Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka ametoa wito kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA) Mkoani humo
kusimamia utekelezaji wa Miradi ya ujenzi
wa barabara na madaraja kwa kuzingatia weledi.
Mtaka ametoa wito huo wakati akifungua
kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa huo, kichofanyika leo Mjini Bariadi
Mkoani humo.
" Nawaomba TARURA mfanye kazi kwa
kuzingatia weledi, siyo madaraja yanajengwa mnapeleka karavati zinavunjika
kabla daraja halijajengwa, mahali pa kuweka kokoto mnaweka udongo,
mtaidhalilisha taaluma; ningeomba mzingatie weledi kwa sababu mkifanya vibaya
wananchi watatushtaki watasema tumeanzisha wakala ambaye hana maana kwao"
amesema Mtaka.
Ameongeza kuwa Uongozi wa Mkoa wa Simiyu
haujapata shida juu ya miradi ya barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara
Nchini (TANROADS), hivyo ipo haja pia kwa TARURA kusimamia utekelezaji wa
miradi yake katika ubora, kwa kuwa Miradi hiyo imeondolewa katika
Halmashauri (Mabaraza ya Madiwani) na kupelekwa TARURA, ili ipangiwe
mipango na kusimamiwa na wataalam pekee kwa lengo la kuonesha utofauti
kiutendaji na umuhimu wa Wakala huo katika kuwapa huduma bora wananchi.
Wakati huo huo Mtaka
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kutoa shilingi Bilioni 86.1 kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara ya
Bariadi -Maswa yenye urefu wa Kilomita 49.7 kwa kiwango cha lami, ambayo
amesema ikikamilika itaifanya Bariadi na Maeneo mengine ya Mkoa huo kama
Malampaka(Maswa) kuwa maeneo ya kibiashara.
Aidha, amewataka Wakurugenzi
wa Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri ya Wilaya Maswa kutumia fursa hiyo
kujenga vituo vya mabasi vya kimkakati vitakavyoendana na kasi ya uingiaji wa
magari mengi baada ya kukamilika kwa barabara ya Maswa-Bariadi na Ujenzi wa
Reli ya “Standard Gauge” na Bandari kavu
itakayojengwa Malampaka wilayani Maswa.
Akiwasilisha taarifa ya barabara
zinazosimamiwa na TANROADS, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Albert
Kent amesema Barabara ya Bariadi-Maswa itajengwa kwa kutumia fedha za
Serikali ya Tanzania na itachukua muda wa miezi 24 mpaka kukamilika kwake,
ambapo amebainisha kuwa Mkandarasi Kampuni ya M/s CHICO ameshawasili eneo la
kazi(site).
Kwa upande wake Katibu
Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini ameomba wazo la marekebisho ya
Viwango vya fedha zinazotakiwa kwenda TANROADS na TARURA ambalo lilitolewa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, lifanyiwe kazi ili TARURA wapate fedha
na kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusaidia barabara za Halmashauri zisife.
Sagini ameongeza kuwa Halmashauri
zishirikiane na TARURA kutafuta namna ya kuzifanyia matengenezo barabara za
Vijiji ambazo haziko chini ya usimamizi wa wakala huo (TARURA), lakini ni za muhimu kwa maendeleo ya wananchi hususani
zinazounganisha vijiji ili kurahisisha mawasiliano kati ya kijiji na kijiji.
Meneja wa TARURA Mkoa wa
Simiyu,Mhandisi Peter Mosha amesema mwaka 2017/2018 Mkoa huo umeidhinishiwa
zaidi ya shilingi bilioni sita kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye mtandao
wa barabara wenye jumla ya kilomita 1780.87 , madaraja na makaravati katika
Halmashauri zote sita za Mkoa kulingana na mahitaji na mpango wa bajeti wa
Halmashauri husika.
Naye Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,
Mhe. Mashimba Ndaki amesema Wakala wa Barabara (TANROADS) unapaswa kuhakikisha
barabara zote zinawekewa vivuko ili kuwasaidia wananchi kuvuka kwa
usalama.
Akipongeza kazi inayofanywa na TANROADS
Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga ameomba TANROADS
kuona namna ya kufanyia kazi kona nyingi zilizopo katika barabara ya
Bariadi-Lagangabili-Kisesa pamoja na kuangalia upanuzi wa barabara
mbalimbali zinazosimamiwa na Wakala huo ili zisisababishe uharibifu wa magari.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Barabara
ya Mkoa huo(hawapo pichani) katika Kikao cha bodi hiyo kilichofanyika jana
Mjini Bariadi, (kushoto) Katibu Tawala Mkoa, Ndg.Jumanne Sagini na Mkuu wa
Wilaya ya Bariadi,Mhe.Festo Kiswaga(kulia)
Meneja wa Wakala
wa Barabara Mijiji na Vijijini(TARURA) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Peter Mosha
akiwasilisha taarifa ya wakala huo(Mkoa) kwa Wajumbe wa Bodi ya Barabara katikakikao
cha bodi hiyo kilichofanyika Mjini Bariadi.
Meneja wa Wakala
wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Albert Kent akiwasilisha
taarifa ya miradi inayosimamiwa na wakala huo Mkoani humo, katika Kikao cha
Bodi ya Barabara kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya
ya Maswa Mhe.Dkt. Seif Shekalaghe akichangia hoja katika Kikao cha Bodi ya
Barabara Mkoa wa Simiyu kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mbunge wa Jimbo la
Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki akichangia hoja katika Kikao cha Bodi ya
Barabara Mkoa wa Simiyu kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Baadhi
ya Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu wakifuatilia hoja mbalimbali
zilizokuwa zikiwasilishwa katika Kikao Bodi hiyo kilichofanyika leo Mjini
Bariadi
0 comments:
Post a Comment