Na
Stella Kalinga
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa
Simiyu na Taifa kwa ujumla kushiriki katika Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru,
Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana mwaka
2016, yatakayofanyika mkoani humo.
Akizungumza
na waandishi wa Habari Ofisini kwake Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu umepewa
heshima ya kuwa mwenyeji wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya
kifo cha Baba wa Taifa na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yatakayofanyika Oktoba
14, 2016 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mtaka
ameeleza kuwa Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye
pia atashiriki Ibada ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwl.
Julius Kambarage Nyerere, itakayofanyika siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016
katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yohana, Mjini Bariadi kuanzia saa 1:00
kamili asubuhi.
Wakati
huo huo Mtaka amesema maadhimisho ya wiki ya vijana yatafunguliwa rasmi tarehe
08 Oktoba, 2016 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) katika Uwanja wa SABASABA
Mjini Bariadi; ambapo shughuli mbalimbali za vikundi vya maendeleo ya vijana
kutoka Halmashauri zote nchini zikiwemo za ujasiriamali pamoja na ugunduzi wa
kisayansi ambao umethibitishwa na Tume ya Taifa ya Sayansi zitaoneshwa katika
mabanda maalum yaliyojengwa katika uwanja huo.
“Kwa upande mkoa wa Simiyu vikundi vyetu vya
vijana vimejiandaa kuonesha shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa katika
Halmashauri husika;ambapo kimkoa tunatekeleza mkakati wa kila wilaya kuzalisha
bidhaa/huduma moja yaani (one district one product). Kulingana
na mkakati huo Vijana wa Wilaya ya Meatu wameanzisha kiwanda cha kusindika
maziwa ya ng’ombe, Maswa kiwanda cha kuzalisha chaki na wilaya nyingine
tunaendelea kujipanga kuzalisha bidhaa nyingine” alisema Mtaka.
Aidha,
Mtaka amewakumbusha wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Maadhimisho haya ni fursa
kwao kiuchumi na kijamii kwa kuwa watapokea wageni wengi kutoka maeneo
mbalimbali nchini ambao watahitaji malazi, chakula na huduma nyingine muhimu,
hivyo waoneshe ukarimu na ushirikiano wa hali ya juu ili kuupa heshima mkoa
huo.
Naye
Pendo Benjamin Mkazi wa Mtaa wa Sima mjini Bariadi amesema amepokea kwa furaha
suala la kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kufanyika mkoani Simiyu kwa kuwa ni
la kihistoria, pia ni fursa kwa wafanyabiashara wa vyakula, nyumba za kulala
wageni na mahitaji mengine.
Sanjali
na hilo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi
kuchangia damu kwa hiari katika uwanja wa SABASABA kuanzia tarehe 08/10/2016
hadi 13/10/2016, zoezi ambalo litafanywa na Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa
kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu na Shirika la AGPAHI kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji wa
damu hususani mama wajawazito, majeruhi wa ajali na watoto wenye umri chini ya
miaka mitano.
Kilele
cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa na
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana kwa mwaka 2016 ni tukio la kihistoria kwa Mkoa wa
Simiyu na la kwanza kwa Mhe.Rais wa awamu ya tano tangu alipopata ridhaa ya
wananchi kuliongoza Taifa letu.
Sehemu
ya Jengo la Ofisi ya Vijana wa Wilaya ya Meatu wanaojishughulisha na usindikaji
wa maziwa (MEATU MILK)
|
0 comments:
Post a Comment