Thursday, December 28, 2017

PROFESA NDALICHAKO: WIZARA YA ELIMU HAINA URASIMU KUSAJILI SHULE IKIWA VIGEZO VIMEZINGATIWA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Wizara yake haina urasimu wowote katika usajili wa shule ikiwa vigezo vyote vinavyotakiwa vimezingatiwa katika uanzishwaji wa shule hizo.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo jana wakati alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika Shule Shikizi/tarajali ya Njalu iliyopo Habiya Wilayani Itilima na alipotembelea shule ya Sekondari ya Chegeni inayoendelea kujengwa Kijiji cha Bulima wilayani Busega,  zote zikiwa zinajengwa kwa nguvu ya wananchi.

 “Lengo la Serikali ni kuwa na shule nyingi lakini ni lazima vigezo na masharti yaliyowekwa na Wizara yazingatiwe; Kuna watu ambao siyo waaminifu, zamani ilikuwa hata mtu akiwa na madarasa matatu akiomba usajili anaruhusiwa na shule inasajiliwa lakini wakisharuhusiwa wanabweteka na matokeo yake wanaleta shida kwa watoto wetu” alisema Profesa Ndalichako.

Ameongeza kuwa Wadhibiti ubora wapewe nafasi ya kushiriki katika vikao vya Mabaraza ya madiwani ili waweze kutoa elimu na mwongozo kwa madiwani juu ya mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa wanapotaka kuanzisha shule katika maeneo yao na wataalam wa elimu wasaidie katika kutoa elimu juu ya miongozo na vigezo vyote.

Aidha, amewapongeza wananchi wa Habiya Itilima na Bulima Busega kwa kuchangia nguvu na michango yao katika  kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli kwenye ujenzi wa shule hizo na akawataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda wasiwape majukumu mengine.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mbunge wa Itilima Mhe.Njalu Silanga na Mbunge wa Busega, Mhe.Dkt.Raphael Chegeni wamesema wananchi katika maeneo zilizopo shule hizo wako tayari kuunga mkono Juhudi za Serikali katika ujenzi wa shule,  hivyo wakaomba watakapokamilisha ujenzi wa miundombinu kulingana na miongozo waliyopewa wasajiliwe shule hizo ili kutoa nafasi kwa watoto kupata mahali pa kujifunzia.

“Mhe.Waziri tunakubali kufuata maelekezo yako na tunaomba tutakapo kamilisha mahitaji tunaomba shule hii iweze kusajiliwa na katika Jimbo langu kuna shule 22 za aina hii ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi” alisema Njalu Silanga Mbunge wa Itilima.

Pamoja kutoa maelekezo na mwongozo kwa wananchi Mhe. Waziri wa Elimu ameahidi kuchangia ujenzi wa shule hizo kwa kutoa saruji mifuko 100 kwa Shule ya Njalu(Itilima) na Mifuko 150 kwa Shule yaChegeni (Busega) na kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kuhakikisha kuwa wanatafuta vifaa vingine ili kukamilisha miundombinu inayotakiwa kwa kushirikiana na wananchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Itilima itachangia  saruji mifuko 100 kwa shule ya Msingi (shikizi) Njalu (Itilima) na Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Busega itachangia mifuko 50 kwa Shule ya Sekondari Chegeni(Busega) .

Shule ya Msingi Njalu (Shikizi) hadi sasa ina vyumba vya madarasa vitano, ofisi moja ya walimu  na ina upungufu wa chumba kimoja cha darasa, ofisi ya walimu 01 pamoja na matundu ya vyoo matano (05) na mpaka sasa Mbunge wa Jimbo la Itilima ametoa zaidi ya milioni 26.


Kwa upande wa   Shule ya Sekondari ya Chegeni inayoendelea kujengwa mpaka sasa  ina vyumba viwili vya madarasa, ofisi moja ya walimu, ina upungufu wa vyumba viwili vya madarasa, vyumba vitatu vya maabara, matundu 10 ya vyoo, maktaba, jengo la utawala na nyumba mbili za walimu ambapo hadi sasa Mbunge wa Busega Dkt.Raphael Chegeni ameshangia jumla ya shilingi  milioni 10 katika kuwaunga mkono wananchi. 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Bulima Kata ya Nayashimo Wilayani Busega Mkoa waSimiyu wakati wa ziara yake mkoani humo.
Mbunge wa Jimbo la Busega Mhe.Dkt.Raphael Chegeni akizungumza na wananchi wa Bulima wakati Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako alipotembelea shule ya Sekondari inayojengwa kwa nguvu za wananchi ambayo imepewa jina la Mbunge huyo (Chegeni Sekondari) jana.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako(kulia) akiweka Jiwe la Msingi Vyumba vya Madarasa  vya Shule ya Msingi iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kupewa jina la Mbunge Njalu(Shule ya msingi Njalu) iliyopo Habiya wilayani Itilima wakati wa ziara yake jana.
Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe.Njalu Silanga akizungumza katika uwekaji wa Jiwe la Msingi la Vyumba vya Madarasa Shule ya Msingi Njalu (Shule shikizi) iliyoko Habiya wilaya ya Itilima wakati wa Ziara ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako wilayani humo jana
Diwani ya Kata ya Nyashimo na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega akizungumza na wananchi wa Bulima wakati Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako alipotembelea shule ya Sekondari inayojengwa kwa nguvu za wananchi ambayo imepewa jina la Mbunge wa Busega Dkt.Raphael Chegeni (Chegeni Sekondari) jana.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bulima Kata ya Nyashimo wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako wakati alipopita kuona ujenzi wa shule ya sekondari Chegeni ambayo inajengwa kwa nguvu ya wananchi hao wilayani Busega.
Kutoka kushoto Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Diwani ya Kata ya Nyashimo na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mickness Mahela, Mkurugenzi Busega na Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu wakifurahia jambo wakati wa Ziara ya Waziri wa Elimu wilayani Busega.
Kutoka kushoto Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako wakiteta jambo wakati wa ziara ya Mhe.Waziri wa Elimu wilayani Itilima jana.
Kutoka kushoto Mbunge wa Jimbo la Busega Mhe.Dkt.Raphael Chegeni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Joyce Ndalichako, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mickness Mahela, Mkurugenzi wa Busega Anderson Njiginya wakifurahia jambo  wakati wa Ziara ya Waziri wa Elimu wilayani Busega.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Habiya mara baada ya kukwa nguvu ya wananchi  katika Shule ya msingi Njalu(Shule shikizi) wakati wa ziara yake wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!