Wednesday, December 6, 2017

SIMIYU YAJIPANGA KUVUNA TANI 490,000 ZA PAMBA MWAKA 2018

Mkoa wa Simiyu unatarajia kuvuna takribani tani 264,000 sawa na kilo milioni 264 hadi tani 490,000  sawa na kilo milioni 490 za zao la pamba, katika msimu wa mwaka 2017/2018 kutoka kilo milioni 70 za mwaka 2016/2017.

Hayo yamesemwa  na Afisa Kilimo Ofisi Mkuu  wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Elias Kasuka  katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa(RCC) kilichofanyika Mjini Bariadi.

Kasuka  amesema  mkoa wa Simiyu una jumla ya wakulima wa pamba 301, 000 watakaolima pamba katika msimu huu, katika eneo la zaidi ya ekari 700,000 huku matarajio ya mavuno yakiwa ni zaidi ya kilo 700 kwa ekari moja.

Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka amesema Watalaam wa Kilimo wa Mkoa na Wilaya waandae mipango kazi yao itakayoonesha ratiba ya kuwatembelea wakulima wa pamba katika kipindi chote cha msimu tangu kupanda mpaka watakapovuna, ili malengo hayo ya kuongeza mavuno yaweze kutimia.

Mtaka ameongeza kuwa Zao la pamba linachangia kwa kiasi kikubwa mapato kwa Halmashauri za Mkoa huo, hivyo Wakurugenzi wanapaswa kuhakikisha Maafisa Kilimo wanawezeshwa muda wote wanaohitaji kuwafikia wakulima katika kipindi cha msimu wa kilimo badala ya kusubiri wakati wa ukusanyaji ushuru baada ya mavuno.

“Wakurugenzi nilishawaambia Uhai wa Halmashauri zenu uko kwenye ushuru wa pamba hakikisheni Maafisa Kilimo wanawezeshwa kuwafikia wakulima; Wakuu wa Wilaya pia  kagueni mashamba ya pamba kwenye maeneo yenu. Wenyeviti wa Halmashauri niwaombe tusichangamkie pamba wakati inapovunwa tu, tuichangamkie hata pale inapokuwa shambani, tuwaone wananchi wanapolalamika kuwa mbegu hazijaoota au dawa hii haiuwi wadudu”alisisitiza Mtaka.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe ameomba Uongozi wa Mkoa kuwasiliana na Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba ili wakulima ambao hawajapata mbegu za pamba katika baadhi ya maeneo wapate haraka kabla ya msimu wa upandaji kuisha.

Akiwasilisha taarifa ya  Maendeleo ya Sekta ya Kilimo , Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt.Gamitwe Mahaza amesema hadi kufikia Oktoba 30 mwaka huu jumla ya tani 3,628.727 za mbegu za pamba zilikuwa zimeshasambazwa sawa na wastani wa asilimia 48.0 ya lengo la kusambaza tani 7,485.400.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema  Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imetenga fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Majengo ya Ofisi na Karakana za Shirika la Maendeleo ya Viwanda VidogoVidogo (SIDO) Mkoani humo, ambayo yanatarajiwa kuanza kujengwa mwishoni mwa mwaka huu katika eneo la Isanga Bariadi Mjini na Mkandarasi ambaye ni SUMA JKT ameshafika kuona eneo husika.

Amesema Serikali inakusudia kujenga SIDO ya kisasa itakayokidhi mahitaji yanayoendana na wakati ikiwa ni pamoja na  kuwa mahali sahihi pa makundi muhimu hususani vijana na wanawake kupata mafunzo ya kuendesha shughuli zao za uzalishaji na viwanda vidogo.

“ Kila DC , Diwani tunapoenda kujenga SIDO kwenye Mkoa wetu,changamkia fursa, wananchi katika maeneo yenu waje na miradi ya viwanda vidogo vidogo, Tumeongea na Baraza la Taifa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na wadau wengine kuhusu miradi hii  midogo midogo; tuna uzalishaji wa viatu vya ngozi Busega, Bariadi na Maswa, tunataka kila kikundi kiende kwenye uzalishaji wa eneo lake la umahiri katika bidhaa za ngozi “ alisema.  

Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya Mkoa huo ya Wilaya moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja(One District One Product-ODOP) na umedhamiria kuanza kutekeleza mpango wa Bidhaa Moja Kijiji Kimoja(One Village One Product-OVOP)
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akifungua kikao cha Kamati yaUshauri ya Mkoa huo(RCC), kilichofanyika jana Mjini Bariadi, (kushoto)Mbunge wa Bariadi Mhe. Andrew Chenge,(wa pili kushoto) Katibu Tawala mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini na ( kulia) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dkt.Gamitwe Mahazaakiwasilisha Taarifa ya Mkoa ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!