kuziongezea thamani bidhaa zote zitokanazo na kilimo na mifugo kama  vile mazao ya nafaka na mikunde, ngozi na nyama ambapo kwa upande wa mifugo maziwa tayari yameshaanza kusindikwa Wilaya ya Meatu.

Akizungumza katika Kongamano hilo  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Sera za kiuchumi na Kijamii (ESFR) ametoa wito kwa vijana kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa fursa zipo katika nyanja mbalimbali ili watimize wajibu wao katika kubuni miradi hususani viwanda vidogo vidogo.

Kongamano la vijana Mkoani Simiyu lilihusisha vijana kutoka idara na taasisi mbalimbali,vyuo vikuu, vikundi vya wajasiriamali kutoka sehemu mbalimbali nchini ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na Mageuzi ya kiuchumi yanayohitajika kuboresha maisha ya vijana, Fursa za Vijana katika Uchumi wa Viwanda, umuhimu wa viwanda vidogo vidogo katika maendeleo ya viwanda nchini, fursa mpya katika kilimo Biashara na kadhalika.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akiwa amesimama katikati ya mabango ya Chaki za Maswa na Maziwa ya Meatu bidhaa ambazo zinazalishwa chini ya Kauli mbiu ya Mkoa huo ya “Wilaya moja bidhaa moja”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akipokea zawadi ya mafuta kutoka kwa kijana mjasiriamali kutoka Mkoa wa Lindi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na viongozi wa Mkoa wa Simiyu kabla ya kuanza Kongamano la Vijana wa Mkoa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Sera za kiuchumi na Kijamii (ESFR) Dkt. Tausi Kida akitoa mada kwa washiriki wa kongamano la Vijana wa Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (wa tatu kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa nne kushoto) wakiteta jambo kabla ya Kongamano la Vijana wa Mkoa huo kufunguliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Sera za kiuchumi na Kijamii (ESFR) Dkt. Tausi Kida na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ufunguzi wa Kongamano la Vijana wa Mkoa wa Simiyu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na vijana wa mkoa wa Simiyu katika kongamano la mkoa la vijana hao.
Mkuu wa Wilaya ya Masw, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe akiwakaribisha washiriki wa Kongamano la Vijana Mkoa wa Simiyu lililofanyika Mjini Bariadi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi (Mwenyeji) , Mhe. Festo Kiswaga.
Baadhi ya washiriki wa kongamano la Vijana Mkoa wa Simiyu wakfuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa.
Kutoka kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Sera za kiuchumi na Kijamii (ESFR) Dkt. Tausi Kida, Waziri Jenista Mhagama, Mwakilishi wa Katibu Mkuu UN, Amoni Manyama, Naibu Waziri Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde na Mmoja wa Wawasilisha mada.    
Baadhi ya washiriki wa kongamano la Vijana Mkoa wa Simiyu wakfuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!